AKILIMALI: Kwa mtaji wa Sh40,000 pekee wanahesabu maelfu zaidi kutokana na ufugaji mseto

AKILIMALI: Kwa mtaji wa Sh40,000 pekee wanahesabu maelfu zaidi kutokana na ufugaji mseto

Na MERCY MWENDE

CHANGAMOTO za ulipaji wa mikopo na migogoro ya wanachama imechangia pakubwa kufeli kwa vyama vingi vya kilimo na ufugaji mashinani.

Lakini kwa wenyeji 15 wa Othaya katika Kaunti ya Nyeri, kikundi chao cha kuweka akiba kimekuwa tegemeo kuu kwa miaka tisa sasa.

Wanachama hao wa kikundi cha Konyu Self Help Group waliungana kwa nia ya kufaidika na msaada wa kifedha kutoka kwa serikali, ambao ulikuwa ukitolewa wakati huo bila malipo.

Sababu ya umaskini wenyeji hao hawangeweza kumudu bei ghali ya kununua mashamba waingilie kilimo cha kahawa na majani chai kinachonawiri eneo hilo la Kati mwa Kenya.

Badala yake walitumia Sh40,000 walizopewa na serikali – kupitia mpango wa kutokomeza umaskini kwa wakaazi wa Othaya – kuanzisha kikundi chao.

Vile vile, walichanga Sh200 kila mwezi wakinuia kuzidisha kitita hicho ili kuwekeza katika kilimo biashara cha kiwango kidogo. Baada ya mwaka, walipokea mkopo wa Sh500,000 kutoka kwa Hazina ya Uwezo walizotumia kununua mbuzi 25 wa kufuga wakagawana.

Wakati huo kikundi kilikuwa kimeongezeka hadi wanachama 25.

Hivyo kila mwanachama alihitajika kuchukua mbuzi mmoja – ila ndume alimilikiwa na wanachama wote.

Kupitia Chama cha Wafugaji Mbuzi wa Maziwa Kenya (Dairy Goats Association of Kenya- DGAK) mjini Nyeri, walipata mafunzo jinsi ya kufanya mbuzi wao wanawiri kupitia malisho bora.

Chama hicho pia kilikubali kubadilisha ndume wao kila baada ya siku 15 kwa minajili ya kupata kizalishi bora.

Baada ya mbuzi hao kukomaa tayari kuuzwa, wanachama hao hutafuta soko na kuwauza kwa pamoja kisha pesa zote wanazokusanya hugawanywa baina yao.

“Mpango huu unahakikisha kwamba kila mwanachama anawalea mbuzi wake vizuri, kwani mwishowe tunapowauza kila mmoja hula jasho lake,” asema mwenyekiti wa kikundi, John Mwangi.

Ili kuongeza mapato ya kikundi chao cha Konyu Seelf Help Group, walichangamkia pia ufugaji wa nyuki.

Aidha, sababu nyingine ya wao kuchangamkia ufugaji wa nyuki ni ongozeko la maradhi ya kifua miongoni mwa wakazi wa Othaya, ambapo inaaminika kuwa asali ni tiba asili na bora kwa maradhi hayo.

Muda si muda, walifanikiwa kupewa mkopo mwingine wa Sh100,000 kutoka Hazina ya Uwezo, walizotumia kutengeneza mizinga na vifaa vingine vya kuanzisha ufugaji nyuki.

Wakaunda mizinga 25 aina ya Top-Bar waliyogawanya baina yao.

Pesa zilizosalia waliwanunua kuku 23 wa kufuga, ambao pia waligawana.

Baada ya kumaliza kulipa mkopo wao mwaka jana, walipokea Sh290,000 kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Ustawi wa Kilimo (IFAD) walizotumia kuzamia katika sekta nyingine ya ufugaji – samaki.

Kando na kuwafunza kuhusu ufugaji bora wa samaki, shirika hilo liliwapa vichengo 200 vya samaki aina ya Catfish walivyogawa baina yao.

Wanachama nao walihitajika kujengea samaki hao wachanga vidimbwi.

Baada ya kukomaa, samaki hao huuzwa Sh600 kwa kilo, ingawa ukinunua samaki mmoja pekee utalipia Sh300.

Nayo lita ya asali wanauza Sh800, gramu 250 ikiwa Sh350.

Kulingana na mwanachama Jacob Kamotho, mbuzi mmoja hutoa lita mbili za maziwa kwa siku – lita moja ikiuzwa Sh50. Aidha, mwanambuzi huuzwa Sh10,000.

 

Jacob Kamotho akimshughulikia mmoja wa mbuzi wake wa maziwa, nyumbani kwake kijini Konyu mjini Nyeri. Yeye ni mwanachama wa kikundu cha Konyu Self Help Group. Picha/ Jospeh Kanyi

Mbolea ya mbuzi hao ni Sh500 kwa kilo sokoni, ambapo Kamotho anasema humletea faida ya Sh20,000 kila mwezi.

Kuku nao huuzwa kwa Sh800.

Wateja wao kwa wingi huwa ni wakazi wa miji ya Othaya na Nyeri.

Pamoja na faida zote wanazopata, bado wanachama hao huhitajika kuchanga Sh300 kila mwezi kama akiba katika mfuko wa kikundi. Ingawa baadhi waliondoka kundini, waliosalia wana akiba ya Sh10,000.

Vile vile, wao hutembeleana mara kwa mara kuhakikisha kila mmoja anaendeleza ufugaji wake vyema.

Kila wanapokumbana na tatizo katika mradi mmoja, huwaalika wataalamu kuwapa mafunzo jinsi ya kujikwamua na kuendelea.

Changamoto kuu wanayopata ni bei ghali ya vyakula vya mifugo wao.

Kamotho anatoa mfano wa bei ya lishe ya mbuzi ambayo imepanda mno katika kipindi kifupi.

“Mwaka jana Desemba kilo 50 ya chakula aina ya Dairy Meal ilikuwa Sh1,800 lakini sasa imepanda hadi Sh2,500,” aeleza.

Nayo lishe ya samaki inagharimu mfugaji Sh4,500 kwa kila kilo 25.

You can share this post!

KAMAU: Ndoa: Waafrika wajifunze kutokana na Wazungu

Ghost Mulee akwama India baada ya Kenya kusimamisha safari...