AKILIMALI: Kujiamini kumemfanya awe hodari katika ufugaji-biashara

AKILIMALI: Kujiamini kumemfanya awe hodari katika ufugaji-biashara

Na SAMMY WAWERU

VERONICA Wamuyu Kihagi ni mama mwenye bidii za mchwa, watoto wake sita akiwalea kupitia mapato ya ufugaji mbuzi wa maziwa.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, kijiji cha Kirurumo, Muruguru, Kaunti ya Nyeri, uliko mradi wake, alisema kwa kiasi kikubwa wanawe amewasomesha kupitia ufugaji.

Ni shughuli ambayo hakuiingilia leo, jana wala juzi, ila alipoolewa na mume wake, Mzee Ernest Kihagi.

Alilelewa katika mazingira ya mbuzi, na miaka kadhaa baada ya kupata boma aligeuza uzoefu huo kuwa biashara.

Akichanganua kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii, hasa katika sekta ya kilimo-ufugaji-biashara, Wamuyu anasema mama ana ushawishi mkubwa katika maendeleo ya boma.

Hata ingawa amekula chumvi, kinyume na miaka ya awali ambapo sauti ya mwanamke ilikuwa dhaifu na nyonge katika jamii, anasema dhana hiyo sasa imepitwa na wakati.

“Hamasisho kwa mwanamke, hususan kimasomo na kimaendeleo ni kuboresha jamii na taifa kwa jumla,” Wamuyu anasema.

Huku akikiri binti zake watatu, wameiga nyayo zake katika ufugaji wa mbuzi wa maziwa, nyama na wa kuuza, mama huyu anasema mizozano kwenye ndoa itakuwa haba endapo wanawake watawajibika kwa kutafuta njia mbadala kujiendeleza kimaisha.

Chaguo la mbuzi, kwa mujibu wa maelezo ya Wamuyu ni mojawapo ya miradi ambayo wanaweza kukumbatia.

“Kwanza, zizi lisiwe kisingizio. Mbuzi hawahitaji kipande kikubwa cha makazi,” asisitiza.

Aidha, kuna wakazi wa mijini wenye ari ya mbuzi wamefanikisha ufugaji.

Kulingana na Joseph Mathenge, anayeendeleza ufugaji wa mbuzi wa maziwa wa kisasa eneo la Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, kilomita chache kutoka Thika Superhighway, zizi lenye urefu wa futi 30, upana futi 8 na futi 13.7, kimo kuenda juu, lina uwezo kusitiri karibu mbuzi 20.

“Baada ya kuzingatia vigezo faafu vya ujenzi, ligawanye liwe na sehemu ya wale wa kukama, wanaojitayarisha kujifingua, beberu na vibuzi,” Mathenge ashauri.

Mfugaji huyu mwenye tajiriba ya muda mrefu, anasema kwenye paa unaweza kutengeneza eneo maalum kuhifadhi malisho.

Mtazamo wake si tofauti na wa Veronica Wamuyu.

Kando na chakula cha madukani, mama huyu hukuza nyasi za mabingobingo (napier), nyasi zinginezo na majani salama ya mimea.

“Nina mashine ya kusaga malisho mabichi, ambapo huyachanganya na madini yenye virutubisho faafu vya mifugo,” anadokeza.

Mfumo wa mashine za kusaga malisho ya mifugo, unasifiwa kusaidia kupunguzia wakulima gharama.

Aidha, kuna zinazotumia nguvu za umeme, nguvu za kawi (jua), mafuta ya petroli na zingine huzungushwa kwa mikono.

“Nikifanya hesabu, kwa siku mbuzi mmoja humpa kikombe kimoja pekee cha chakula cha madukani,” Wamuyu anasema.

Dkt Josphat Muturi, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya afya ya mifugo, CKL Africa Ltd – Kampuni ya kutengeneza madini, anashauri wafugaji kukumbatia matumizi ya nyasi za Fodder.

Zinajumisha lucerne, hay, silage, Desmodium na majani ya nafaka kama vile mahindi.

“Zikaushwe kiasi. Zina ukolevu wa kiwango cha juu cha virutubisho, hivyo basi kuchangia ongezeko la uzalishaji maziwa,” Dkt Muturi, na ambaye ni meneja wa masuala ya afya ya mifugo CKL Africa Ltd, anaelezea.

 

Beberu ambaye Veronica Wamuyu Kihagi alitunukwa na serikali ya Kaunti ya Nyeri. Picha/ Sammy Waweru

Mengine muhimu, ni usafi wa mazingira, kuzingatia matibabu ili kukabili kero ya magonjwa na vimelea, na kuhakikisha maji yapo kwa wingi na safi.

“Muda ambao nimekuwa katika ufugaji wa mbuzi, nimejaribu kadri niwezavyo kuzingatia usafi, malisho bora, na chanjo kila baada ya miezi mitatu. Athari za wadudu na magonjwa zinakuwa finyu,” Veronica Wamuyu anasema.

Ni kutokana na bidii za mama huyu, jitihada zake zimetambuliwa katika ngazi ya kaunti na kitaifa.

Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki wakati akiwa madarakani na Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, wamempa Wamuyu na mume wake, Ernest Kihagi tuzo kufuatia upekee wao katika ufugaji wa mbuzi wa maziwa .

Serikali ya Kaunti ya Nyeri, kupitia Gavana Mutahi Kahiga pia imewatambua kwa kumpa beberu wa kujamiisha.

“Anachoweza kufanya mwanamume, mwanamke pia atakifanya bora,” Wamuyu asema, akihimiza kina mama wenza kutolaza damu katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Anasema mizozano inayoshuhudiwa kwenye ndoa, mwanamke akijituma kufanya kazi itaweza kuangaziwa.

“Changamoto nyingi katika ndoa zinachangiwa na mmoja wa wanandoa kutokuwa na chanzo cha mapato.

“Wote wakiwa na kazi, amini usiamini zitapungua na kila mmoja kutekeleza majukumu yake. Ufugaji ni miongoni mwa miradi ambayo wanawake wanaweza kujiimarisha nayo,” asema, akisisitizia mchango wa mama kwenye familia.

You can share this post!

Malalamiko tele chombo cha kukagua mizigo kikiharibika...

Agala na Makokha wabanduliwa kwenye voliboli ya ufukweni...