Makala

AKILIMALI: Kwake matunda ni tiba na pesa

August 25th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KILA mtu anafahamu kuwa matunda ni muhimu sana kwa afya hasa wakati huu wa kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Matabibu wamekuwa wakisema kuwa tunda moja kwa siku hufukuza maradhi.

Pamoja na haya, kuna wale wanaofaidika sana kutokana na matunda, sio tu kama mlo lakini pia kama chanzo cha mapato.

Kwa Bi Keziah Wahome na mumewe Jesee Wahome, kutoka Ndungamano, Kaunti ya Nyeri matunda yamekuwa yakiwapa donge kwa miaka tisa sasa na hawana mipango ya kuacha zaraa hii.

“Tulianza kilimo cha matunda 2008, tukiwa na kundi lililoundwa na marehemu Profesa Wangaria Mathai la Green Belt Movement pamoja na vijana kutoka eneo hili. Wajibu wetu ulikuwa kupanda miti. Tulifunzwa jinsi ya kutayarisha miche katika mahema (greenhouses),” alisema Bi Wahome.

Anasema baada ya kifo cha Profesa Mathai waliamua kuendeleza ukulima wakitumia ujuzi waliopata. Wawili hao walianzisha kampuni ya Forest Edge Nurseries na wamekuwa kivutio kwa wakulima na maafisa wa kilimo kaunti ya Nyeri.

Katika mradi wao wanakuza avocado, nyanya, pepino tikiti na karakara (passion). Wawili hawa wamebobea katika kilimo hivi kwamba maafisa wa kilimo huwapeleka watu kwao kwa mafunzo.

Bi Wahome asema walisajili kampuni yao kupitia shirika la afya mimea nchini (KEPHIS) mwaka wa 2014.Kusajili kampuni yao, aeleza, kuliwafungulia milango na wakaanza kualikwa kutoa mafunzo katika maonyesho ya kilimo ya Nairobi na kaunti ya Nyeri.

“Sisi tunapenda sana kilimo. Kabla ya kuanza kulima matunda, tulikuwa tukifuga kuku wengi sana lakini kwa bahati mbaya, magonjwa kadhaa yaliwaathiri wakaaga dunia. Hapo ndipo tulipoamua kujaribu kilimo cha majani chai. Lakini yalikosa faida na tukaamua kuyakata na kuanza kilimo cha matunda,” aeleza.

Anasema matunda yana mapato mazuri na soko tayari kila wakati. Tulipata ushauri na mafunzo kutoka kwa maafisa wa kilimo na kuhudhuria semina na tangu hapo, tukatia bidii na tumefika hapa,” Jesee alielezea Akilimali.

Anasema huwa wanaandaa mafunzo kwa wakulima bila malipo.

“Huwa tunafanya hivi ili kuwezesha wakulima wengine kuwa bora kama sisi na kutumia vyema mashamba yao,” Jessee alitufafanulia.

Katika shamba lao la ekari mbili, huwa wanapata Sh50,000 kwa mwezi.

Huwa wanauza miche kwa Sh100 ikiwa itawalazimu kusafirisha miche hadi shamba la mnunuzi. Wana miche zaidi ya Sh20,000 katika mahema kwenye shamba lao.

Bi Wahome anasema huwa wanatumia mbolea kutoka kwa mifugo na hawatumii kamwe fatalaiza ya kisasa.

“Baada ya kuchimba mashimo, huwa tunachanganya udongo wa juu, ambao huwa na rutuba, na mbolea kutoka kwa mifugo kama ng’ombe kabla ya kupanda,” asema.

“Huwa ninaudhika sana kila ninaposikia vijana wakiteta kuwa serikali haijawasaidia kupata ajira, serikali haitakusaidia iwapo hautajisaidia; sio lazima mtu aajiriwe ofisini kwa sababu anaweza kubuni ajira. Kupitia kilimo hiki, ninaweza kuwalipia wanangu karo shuleni na pia kuwaajiri vijana kufanya kazi shambani mwangu.” Keziah alielezea.

Lakini hakuna kazi isiyokuwa na changamoto zake. Kuna magonjwa yanayoathiri mimea na dawa za kunyunyuzia huwa ni bei ghali.

Bi Keziah Wahome mkazi wa Ndungamano, Nyeri katika shamba lake ambapo anapanda aina tofauti za mitunda. Picha/ Benson Matheka

Pia, baridi inayopatikana eneo hili huweza kuathiri mimea na kufanya isikuwe ipasavyo. Kwa wanaotaka kujiunga na fani ya kilimo, “Sio rahisi. Lazima uweze kujikakamua na kutia bidii ili ufaulu. Ni vyema kutafuta ushauri wa waliofaulu katika kilimo ili ujifunze zaidi.” Bw Wahome alifafanua

Katika siku za usoni, wanaazimia kufikia wakulima zaidi sio tu kaunti ya Nyeri mbali kote nchini.

Aidha, Bw Wahome anasema lengo lao ni kufikia Wakenya wote na kuwahamasisha ili wabadilishe mawazo yao kuhusu kilimo.

“Tunalenga hasa vijana ambao wana uwezo wana nguvu za kubadilisha maisha yao na nchi kwa jumla. Tunataka kuwaonyesha jinsi ya kubuni nafasi za kazi kwa kutia bidii. Tunataka kuwadhihirishia kwamba kilimo ni nguzo ya uchumi wa nchi,” asema.