Makala

AKILIMALI: Machungwa kwake dhahabu

April 25th, 2019 3 min read

Na PETER CHANGTOEK

BW Justus Kimeu alipokata kauli kujiuzulu katika ajira yake ya ukarani mnamo mwaka 2003, alikuwa na azma ya kujitosa kikamilifu katika biashara ya kuyauza makaa; biashara ambayo kwa wakati huo, ilikuwa ikivuma.

Hata hivyo, miaka sita baadaye, aliamua kuitia kikomo biashara hiyo, na kufunganya virago vyake halafu akaanza safari ya kuenda nyumbani mashambani ili kukiendeleza kilimo cha uzalishaji wa machungwa.

Kimeu ambaye ni mzawa wa kitongoji cha Kathiani, eneobunge la Wote, katika Kaunti ya Makueni, alikuwa na wazo la kuikuza mimea izaayo matunda ya machungwa ya kupandikiza (grafted oranges).

“Nilianza kuikuza michungwa mwaka wa 2007 nilipokuwa nikiiendesha biashara yangu ya makaa. Sikuwa na uhakika kama mmea huo ungenipa riziki,” anasema Kimeu.

Mkulima huyo alianza kwa kukusanya mbegu za malimau na kuzikausha na kuzipanda katika kitalu na baada ya majuma kadhaa, mbegu zizo hizo zikaota.

Bw Justus Kimeu akiwa katika shamba analolitumia kuikuza michungwa katika kitongoji cha Kathiani, Wote, Kaunti ya Makueni. Picha/ Peter Changtoek

Wiki tatu baada ya mbegu hizo kuota, mkulima huyo akaipandikiza miche na kuipanda kwenye vyungu. Baadaye, akaihawilisha miche hiyo na kuipanda shambani.

Kisha baada ya muda wa miezi mitano, akaipandikiza miche hiyo kwa kuitumia mimea ya machungwa na machenza (tangerines) na mimea mingine.

Baada ya miezi 14, Kimeu akaanza kuyachuma matunda yake ya kwanza. Hata hivyo, aliyachuma matunda kilo tatu tu kutoka kwa kila mmea.

“Nilianza kwa mimea 150 niliyoipanda kwenye shamba nusu ekari. Kwa hivyo, nilichuma kilo 450, ambayo niliuza huku,” anafichua mkulima huyo.

Hakufa moyo, bali alikiendeleza kilimo hicho ima fa ima. Msimu mmoja baada ya mwingine, matunda yake yakawa yanazidi kuongezeka.

Mnamo mwaka 2009 aliifunga biashara ya kuuza makaa na kutilia maanani shughuli ya uzalishaji wa machungwa ambapo alilipanua shamba la ukuzaji wa mimea hiyo kuwa ekari tatu.

Kwa wakati huo, mimea yake ilikuwa ikiyazalisha matunda tani mbili hadi tatu kwa msimu, kinyume cha matarajio yake ya kuchuma kilo 70 kutoka kwa mmea mmoja.

“Nilijaribu kuweka mbolea zaidi kwenye mimea yangu ili kupata mazao lakini sikufaulu. Mazao yangu yaliendelea kuwa hivyo bila kuongezeka,” anasema mkulima huyo ambaye shamba lake linajulikana kwa jina Lotta Agrifarm.

Milango ya ufanisi ilifunguka mnamo mwaka 2012, wakati shirika moja la Kenya lisilokuwa la kiserikali lijulikanalo kwa jina Pafid (Participatory Approaches for Integrated Development), lilipompa mafunzo kuhusu kilimo hicho.

Shirika hilo huwafunza wakulima kuhusu mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga na madhumuni yalo ni kukiboresha kilimo na maisha ya wakulima kwa kuwapa mafunzo ili kuimarisha uzalishaji wa chakula.

“Niliambiwa kuwa Pafid ilikuwa ikiwapa mafunzo wakulima wanaotumia mashamba madogomadogo na wakulima wa pamba, katika maeneo yenye ukame katika mashariki ya Kenya,” akasema Kimeu.

Mafunzo

Mbeleni, alikuwa hana nia ya kutaka kupewa mafunzo mahususi, lakini kwa kuwa alikuwa akitaka kuyapata mazao mengi ya matunda katika shamba lake, akalegeza msimamo wake na akakubali kupewa mafunzo hayo.

Hakujuta kupokea mafunzo hayo kwa sababu baada ya muda wa miezi 18, alikuwa ameongeza kiasi cha shamba kuwa ekari tano, na kwa wakati huu ana shamba ekari saba analolitumia kuikuza michungwa.

“Mazao yangu yaliongezeka kabisa na kwa wakati huu ninachuma matunda tani 20 kutoka kwa mimea yangu 2,000,” anafichua.

Ametengeneza sehemu ya kuyateka na kuyahifadhi maji ya mvua ardhini ili yatumike wakati panapokuwa na kiangazi, na yeye huzitumia mbolea asilia.

Mbali na kuongezeka kwa mazao, mbinu ya kilimo anayoitumia ijulikanayo kama Climate Smart Agriculture, pia huongeza muda wa mazao kuwapo kwa muda mrefu pasi kuharibika. Matunda hukaa kwa muda wa miezi mitano badala ya mwezi mmoja.

Ili kuhakikisha wadudu waharibifu wanaangamizwa bila kutumia viua-dudu (pestcides), Kimeu huutumia ulimbo fulani kuwanasa wadudu hao.

Aidha, mbinu hiyo ya kilimo humwezesha mkulima kuikuza mimea mingine kwa nafasi inayoachwa kati ya mimea. Mimea ya kuugubika mchanga, mathalan njegere (peas), maharagwe, mitikiti (watermelons), na kadhalika huweza kukuzwa pamoja na michungwa.

Isitoshe, mimea kama vile miharagwe na njegere hugubika mchanga ili usikauke na kupoteza unyevu au maji kwa urahisi. Hali kadhalika, mimea iyo hiyo hutia madini ya natrojeni kwenye mchanga, na hivyo kuongeza rotuba na hatimaye hongeza mazao.