Makala

AKILIMALI: Majitaka yalivyo hatari kwa kilimo mijini

July 16th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MAAFA makubwa ya kiafya yanawakodolea macho Wakenya huku wakulima fulani wakitumia majitaka kukuza mboga zinazouzwa jijini.

Kilimo hiki hatari kimeshamiri viungani mwa miji hususan ya Nairobi na Machakos, huku wakazi wasio na ufahamu wowote wakila vyakula vilivyozalishwa kwa maji hayo machafu yenye sumu hatari.

Imebainika kwamba wakulima hutumia maji kutoka mabomba yaliyopasuka ya kupitisha majitaka ya baraza la jiji la Nairobi, kupanda na kunyunyuzia mashamba.

Wauzaji wa mboga wamekuwa wakimiminika kwa wingi katika mashamba yaliyo eneo la Njiru na Ruai kununua mboga na mazao mengine, bila kujali vyakula hivyo vinaweza kuwasababishia wateja matatizo ya kiafya.

Hii ni licha ya mashirika ya kulinda mazingira na ya kijamii kuelezea wasiwasi wao kuhusu mboga zinazokuzwa katika maeneo hayo.

Wakulima hao, hata hivyo, wamejitetea kwamba kwa miaka mingi wamekuwa wakiendeleza shughuli za kilimo katika eneo hilo.

Hii wamefanya chini ya kikundi chao kilichosajiliwa rasmi kwa jina Kirima Farmers Association, ambacho kilibuniwa na aliyekuwa mbunge wa Starehe marehemu Gerishon Kirima .

Mashamba yao yamepambwa kwa kijani kibichi huku mahindi, migomba na aina tofauti za mboga zikinawiri hata wakati wa kiangazi.

Mto Ngong ulio karibu na hapo umechafuka kabisa huku Mamlaka ya Kusimamia Mazingira (NEMA) ikipambana kuusafisha.

Wanachama wa kikundi hiki wanakiri kwamba wakazi wapatao 800 wamekuwa wakitumia majitaka kukuza mboga.

Bw Robert Kamau, aliyedai kwamba hawezi kuacha kulima katika eneo hili kwa sababu hana ajira nyingine alisema baadhi yao wamekuwa wakihepa maafisa wa serikali na kufanya kazi shambani usiku.

Shirika la kulinda mazingira linasema maji taka wanayotumia wakulima hao kukuza mazao yao yana sumu hatari inayoweza kusababisha madhara katika mwili wa binadamu.

Shirika hilo linasema baadhi ya maji hayo yanatoka katika viwanda vinavyotumia kemikali kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Kulingana na wataalamu wa NEMA, majitaka huwa na kiwango kikubwa cha madini ambayo bila shaka yana uwezo wa kuleta athari za kiafya katika mwili sio tu wa mwanadamu bali pia wanyama.

Utafiti uliofanywa na NEMA ulidhibitisha kiwango cha madini hatari yaliyopatikana kwenye mboga zilizokuzwa kwa majitaka ni pamoja na chromium, cadmium, copper, lead, nickel, zinc, cobalt magnesium, chuma na asenic.

Katika majaribio, sampuli za maji kutoka maeneo kadha ya upanzi wa mboga yalikusanywa, huku mboga, matunda na mchanga tofauti pia zikuhusishwa kwenye utafiti huu. Wataalamu wanasema kulingana na tafiti, kutumia mboga zilizo na madini haya hatari kwa muda mrefu, unaweza kusababisha maradhi ya figo na katika sehemu zingine za mwili.

Lakini kwa kutofahamu, wakulima wanaendelea kupanda mboga hizi bila kuelewa hatari inayonuikia.

Wanamazingira wanasema tafiti zimeonyesha kuwepo kwa kiwango kikubwa zaidi cha asidi katika mchanga ulionyunyuziwa maji taka, ikilinganishwa na ule ulionyunyiziwa maji safi au mvua.

“Matokeo ya tafiti yameonyesha kuwa, mbali na kuwepo kwa kiwango cha juu cha madini hatari kupita kiwango kinachohitajika mwilini, na iwapo mboga hizi zitatumika kama chakula, huenda zikawa na athari nyingi mwilini katika siku zijazo,” inaeleza ripoti ya NEMA.

Shirika la watumiaji bidhaa nchini COFEK linasema NEMA linafaa kuchukua hatua kukomesha kilimo kwa kutumia maji taka.

Cofek linasema kwamba majitaka yana madini hatari ya risasi ambayo ni hatari kwa mazingira na maisha na mwili wa mwanadamu.

NEMA inasema ilichukua hatua baada ya kugundua kuwa kanuni za kudhibiti mazingira zilikuwa zikikiukwa.