Makala

AKILIMALI: Kuku si kitoweo tu, ni kitega uchumi murua

September 10th, 2020 5 min read

PHYLLIS MUSASIA na CHRIS ADUNGO

WATU wengi nchini wanaendesha ufugaji wa kuku lakinisi kila mmoja anayefaulu muda anapojitosa katika biashara hiyo.

Alipoanza mradi wa kufuga kuku wa kienyeji miezi mitano iliyopita, Isaac Achola alinuia kujipatia shughuli ya kufanya nyumbani badala ya kukaa bure.

Hii ni baada ya janga la corona kusitisha shughuli nyingi nchini ikiwemo nafasi za biashara ya kazi aliyofanya awali.

Mtaalamu huyo wa maswala ya kudhibiti wadudu, alianza mradi wa kuku mapema mwezi wa nne mwaka huu, kwa kuku 100 pekee.

Muda mchache baadaye, idadi ya kuku wake imeongezeka zaidi ya mara nne na kumwezesha kupata wazo la kushiriki kilimo biashara.

“Baada ya kuanza na kuku 100, bidii niliyokuwa nayo ilifanikisha mradi huu na idadi ya kuku kuongezeka na sasa wengi wao wako tayari kwa soko,” anasema.

Kufikia wakati huu, Achola wa eneo la Imani mjini Nakuru, anafuga kuku wa kienyeji walioboreshwa 450, bata mzinga 70 na ndege wa Guinea wanane.

“Nilipoona kwamba ndege wangu wanaendelea vyema, nilitafuta ujuzi zaidi wa kilimo cha kuku kutoka kwa wataalam wa kampuni ya mashamba ya Bidco O’lake hapa Nakuru. Walinipokea vyema na kunielimisha kuhusu mbinu bora zaidi,” akasema.

Achola alitumia takribani Sh260, 000 kujenga nyumba ya kuku hao pesa ambazo zilitumika kununua mabati, mbao, waya ya kuku miongoni mwa vifaa vinginevyo. Kwenye awamu ya kwanza, vifaranga 100 walimgharimu Sh8, 000. Mradi huo, Achola anasema ni wa familia yake ambapo mkewe Shilla Chepkemoi na watoto wao wawili husaidiana kuwashughulikia kuku hao.

“Wakati huu kila mmoja wetu ana kazi ya kufanya ili kuchangia ukuaji wa mradi. Tumegawana majukumu na kila tunapoamka asubuhi, sisi hubidiika ipasavyo,”anaeleza.

Alieleza kuwa, “Kunao yule ambaye hufagia na kusafisha nyumba ya kuku, mwingine huosha vifaa vya chakula kabla ya lishe, kuangalia vifaranga na pia kukusanya mayai.”

Kwa siku moja, Achola hukusanya kati ya mayai 50 na 60 ambapo huuza kila yai kwa Sh15. Kreti moja, yeye huuza kwa Sh450 haswa katika maduka ya eneo analoishi.

Ili kuongeza idadi ya kuku, wale ambao wameshataga mayai hukaa kwenye mayai yao kwa muda wa siku 21 ili kupata vifaranga.

Aidha, Achola hununua vifaranga wengine kutoka kampuni ya Sasso.

Kuku wake ni wa rangi na hukomaa kati ya miezi mitatu na nne.

Vifaranga wakiwa bado wadogo, huwalisha chakula ambacho kimetengezwa hususan kutumika na vifaranga kwa kipindi cha wiki sita. Baadaye hubadilisha chakula na kuwapa lishe ya kuwasaidia kuendelea kukua wanapotimiza wiki 20.

Kuku hao baadaye hupewa lishe ya mwisho ambayo huwasaidia kutaga mayai ingawa sasa hutegemea ikiwa ni wa kutaga au wa nyama.

“Vyakula hivi vyote huwa vya kununuliwa japo vya kienyeji. Kuku wanapaswa kula kwa muda wa masaa mawili kisha uwaachilie watafute nyasi, wadudu na vyakula mbadala kule nje,” anasema.

Achola anaeleza kuwa bata mzinga husaidia kulinda kuku na huhakikisha kwamba wote wako salama.

Yeye huuza yai moja la bata kwa Sh150.

Ingawa analenga maduka ya jumla na hoteli kama soko yake kuu, anasema tayari ameanza kuuza jogoo ambao wako tayari kwa watu binafsi, kwa Sh1, 200.

Kwa muda wa mwaka mmoja, anatazamia kupanua mradi huo na kufuga kuku 3, 000.

Baadhi ya changamoto anazopiti ni pamoja na kuzuia magonjwa kama vile Newcastle na Gumboro.

Bw Achola alisema hunyunyuzia dawa katika nyumba ya kuku hao kila baada ya wiki tatu ili kuzuia wadudu.

Anasema alichagua kufuga kuku wa kienyeji walioboreshwa kwa sababu ni rahisi kuwalinda na kwamba wanastahimili magonjwa.

Aidha, wao hukomaa haraka na uzani wao huwa mwingi ikilinganishwa na kuku wengine.Achola hayuko pekee yake katika ufiugaji huu. Humu nchini wengi wameingilia ufugaji kuku.

Katika eneo la Kibomet kwenye Barabara Kuu ya Kitale kuelekea Kapenguria katika Kaunti ya Trans-Nzoia, tunakutana na Mary Wamaitha Mwangi ambaye ni mfugaji wa kuku.

