Makala

AKILIMALI: Matunda ya stroberi yatia ladha maisha yake ya uzeeni

August 13th, 2020 3 min read

Na RICHARD MAOSI

KWA kutumia muda wa nusu saa hivi kutoka mjini Kiambu, Akilimali inazuru eneobunge la Gatundu na kukutana na Daniel Gitau ambaye ni mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Reli la Kenya.

Gitau ni mkulima wa Stroberi aina ya Chandler katika shamba la Kimunyi.

Anasema alianzisha mradi huu mnamo 2013 ili kujiongezea kipato mbali na kukuza mboga za kiasili, vitunguu na sukumawiki.

Kwanza alifanya utafiti mtandaoni kuhusu zao la stroberi na kutafuta soko, akisema si wakulima wengi nchini ambao wamechangamkia stroberi kwani wengi husadiki kuwa ni zao la kigeni.

Katika kilimo-biashara, maandalizi ya kupanda stroberi yanatakikana kuanza mapema, mipango kabambe ikitiliwa maanani. Aidha, mkulima hutakiwa kuandaa shamba na kuweka mbolea ya kutosha, ambapo stroberi huchukua kati ya miezi 3-4 kukomaa.

Vilevile, Gitau anasema mkulima anatakiwa kupanda mimea yake msimu wa jua, ili kufanya matunda yaive haraka na kupata rangi nyekundu iliyokolea, tayari kumpatia tija nzuri pindi yanapouzwa sokoni.

Hii huhitaji bidii za mkulima, anayetakiwa kujizatiti zaidi. Pia anatakiwa ajihami na mitambo, apate ushauri wa mtaalam wa mimea (agronomist), elimu kuhusu mabadiliko ya hali ya anga na mtaji wa kutosha.

“Mbali na kuwaajiri vibarua wanaosaidia kufanya kazi ya shambani, mke wangu amekuwa akisaidia kutunza mazao wakati nikitafuta soko la nje mjini Kiambu, Nairobi, Naivasha na Nakuru,” asema.

Kufikia sasa Gitau anamiliki mimea 32,400 ambapo kila mmea hubeba takriban matunda 40 msimu ukiwa mzuri.

Kwa wiki, Gitau huvuna mara tatu na kupakia matunda ya stroberi kiasi cha gramu 250, ambapo gramu 250 huuzwa kwa Sh150, huku kilo moja ikiuzwa Sh600.

Wakati mwingine mazao ya stroberi huwa yamefurika sokoni, jambo linalofanya bei yake kuteremka pakubwa, hivyo basi humlazimu Gitau kutembeza mazao yake katika makazi rasmi ya watu, na kuchuuza kwa bei ya chini.

Pili, kwa sababu zao hili huharibika haraka, soko la uhakika ni jambo la kimsingi kwa mkulima anayetegemea stroberi, kwani mkulima anapaswa kujizatiti ili kuhakikisha anapata soko kwa mazao yake haraka yasije yakaharibika kabla ya kununuliwa.

“Maduka ya kijumla na wanunuzi wa kibinafsi ndio huchukua nafasi kubwa ya kuagiza. Mara nyingi wamekuwa wakiagiza bidhaa hii kabla ya kuvunwa, na wakati mwingine wakinisukuma kutafuta stroberi kutoka kwa wakulima wengine,” aliongezea.

Kulingana na Gitau, mmea mmoja wa stroberi unaweza kutoa kilo moja ya matunda haya kila wiki endapo mkulima atatunza mimea yake vyema kwa kunyunyizia maji ya kutosha na kuikinga dhidi ya maradhi.

Mara tu baada ya kupanda mimea, maji ya kutosha, mbolea, dawa ya kurashia, jua la kutosha na kupalilia kila mara ni mambo muhimu ya kuzingatia, katika hatua za awali.

Anaeleza kuwa mboji kutoka na kinyesi cha mbuzi na kondoo ndio wenye manufaa zaidi kwa mimea kutokana na virutubishi vingi na madini ya hali ya juu.

Isitoshe wakulima wengi kutoka Kiambu ni wafugaji wa kondoo na mbuzi, hivyo basi upatikanaji wa mbolea ya aina hii ni rahisi.

Kwa mwaka mmoja, Gitau hutumia zaidi ya kilo 50 za mbolea, akiongezea kuwa miezi 5-6 inatosha mbolea kuoza na kuchanganyika vizuri na mchanga.

Hata hivyo, zao la stroberi humea karibu na mchanga, mizizi yake si ya kina kirefu na ndiyo maana stroberi zinaweza kuvamiwa na vidudu vinavyopatikana juu ya udongo au baridi kali ya kipupwe.

Pia anawashauri wakulima wasitumie kiwango kikubwa cha dawa za kupulizia hususan msimu wa mvua. Anasema maji yaliyokolea dawa kupita kiasi yanaweza kusombwa mtoni na kusababisha uchafuzi wa mazingira.

Isitoshe, ili kuzuia mimea isije ikaathirika na wadudu waitwao white flies, kupindua matawi kila asubuhi na kuchunguza endapo mabaka meusi yameanza kutokea ni miongoni mwa mambo ambayo ameweka katika ratiba.

Hii ikiwa ni ishara tosha kuwa huenda mimea haipati maji ya kutosha ama baadhi ya wadudu wameanza kutafuna mashina na mizizi.

Mara nyingi mabaka meusi husababishwa na fangasi ambazo hupulizwa na upepo ama kunyunyizia maji mengi kupita kiasi.

Hata hivyo, Gitau anasema zao la stroberi ni la manufaa mengi kwa afya ya binadamu kwani husaidia kupunguza shinikizo la damu mwilini mbali na kulainisha ngozi.

Stoberi pia inaweza kuongezewa thamani kwa kutengeneza siagi ya kiasili ya stroberi kama wanavyofanya wakulima wengi kutoka eneo la Ol-Joro-Orok, Kaunti ya Nyandarua.

Kuongezea stroberi thamani ni njia mojawapo ya mkulima kujiongezea kipato na kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana wanaoweza kutumika kama ‘mabalozi’ wa kutembeza bidhaa hizi kwa wanunuzi.