Makala

AKILIMALI: Mbinu mpya ya kilimohai kukuza matundadamu

December 24th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Ikiwa kuna uamuzi anaojivunia ni kuingilia ukuzaji wa matundadamu, kutokana na oda chungu nzima alizopata na anazoendelea kupata za matunda hayo.

Licha ya kuwa Charity Kigera ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), anasema hatua aliyochukua ni ya busara kwani yuko safarini kuafikia matamanio yake – kuwa miongoni mwa wakulima wanaosadia kutatua uhaba wa matunda nchini.

“Nimekuwa nikitamani sana kufanya kilimo cha matunda, na kuingilia ukuzaji wa matundadamu ni mwanzo wa safari ya kulisha taifa kwa matunda,” anasema mkulima huyu mchanga.

Maajabu aliyofanya kiasi cha shamba analolima tree tomato eneo la Nyandarua kuwa kivutio kwa kila mmoja, anasema msingi wa ufanisi huo ni utafiti wa kina aliofanya, ambao unajumuisha kusoma makala ya kilimo kwenye intaneti na mkulima aliyempa tunda. Hata ingawa ni chipukizi, anasema hakushuhudia ugumu vile kukuza matundadamu yanayoendelea kumtia tabasamu.

Maandalizi ya miche kitaluni yalichukua muda wa miezi mitano. “Shamba niliandaa kama linavyoandaliwa kupanda mimea mingine,” anadokeza. Kulingana na Charity, aliandaa mashimo yenye kina cha urefu wa futi 2 hadi 3, kuenda chini. Upana wa shimo unapaswa kuwa futi 4.

“Nafasi ya shimo moja hadi lingine kwenye laini niliipa mita moja, huku nafasi ya laini hadi nyingine ikiwa ni mita moja na nusu,” anafafanua. Kinachochangia mazao ya Charity yawe na ushindani mkuu sokoni, ni kuyalima kwa kuzingatia mfumo wa kilimohai. Kimsingi, anadokeza kwamba hakutumia fatalaiza.

“Nilitumia mbolea ya mbuzi, nikachanganya vijiko viwili vya kinyesi kilichoiva na ndoo moja ya udongo,” anasema. Wataalamu wa kilimo wanashauri mbolea ichanganywe na udongo wa juu, uliotolewa kwenye shimo.

“Udongo wa juu ndio bora zaidi kuuchanganya na mbolea au fatalaiza,” anasisitiza mtaalamu Edwin Njiru. Matunzo ya matundadamu yanajumuisha kuyanyunyizia maji, kupalilia dhid ya kwekwe na dawa kukabili magonjwa na wadudu.

“Badala ya kutumia fatalaiza kunawirisha mazao, nilitumia mbolea ya mbuzi tunaofuga,” anadokeza Charity. Mkulima huyu anasema mitundadamu ikiwa michanga, inapoanza kuchana maua na kutunda, inahitaji maji kwa wingi.

Aidha, hutegemea maji ya mvua na kisima chenye urefu wa futi 100 walicho nacho. Matundadamu yanachukua takriban mwaka mmoja kukomaa, kuanza mavuno.

Ekari moja inakadiriwa kusitiri mitundadamu 1, 000. Kwa kuzingatia taratibu faafu kitaalamu, mti mmoja una uwezo kuzalisha wastani wa kilo 125 kwa mwaka.