Makala

AKILIMALI: Mapera yake ya Kizungu huwindwa na ndege, naye amepata suluhu

October 3rd, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

MATUNDA aina ya peasi yanaweza kukua vyema katika sehemu za nyanda za juu, hususan Bonde la Ufa na eneo la kati miongoni mwa kaunti nyinginezo nchini.

Faida zake ni nyingi ikiaminika kuwa zinaweza kusafisha mishipa ya moyo, hutibu mafua pamoja na kurahisisha mmeng’enyo wa chakula pindi kinapoingia tumboni.

Hili ni tunda ambalo wakulima wengi hawajakuwa wakilipatia kipaumbele, kama vile ndizi, mipapai, machungwa matikiti maji na ndimu.

Kaunti ya Nyandarua ni miongoni mwa maeneo yanayokuza matunda haya kwa wingi, huku wakulima wengi wakiyakuza matunda haya ndani ya kitalu au mashamba ya kibinafsi.

Hata hivyo mbali na ladha yake nzuri ndege na wadudu wamekuwa kero kubwa, jambo linalowafanya wakuzaji kukadiria hasara kubwa kwa kufikisha mazao duni sokoni.

Hata hivyo Akilimali ilitemblea baadhi ya mashamba kujifundisha mengi, jinsi wakulima wamekuwa wakijifaidi kutokana na zao la peasi na mmoja wao ni Philip King’ori, ambaye anakuza peasi ndani ya aina maalum ya nyumba.

Ukitazama kwa mbali utafikiria ni nyumba ya kawaida au ghala la kuhifadhia nafaka.

Nyumba yenyewe ni sawa na kitalu, isipokuwa imezingirwa kwa waya na kutundikiwa neti juu yake, ili miale ya jua na hewa safi ziweze kupenya kwa urahisi ili kuzifanya peasi ziweze kuiva.

Anasema kuwa aliamua kuzungusha waya na kutumia neti sawia, kwa sababu ndege ndio wamekuwa wakiharibu matunda ya wakulima wengi kabla ya kuvuna.

Anasema kipande hiki kidogo cha ardhi(robo ekari), kinatumika kama karakana ya kufanyia utafiti, kwa sababu vyuo vingi kutoka nchini Kenya na Ulaya vimekuwa vikifanyia utafiti wao hapa.

Kwa wakati mmoja ndani ya nyumba hii maalum ya kukuza peasi, watu 50 wanaweza kuingia pasipokuwa na msongamano ili waweze kufurahia ukulima anaoendelea.

Anasema kuwa huwa hatozi malipo ya aina yoyote, kwa sababu nia yake kuu ni kuwasaidia wakulima wadogo waweze kutekeleza kilimo cha peasi kwa kuzingatia kanuni zote zinazostahili.

Akiwa meneja wa eneo hiI linalofahamika kama Tumor Hill anasema aina ya peasi wanazokuza ni pandikizi (cross breed) ya matufaha na peasi zile za kawaida.

Philip anasema nyumba hii ni takriban mita 20 kwa 30 hivi mstatili, akiamini kuwa kitaaluma matunda haya huhitaji nafasi ya kutosha ili matawi yake yaweze kuwanda bila kushindania virutubisho muhimu vinavyoweza kupatikana mchangani.

“Kwa msimu mmoja ambao ni miezi mitatu mkulima anaweza kuvuna kilo 20 ya peasi, ambapo kila tunda moja huuzwa Sh20 na wakati mwingine Sh25,” Philip akasema.

Katika kaunti ya Nyandarua msimu mzuri wa kupanda matunda haya ni baina ya Agosti na Septemba, ambapo huanza kutoa maua baada ya mwezi mmoja unusu ishara tosha yanaelekea kukomaa.

Hatimaye ganda la nje huanza kukolea rangi ya kijani kibichi na ifikapo Machi na Aprili matunda ya mkulima huwa tayari kwa ajili ya kuvunwa.

“Msimu wa kukua sio rahisi peasi kukabiliwa na viwavi jeshi wala wadudu aina ya aphids kwa sababu hii ni mimea inayochipuka bila kupandwa katika mashamba mengi, ”aliongezea.

Lakini endapo mkulima anataka kuipanda mimea hii anaweza kuyakata mashina, na kuyatundika ardhini kina cha sentimita 15 na kunyunyizia maji hadi shina litakapochipuka.

Alisema kuwa peasi zinafaa kupandwa kwa urefu wa mita 6 kutoka kwenye mmea mmoja hadi mwingine.Wakati mwingine mkulima anaweza akalazimika kuongeza urefu kulingana na ukuaji wa matunda yake.

Pindi mimea inapokomaa mti mmoja unaweza kubeba baina ya peasi 30-40, akiamini kuwa tija ya kilimo hiki ni kubwa ikilinganishwa na kilimo cha aina nyingine.

Alieleza kuwa mkulima anastahili kutumia kilogramu 200 ya samadi kila msimu, na wakati mwingine anaweza kutumia mbolea za DAP na kuchanganya na ile ya NPK.

Mbolea za viwanda zinastahili kunyunyizwa wakati ambao mimea imeanza kutoa maua, kwa mara ya kwanza ili kuongezea madini ya phosphorus na Magnesium ambayo ni haba mchangani.

Pili Philip alieleza kuwa ili mimea ya peasi iweze kufanya vyema mkulima ahakikishe kuwa anayakata magugu kila wakati.

Magugu yanayokabili matunda ya mwituni ni sugu hivyo basi, mkulima ahakikishe anayaangazia matunda yake tangu yakiwa changa hadi yatakapokomaa.

“Kabla mimea haijakomaa ni wazo zuri kwa mkulima kutumia mbolea ya asilia ili isije ikakausha mimea yake,” akaongezea.

Kuwalisha wafanyakazi

Katika shamba lake dogo anamiliki mimea 35 inayobeba matunda ya peasi, ingawa matunda haya hayauzwi sokoni ila yanatumika kuwalisha wafanyakazi katika eneo la Tumor Hill.

Hili ni eneo linalopokea idadi kubwa ya wageni wa kigeni wa humu nchini kufanya mikutano na kufurahia mazingira ya Nyahururu na Nyandarua kwa jumla.

Anawashauri wakulima wadogo kugeukia kilimo hiki ili waweze kujiongezea tija katika ukulima wao, kwani hivi karibuni kiwanda cha kutengeneza juisi ya peasi kimefunguliwa nchini hii ikiwa ni fursa nzuri wanayoweza kutumia wakulima kujiongezea kipato.

Anasema kuwa soko la matunda humu nchini linazidi kupanuka kila kukicha kutokana na idadi kubwa ya watu kushauriwa kula matunda ,hususan wagonjwa ili kukabiliana na ongezeko la maradhi kama vile pumu, ukosefu wa hamu ya kula na shinikizo la damu mwilini.

“Tunda la peasi lina vitamini A na B kinyume na matunda mengine yenye vitamini C pekee,”alisema Philip