Makala

AKILIMALI: Mashine za kisasa kurahisisha kilimo

August 12th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Mfumo wa kutekeleza kilimo kidijitali umekuwa ukipigiwa debe kutokana na uvumbuzi wa kisasa unaoelekea kurahisisha ukulima, mbali na kupunguza gharama ya uzalishaji.

Ili mkulima afikie kiwango cha kimataifa, hana budi kuelewa kwa kina, sayansi ya maliasili hasa udongo pamoja na ufaafu wake katika ustawishaji wa mimea.

Maji madini na virutubishi kwa kiwango sahihi, ikiwa ni sehemu nyingine ya kuzingatiwa mbegu zinapopandwaardhini na hatimaye kuchipuka.

Kwa upande mmoja wakulima wanashauriwa kuhusisha teknolojia ya kilimo biashara ilmuradi wajiongezee kipato, kutokana na malighafi haba yanayoweza kupatikana katika mazingira yao.

Hii ni baadhi ya mimea iliyokuzwa kiteknolojia. Picha/ Richard Maosi

Aidha, wanahimizwa kuja na mikakati itakayosaidia kukabiliana na uhaba wa mvua ,kwa kupanda mimea inayokomaa upesi kama viazi tamu mawele na mtama.

Changamoto za ukame zinaweza kupigwa teke na kuzilinda raslimali zetu za asili endapo wakulima watalenga kulinda afya ya udongo kupitia mifumo ya agronomia.

Agronomia ni taaluma ya sayansi na udongo, lakini wakati mwingi hujaribu kuonyesha uhusiano uliopo baina ya mimea na mazingira.

Haya ndiyo mawaidha tosha kutoka kwa mtaalam Wambui Ngugi mvumbuzi wa teknolojia na mratibu wa masine za kisasa, zinazoweka kutumika shambani kuanzia kiwango cha kupanda hadi kuvuna.

Wambui Ngugi akionyesha mtambo unaotumika kukata mapande makubwa ya udongo hadi yawe vipande vidogo ili kuruhusu maji na hewa safi kupenya kwa urahisi. Picha/ Richard Maosi

Ngugi anawashauri wakulima kuenda na wakati ili waweze kukabiliana na ushindani mkali unaopatikana kwenye masoko ya kimataifa, yanayojihusisha na ukulima wa mboga na matunda.

“Ubora wa bidhaa hizi unategemea mbinu sahihi za kutekeleza upanzi,kupulizia mimea dawa,kudhibiti magugu na kuvuna kidijitali,”Ngugi alisema.

Anaona kuwa teknolojia ya kisasa inaweza kuwa ya manufaa badala ya kuongeza matatizo kwa wakulima,akisema kuwa hili litawezekana endapo wakulima mashinani watashirikiana na watafiti.

Akizungumza na Akilimali alitufichulia kwamba kiungo muhimu katika shughuli zote shambani ni kuhakikisha mchanga upo katika hali nzuri, ili kufanikisha ukuaji wa aina mbalimbali ya mimea isije kunyauka.

Hawa ni wauzaji wa mitambo ya kisasa waliohudhuria kongamano la wakulima katika shule ya kiufundi ya Rift Valley kuhamasisha wakulima. Picha/ Richard Maosi

“Ili kuwa na ukulima wa kuleta tija,mkulima anapaswa kufuata utaratibu wote wa kufanya mchanga wake uweze kuzalisha mimea yenye afya tele,”alisema.

Teknolojia ya kisasa imekuja na jawabu kwa wakulima wanaotumia nguvu nyingi kupita kiasi,katika harakati ya kuufanya udongo uwe laini.

Maine hizi zinaweza kuvunja matofali ya mchanga hadi uwe vigaevigae au vumbi zinazoweza kuchukua maji na rutuba kwa urahisi.

Ni kwa sababu hiyo shirika analohudumia Bi Ngugi, limekuja na mtambo ya kisasa unaoweza kuvunja na kulainisha udongo ili kuongeza ufaafu wa mchanga kwa shughuli za kilimo.