Yeye amejitosa katika ulingo wa ufugaji wa kuku wa kienyeji ambao anasema wakitunzwa vyema, wana faida kubwa.

Kulingana naye, kwa muda mrefu, amekuwa akijihusisha na kazi za ufugaji wa ng’ombe na kuku pamoja na kilimo cha mahindi lakini katika miaka ya hivi karibuni, amekuwa akijituma sana katika ufugaji wa kuku pamoja na kilimo cha matunda baada ya kuona kuwa kilimo cha mahindi kina matatizo na changamoto tele.

Anasema kuwa ufugaji wa kuku hauna kazi nyingi na tena huwa unaleta mapato ya kila mara. Wamaitha na mumewe walipokata shauri ya kutilia mkazo ufugaji wa kuku, waliamua ya kuwa watatumia mbinu mpya ya ufugaji tofauti na walivyokuwa wamezoea hapo awali.

Mnamo mwezi wa Novemba mwaka jana, walinunua vifaranga 100 kutoka kwa kampuni moja iliyoko mjini Thika pamoja na mashine ya kuangua vifaranga.

Kulingana naye, walinunua vifaranga hawa kwa Sh100 kwa kila mmoja kando na mashine hii maalum ya kuangua vifaranga kwa Sh80,000. Kwa sasa vifaranga hao ni kuku wakubwa ambao huwa wanataga mayai. Mayai haya, anaeleza Wamaitha ndio huwa anauza na mengine anayatumia kuangua vifaranga kwa kuyaweka kwenye mashine hiyo.

Kwa kawaida, mashine hii huweka mayai kwa joto la stima kwa siku 21 hadi pale ambapo vifaranga wanaanguliwa na kukaa kwenye mashine ii hii kwa siku tatu huku vifaranga wakipata chakula zaidi kutoka kwa mabaki ya mayai ili kuwapa nguvu zaidi za kujisimamia.

Baada ya siku hizi tatu, vifaranga hawa hutolewa kwenye ile mashine na kuwekwa katika sehemu tofauti ambako kuna joto na mwangaza wa stima na kula chakula aina ya Chick Mash hadi pale wanapotimu umri wa wiki sita.

“Baada ya wiki hizi tatu, huwa nawahamisha na kuwaweka kwenye vyumba vya nje ambako wanakula aina ya chakula cha Growers Mash hadi wanapotimu miezi sita na kuanza kula chakula aina ya Layers,” anaeleza Bi Wamaitha.

Kuanzia mwezi wa sita, Bi Wamaitha anaongeza, kuku wa kike huanza kutaga mayai lakini jogoo huwa anawauza huku akibakisha wachache wakuwezesha kuku wengine kutaga mayai.

Kwa kawaida, huwa anauza jogoo kwa Sh1,000 wenye umri wa miezi tisa na zaidi. Anasema kuwa kazi yake ya kila siku ni kutunza kuku hawa kwa kuwapa chakula na maji hata kama si kazi ngumu kwake kwani huwa inamchukua saa chache kuwalisha kuku hawa na vifaranga, wote kwa jumla wakiwa zaidi ya mia tano.

Wamaitha anaeleza ya kuwa soko la kuku wake liko haswa eneo la Kitale mjini ambako huwa anauzia watu binafsi ama vikundi vya watu wanaohitaji kuku wengi wa kufanya sherehe mbalimbali.

Soko kuu

Aidha, soko kuu la mayai liko jijini Nairobi ambako huwa anauza kwa wingi katika eneo la Githurai na soko la Kamukunji ambako wanunuzi wa idadi kubwa ndio wateja wake. Akiwa mjini Kitale anachohitajika kufanya ni kutuma mayai haya kupitia kwa usafiri wa umma wa mabasi ambako wateja wake wanayapokea jijini Nairobi.

Kuhitajika kwa kuku zaidi kwenye soko huwa kunampa msukumo wa kila siku kufuga kuku zaidi.

Kulingana naye, kuku wanahitajika kwa wingi zaidi katika eneo la Kitale na Nairobi ambapo wafugaji hawajafikisha kiwango cha kutosheleza soko. Kutokana na hali hii, anasema kuwa anatazamia kufuga kuku wengi zaidi ya anavyofanya kwa sasa. Baadhi ya manufaa ambayo anayapata kutokana na ufugaji huu ni kwamba kuku wamempa yeye na mumewe ajira ya kila wakati ambayo inawapa riziki yao ya kila siku.

Aidha, kuku wamemwezesha kusomesha watoto wake hadi vyuo vikuu. Kando na hayo, huwa anapata mbolea ya kiasili kutoka kwa kuku hawa ambayo huwa anaitumia katika kilimo cha mboga za aina mbalimbali na matunda katika shamba lake.

Changamoto ambazo huwa anakumbana nazo kila mara ni kupigana na magonj- wa kwa kuwapa dawa kuku wake. Vile vile, mashine aliyonunua imemfeli kwa njia kubwa kwani alipoinunua alijua ya kuwa ina uwezo wa kuangua vifaranga asilimia 90 ilhali inafaulu kuangua asilimia 20 kati ya mayai mia sita anayoweka kwenye mashine.

Kwa sasa, mashine hii ambayo ina uwezo wa kuwekwa mayai 1,260, anaamini ya kuwa haijaafikia viwango vinavyohitajika.