Makala

AKILIMALI: Licha ya ulemavu wake, yuko mstari wa mbele kufuga nyuki

April 18th, 2019 2 min read

NA PETER CHANGTOEK

LICHA ya ulemavu alionao, amekuwa akishughulikia ufugaji wa nyuki kwa muda wa zaidi ya miaka 20.

Bw Samwel Tangus, mkulima katika kitongoji cha Tendwet, eneo la Segemian, eneobunge la Narok Magharibi, katika kaunti ya Narok, amekuwa akishughulikia ufugaji wa nyuki tangu mwaka wa 1994.

Mkulima huyu ambaye anakabiliwa na changamoto ya ulemavu wa mguu mmoja uliosababishwa na Polio, alianzisha shughuli hiyo kwa kuitumia mizinga ya kienyeji, lakini kwa wakati huu, anaitumia mizinga ya kisasa.

Ni kuanzia mwaka 2005 ambapo alipata mwanzo mpya baada ya shirika moja la kushughulikia utunzaji wa wanyamapori kuanza kutoa hamasisho kwa wakulima katika eneo hilo kuhusu mbinu za kilimo, ambazo hazihusiani na ulimaji wa mashamba bali ufugaji.

Shirika hilo lijulikanalo kwa jina WWF, lilitoa mafunzo kwa wakulima kuhusu ufugaji wa kuku na nyuki, kati ya shughuli nyingine za kilimo zinazohusiana na ufugaji.

Bw Tangus, pamoja na wakulima wengine wakashauriwa kuunda muungano wa watu kumi na watano, kisha wakapewa mizinga ya kisasa ili waanzishe shughuli ya ufugaji.

“Tuliambiwa tuunde muungano na tumteue mwanachama mmoja ambaye angejitolea ili mizinga iwekwe kwake. Na kwa kuwa tayari nilikuwa na mizinga mitano ya kienyeji iliyokuwa imetengenezwa kwa magogo na nilikuwa na nyuki, wanachama wakaamua tuiweke mizinga kwangu. Tulipewa mizinga 10,” asema Tangus mwenye umri wa miaka 59.

Samwel Tangus akionyesha mizinga anayoitumia kuwafuga nyuki katika shamba lake lililopo katika eneo la Tendwet, Segemian, kaunti ya Narok, mnamo Jumamosi, Machi 16, 2019. Picha/ Peter Changtoek

Miezi michache baada ya kuianzisha shughuli hiyo, wenzake walianza kulegea na kupunguza juhudi zao.

“Tulikuwa tukiandaa mikutano kwangu kila mara, lakini baadaye wenzangu wakawa hawaji hata nikiwaalika tupange mikakati ya kuboresha ufugaji. Baadaye wakaamua kuniachia mizinga hiyo kwa mioyo safi,” aeleza mkulima huyo.

Mkulima huyu anadokeza kwamba amekuwa akifanya utafiti kwenye mitandao ili kupata habari zaidi kuhusu ufugaji wa nyuki.

“Niliendeleza mradi huo, huku nikifanya utafiti na kuvisoma vitabu vinavyoelezea kuhusu ufugaji wa nyuki. Kwa bahati njema, nina mtoto wangu wa kiume aliyeelimika na yeye alinisaidia kufanya utafiti kuhusu ufugaji wa nyuki nchini Kenya, na pia katika sehemu nyinginezo ulimwenguni,” aeleza mkulima huyu ambaye ni baba wa watoto watano.

“Jirani yangu mmoja aliyekuwa amestaafu jeshini, alikuwa ameanzisha ufugaji wa nyuki na akaniachia mizinga mingine kumi alipokuwa akihama kutoka huku na kuguria alikokuwa amenunua shamba. Aliporudi kuichukua mingine aliyokuwa ameibakisha, akaniongezea mingine mitano,” asema Tangus ambaye alikuwa na uchu wa ufugaji wa nyuki alipokuwa mdogo – zama hizo walipokuwa wakiishi katika eneo la Dondori, Nakuru.

Mizinga yake imewekwa katika sehemu mbili tofauti.

“Shamba langu lote ni robo tatu ya ekari, lakini nimetumia thumuni (?) ya ekari kwa ufugaji wa nyuki,” adokeza.

Kwa wakati huu, Tangus anaendelea kuitengeneza mizinga mingine ili aongeze idadi na kuchuma zaidi kutokana na ufugaji.

Kabla hajaanza kutekeleza shughuli ya kurina asali, yeye huvaa magwanda maalumu ili kujikinga dhidi ya kupigwa usena na nyuki. Aidha, yeye huyatumia maramba (sawdust) au samadi ya ng’ombe kuwashia moto.

Pia huwa na kifaa cha kupulizia moshi na kifaa cha kutia asali iliyorinwa.