Wambui Ngugi kutoka mjini Nakuru akionyesha mtambo unaoweza kuvuna viazi bila kufanya uharibifu wowote. Picha/ Richard Maosi

Udongo unafaa kulainishwa ili kuruhusu mizizi ya mimea kupenya kwa urahisi na hatimaye kufikia virutubishi muhimu kama vile phosphorus na maji yaliyokolea mchangani.

Aidha mizizi ya mimea inaweza kupata mzunguko sahihi wa hewa safi ya oksijeni na nitrojeni wakati wote wa masaa 24 kwa siku saba.

“Isitoshe viumbe wadogo wanaokaa ndani ya mchanga hupata wakati mwafaka wa kufanya kazi yao vyema ikiwa udongo sio tifutifu,”aliongezea.

Ngugi alisema udongo uliolainishwa hufanya mbolea kuchanganyika vyema na mchanga na kutengeneza mazingira mazuri kwa ustawishaji wa mimea ya thamani.

Pia hutoa fursa nzuri kwa mkulima kutandaza mabaki shambani , kwa kutumia masalio ya mimea na magugu yaliyokatwa ambayo hatimaye hutundikwa juu ya mchanga.

Kisayansi masalio haya yanapaswa kuchukua wiki mbili kabla ya kuoza,kisha yakachangia asilimia kidogo ya rutuba ya asilia kwenye mchanga.

Matrakta ya kisasa ya kilimo. Picha/ Richard Maosi

Alieleza hatua hizi zote husaidia mchanga kunyonya unyevu wowote unaopatikana juu ya ardhi, kwa urahisi na kupunguza visa vya mmomonyoko wa udongo.

Mtambo huu wa kulainisha udongo pia unaweza kusaidia katika utengenezaji wa matuta ambayo hupunguza kasi ya maji na hivyo basi kuzima kasi ya maji inayoweza kusomba bidhaa hii muhimu.

Bi Ngugi anawatahadharisha wakulima dhidi ya kutumia moto wakati wa kuyaandaa mashamba yao wakati wa kupanda, kwani moto huangamiza viumbe mbali na kupunguza kiwango cha rutuba katika mchanga.

Kwa mkulima anayepania kutekeleza kilimo ipasavyo anakumbushwa kutumia planter , huu ni mtambo unaotengeneza nafasi za kuweka mbegu na kupanda bila kutegemea uangalizi wa mkulima.

Pili anaweza kutumia sprayer hii ikiwa ni masine ya punde zaidi kufanyiwa majaribio, inayoweza kunyunyizia mimea dawa na wakati mwingine kupima kiwango cha dawa kinazohitajika, kupitia akronomita ya kipekee inayosajili kiwango kinachostahili.

Mimea hii inahitaji mashine za kisasa kuikuza. Picha/ Richard Maosi

Tatu ni mtambo wa harvestor unaoweza kuvuna mimea pindi inapokomaa bila kusababisha hasara wala uharibifu wa aina yoyote wakati ikipenya baina ya mimea iliyostawi shambani.

Bi Ngugi alifichulia Akilimali kuwa kilimo kidijitali ni mfumo ambao unaelekea kuwafaa wakulima wadogo mashinani wasiokuwa na kipato cha juu.

Aidha anawahimiza wakulima wadogo kuhudhuria makongamano ya kitaifa na maonyesho ya kilimo, ili wajipige msasa na kuchangia katika pato la taifa ikizingatiwa kilimo ni uti wa mgongo.

Wakulima wanaolengwa zaidi wakiwa ni wale wanaotokea katika maeneo kame, ambapo mchanga haina rutuba ya kutosha na hufanya nyufa baada ya kukauka.

“Wale wanaokuza maharagwe,mtama,ngano na simsim katika mashamba madogo ambao mara nyingi hutegemea huduma za vibarua kulima na kupalilia na hata kuvuna,”alisema.

Ngugi anasema kilimo pia ni kazi kama ile ya ofisi,ni kwa sababu hiyo anawashauri vijana waliopata elimu kuwa katika mstari wa mbele kufanya kilimo,wala wasisubiri nafasi za ajira kupatikana ambazo ni haba siku hizi.