Makala

AKILIMALI: Mapungufu ya mwilini hayajamzuia kuibuka stadi wa kufuga kuku

April 4th, 2019 3 min read

Na CORNELIUS MUTISYA na CHARLES WASONGA

INGAWA ni mlemavu, Michael Wambua Nduya amedhihirisha bayana kuwa kujipata katika hali hiyo katu sio sababu ya kuanza kuombaomba mitaani umebeba bakuli mkononi.

Hii ndiyo maana aliamua kujituma kwa kuanza kazi ya ufugaji wa kuku wa kienyeji, kazi ambayo imemfanya kuwa kielelezo chema katika jamii.

“Najichumia maelfu ya pesa kila mwaka kupitia ufugaji wa kuku na wala sijihisi kama mlemavu,” asema mkulima huyu mzaliwa wa kijiji cha Nzaikoni, kata ya Iveti, Kaunti ya Machakos.

Kwenye mahojiano na waandishi hawa majuzi nyumbani kwake Bw Nduya, maarufu kwa jina ‘Musavi’, alifichua kuwa alizaliwa akiwa buheri wa afya.

Hata hivyo, afya yake ilianza kudhoofika mnamo 1956 akiwa na umri wa miaka miwili pekee alipokumbwa na maradhi ya polio yaliyopooza miguu yake yote.

“Wakati huo huduma za afya zilikuwa adimu sana eneo letu maana ilikuwa enzi wa ukoloni. Kwa sababu hii, sikupokea chanjo yoyote dhidi ya polio kama ilivyo siku hizi hivyo nikaishia ulemavu,” anasema.

Licha ya kupooza miguu, wazazi wake walimpeleka katika shule ya msingi ya Nzaikoni ambako alikuwa akiishi nyumbani kwa mjomba wake, Matheka Nduya.

Alipohitimisha masomo ya msingi, Wambua alijiunga na shule ya upili ya Kikombi kabla ya kuhamishwa hadi shule ya upili ya Mbooni kulikokuwa na kitengo cha wanafunzi walemavu kama yeye.

“Nilifuzu vyema na nikajiunga na chuo kimoja mjini Machakos kusomea kozi ya uhasibu,” anaeleza Bw Nduya.

Hata hivyo, maisha yake nusura yatumbukie nyongo mwaka wa 1979 mamake alipoaga dunia na akalazimika kukatiza taaluma hiyo.

Aliamua kurejea nyumbani kwao ili ajaribu bahati yake katika fani nyingine za kimaisha.

Kutokana na ushauri aliopata kutoka kwa wachungaji wa kanisa katoliki la Nzaikoni Bw Nduya alishawishika na kukubali kuanza kazi ya ufugaji kuku wa kienyeji.

“Waumini walininunulia vifaranga 10 ilini niweze kuanza safari katika fani hii ya uvuvi. Vile vile nilipewa kipande kidogo ardhi kiasi nusu ekari kando ya kanisa hilo ambako nilijenga kibanda cha kuku,” anaeleza.

Anaongeza: “Nilijizatiti kuwatunza kuku hao nikisaidiwa na marafiki zangu; Mwanzia Mutunga na mwanangu Mutuku Ndolo huku nikachanganya na upanzi wa mboga aina za kabeji, sukuma wiki, pamoja na nyanya.”

Anasema kuanzia mwaka 2004 baraka za Maulana zilianza kumwonekania pale kuku hao walipoanza kuongezeka kupitia uanguaji wa kiwango cha kuridhisha kabisa.

“Nilianza kuingiza mapato mazuri kupitia uuzaji wa mayai na kuku waliokomaa. Wateja walikuwa, na wangali, wenye mikahawa mikubwa mjini Machakos na maeneo ya karibu,” mfugaji huyu anasema.

Laki moja

Kulingana na Bw Nduya kazi hiyo ya kuku ilikuwa ikimwingizia takriban Sh100,000 kwa mwaka mmoja kabla ya kutoa gharama. Hii ni kando na mapato kutoka kwa mauzo ya mboga na nyanya.

Mnamo 2007, maisha ya mkulima huyu yalipata pigo kubwa pale mkewe, Ruth Muthio, aliaga dunia katika hali tatanishi na akabaki na mzigo mkubwa wa kulea watoto wao sita. Kimako kweli!

“Nilifadhaika mno mke wangu alipoaga dunia ghafla kwani alikuwa nguzo kuu katika familia yangu,” Bw Nduya anasema kwa machungu.

Naam! Kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa upishi!

Licha ya mkulima huyu kufiwa na mkewe mpendwa, alijizoazoa na kuamua kuaendelea na kazi yake ya ufugaji wa kuku na kilimo cha mboga huku akishirikiana sako kwa bako na wanawe.

“Tuliendelea kujikimu kwa kuuza kuku na mayai licha ya kuondokewa na mmoja wetu-mama watoto kazi ambazo tunaendelea kufanya mpaka wakati huu,” anasema.

Bw Nduya adokeza kwamba licha ya changamoto za hapa na pale, yeye huuza kuku na mayai na kujiwekea akiba.

Kwa kufanya hivyo, ameweza kuanzisha biashara ya mkahawa katika soko Kathiani ambako amewaajiri watu wanne huku mwanawe kwa jina David Wambua akiwa msimamizi wa biashara hiyo.

“Ninaoena fahari kazi ya mikono yangu. Licha ya ulemavu wangu huu, sijawahi kuombaomba mitaani. Najikimu kimaisha hata kuliko badhi ya watu ambao viungo vya miili yao ni shwari,’’ asema.

Mkulima huyu anaomba serikali, mashirika mbalimbali ama watu binafsi wajitokeze kumfaa kwa hali na mali ili azidi kupanua kazi zake.