Makala

AKILIMALI: Mbuzi wa maziwa wana faida ukizingatia vigezo na masharti

December 13th, 2018 2 min read

NA SAMMY WAWERU

Mbuzi wanafugwa nyumbani kwa minajili ya maziwa, nyama na wengine wakitumia ngozi yake kuunda viatu, mishipi, mikoba na kuamba ngoma.?Wanyama hawa hufugwa kwa gharama nafuu, kwa kuwa ni wastahimilivu wa ukame na maradhi.

Isitoshe, wanaweza kufugiwa kwenye eneo dogo. Aidha, muda wao mfupi wa kuzaa humwezesha mfugaji kuwa na mbuzi wengi kwa kipindi kifupi.?Joseph Mathenge ni mfugaji wa wanyama hawa mtaani Mwihoko, Ruiru kaunti ya Kiambu na anasema anaendesha shughuli hii kwa ajili ya maziwa pekee. Anaeleza kwamba ufugaji wa mbuzi ni rahisi na una gharama ya chini ukilinganishwa na mifugo wengine.

Anasema hutumia muda mfupi mno kwa siku kuwahudumia, akifichua kuwa siri ya ufugaji kwa mifugo wowote wale ni kuhifadhi kiwango chao cha usafi; wao wenyewe na katika mazizi yao.

“Usafi unaanzia zizi wanaloishi, lishe yao iwe safi hasa vifaa wanavyotiliwa chakula na maji,” adokeza.

“Jambo la kwanza ninalofanya asubuhi ni kufagia mazizi ya mbuzi wangu, kuosha vifaa vya maji na chakula. Kifuatacho huwa kuwawekea lishe na maji kisha kukama wale wa maziwa,” anafafanua.

Bw Mathenge anashauri haja ya kuwalisha chakula bora na sahihi, pamoja na kuweka kumbukumbu za uzalishaji.?Aidha, huwapa chakula kilichokauka; nyasi aina ya hay, unga maalum wa mifugo uliosagwa, kando na Lucern na Boma rhodes.

“Chakula kilichokauka hakina wadudu wala maradhi, huwawezesha kunywa maji mengi ili chakula kisagike upesi mwilini. Kwa jumla, maji ni kiungo muhimu kwa mifugo kama yalivyo kwa binadamu,” aeleza.

Anasisitiza kuwa mfugaji azingatie lishe bora ya mbuzi wanaokamwa na vibui wake, yaani watoto. Wataalamu wa masuala ya mifugo wanapendekeza watoto wanyweshwe maziwa ya kutosha siku za kwanza za kuzaliwa.

“Maziwa ya mbuzi yana viinilishe na madini tele, yanayosaidia vitoto kukua kwa siha bora,” anasema Okuta Ngura, daktari wa mifugo na ndege, hasa kuku.?Endapo mbuzi wanaonyesha dalili za maradhi au kushambuliwa na vimelea, ni vyema mfugaji kuomba ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mifugo ili watibiwe mara moja. Hata hivyo, Dkt Ngura anasema mbuzi wana chanjo yake sawa na kondoo ama ng’ombe, haswa wakiwa wachanga kwa sababu ya magonjwa ibuka na minyoo.

Zizi la mbuzi nalo latakiwa liundwe namna ambayo litaweza kuwakinga dhidi ya mashambulizi ya wanyama hatari. Mathenge anasema litengenezwe mahali pasipotua maji.

Mazizi yake ameyaunda kulingana na umri wa mbuzi, na yana ukubwa unaomuwezesha kufanya usafi ipasavyo.?Anapendekeza paa liundwe kwa mabati kiasi kuwa mvua inyeapo maji hayataingia.

Viambaza viwe vya mbao na imara, vinavyoruhusu mwangaza na hewa ya kutosha kupenyeza. Vilevile, sakafu yake iruhusu kinyesi na mkojo kudondoka chini. Anasema mbolea ya mbuzi wake huitumia kukuza mboga na miwa kwenye bustani yake.

Kuna aina mbalimbali ya mbuzi wa maziwa kama; Guernsey, LaMancha, Alpine, Nubian, Saanen, Toggenburg, Oberhasli, Sable na Nigerian Dwarf. Mathenge hufuga Alpine, wenye asili ya mbuzi wa Kiafrika na wale wa Ujerumani. Manufaa ya mbuzi hawa ni kwamba huishi katika mandhari yoyote, na kustahimili hali yoyote ile ya anga.

“Alpine wa kike anapoanza kukamwa huwa hapunguzi kiwango chake cha maziwa, hadi wakati wa kujamiishwa,” aeleza. Mbuzi wa maziwa akitunzwa vizuri hatakuangusha katika uzalishaji wake, kulingana na Bw Mathenge.

“Asubuhi mmoja hunipa kati ya lita moja na nusu hadi mbili za maziwa, kiwango hicho kikiwa sawa na cha jioni,” afichua.?Hii ina maana kuwa mbuzi mmoja kwa siku humpa kati ya lita 3-4. Aghalabu, lita moja ya maziwa wa mbuzi hugharimu Sh200.

Mbuzi wa Alpine huzalisha maziwa kwa muda wa miezi minane mfululizo, kisha anajamiishwa. La kutia moyo kwa aina hii ya mbuzi ni kuwa huzaa mapacha.?Wateja wa mfugaji huyu ni hospitali kadha eneobunge la Ruiru na wakazi wa Mwihoko.