Makala

AKILIMALI: Mbuzi wa nyama wamletea faida kuliko wa maziwa

March 26th, 2020 3 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

ILI kuwa mfugaji hodari wa mbuzi wa nyama, kunayo mambo muhimu ambayo mtu anapaswa kuzingatia.

Kulingana na Bw Peter Tanui wa eneo la Kimilili kaunti ya Trans-Nzoia, amefuga mbuzi wa nyama kwa muda wa miaka 11 bila matatizo.

Bw Tanui ni mtaalamu wa masuala ya Kilimo na pia amesomea taaluma ya kilimo biashara katika chuo kikuu cha Jomo Kenyatta cha Sayanzi na Teknolojia (JKUAT).

“Cha muhimu ni kuhakikisha mbuzi wako wanakula vyema na wanapata nafasi ya kutembea na kutafuta lishe mbadala. Hawafai kutegemea nyasi tu,” Bw Tanui aliambia Akilimali ilipozuru nyumbani kwake.

Na katika eneo la shamba lake ekari mbili na nusu, Bw Tanui amefuga zaidi ya mbuzi 40, wakubwa kwa wadogo.

Anasema idadi hii huongezeka au kupungua ikizingatia kwamba mara kwa mara yeye hununua na kuuza mbuzi hao baada ya muda fulani ili kupata riziki yake ya kila siku.

Jambo la kwanza Tanui alisema mfugaji anapaswa kujua aina ya mbuzi ambao anataka kufuga. Hii itamsaidia kujua kiwango cha gharama ambayo anahitajika kutumia wakati anapofuga na pia kuwa na ufahamu wa soko ikizingatia sehemu anakoishi.

“Watu wengi wanapenda kula nyama ya mbuzi ambaye amenenepa vizuri. Mbuzi mwenye ngozi ilionyooka na kukauka vyema huwa na faida ya juu kwa sababu ngozi hiyo huvutia soko la nje ya nchi kama vile Marekani. Nyuzi zake pia huwa na manufaa kwa mambo mengi,” akasema Bw Tanui.

Kulingana naye, alichagua kufuga aina tatu bora za mbuzi ambao wanajumuisha Alpine, Saanen na Galla ambayo ni bora katika mazingira ya Afrika Mashariki.

Jambo la pili ni jinsi ya kujenga makazi ya mbuzi wako na kuweka ua sehemu yote ambayo itatumika kwa lishe. Ua husaidia kuzuia mbuzi kwenda mbali au kuharibu shamba la mboga na mimea nyingine.

Sehemu wanapolala na kula mbuzi inapaswa kuinuliwa juu ili kuwepo na nafasi kati ya sakafu na eneo la malazi.

Nafasi hii hutumika kumpa mfugaji wakati mwepesi wa kusafisha eneo nzima na kuondoa uchafu wa choo ya mbuzi ambayo pia hutumika kama mbolea kwa ukulima wa mimea.

Usafi wa mara kwa mara na wa hali ya juu Bw Tanui alisema husaidia kuepusha mbuzi na mkurupuko wa magonjwa.

“Siri kubwa kwa ufugaji mzuri wa mbuzi ni kuzingatia usafi. Sehemu ya kulala ya mbuzi inapaswa kuwa safi wakati wote. Aidha, sehemu ya lishe haifai kuwa na uchafu wala makaratasi ya plastiki ambayo husababisha maradhi na hata kifo,” akasema.

Bw Tanui alieleza kwamba mambo aliyozingatia kwa aina wa mbuzi anaofuga ni muda ambao mbuzi hao huchukua kabla ya kukomaa.

“Mbuzi aina ya Alpine huchukua takribani muda wa miezi 5 kabla ya kukomaa na kuwa tayari kwa soko huku Saanen wakichukua miezi 5 pekee,” akasema Tanui na kuongeza kwamba Galla huchukua miezi 4 tu.

Gharama ya kufuga mifugo hawa ni ndogo na kila mfugaji anaweza kupata fursa ya kuifanya kazi hii ikilinganishwa na ufugaji wa wale wa maziwa na ng’ombe.

Asilimia 90 ya chakula cha mbuzi huwa ni nyasi ya kawaida lakini Bw Tanui anasema vyakula vingine kama vile mbegu za alizeti na malenge, matawi ya miti halisi, karoti na mboga za majani husaidia mbuzi kupata madini ya protini, vitamini na kalisi.

“Vyakula hivi husaidia mbuzi kuongeza kilo kwa kasi na ikiwa ni mbuzi wa maziwa basi mfugaji na uhakika kwamba mbuzi wake wataongeza kiwango cha maziwa mara dufu,” akasema.

Maji safi ya kunywa pia ni muhimu sana kwa afya ya mbuzi.

Faida kubwa kwa mfugaji wa mbuzi wa nyama Bw Tanui alisema, huzingatia uzito wa mbuzi hao haswa wakati wa mauzo.

Mbuzi mwenye uzito mkubwa humpa mfugaji pesa nyingi ikilinganishwa na mbuzi aliye na kilo chache.

Jambo lingine la kuzingatiwa na mfugaji kulingana na Bw Tanui ni kuwa na soko la kuaminika.

Swala hili husaidia mfungaji kupata muda wa kulisha mbuzi baada ya kununua na kabla ya kuuza.

“Mfugaji anapaswa kuwa na wakati mwafaka wa kununua na kuuza mbuzi wake. Ikiwa ananunua mbuzi wachanga kila mwezi wa Februari, anapaswa kuwalisha kwa kipindi cha miezi sita hivi kabla ya kufungua soko,” akasema.

Muda huu huwa muhimu kuchunguza jinsi mbuzi wanavyokuwa. Mfugaji hupata pia fursa ya kujua iwapo anapaswa kubadilisha au kuzingatia aina ya mbuzi anaofuga na lishe yao.

Mfugaji anapaswa pia kuwa ma ini wakati wa kuweka mipangilio ili kupata faida bora.

Bw Tanui alisema licha ya kwamba gharama ya ufugaji wa mbuzi ni rahisi ikilinganishwa na ufugaji wa wanyama kama vile ng’ombe na nguruwe, mipangilio ya mapema kuhusu jinsi ya kuwa mfugaji bora hutoa mwelekeo kamili. Mbuzi wa nyama aliyekomaa vyema wa aina ya Galla huuzwa kati ya Sh10, 000 na Sh15, 000 ikizingatia msimu na soko. Aidha, mbuzi mdogo wa aina sawia huuzwa kwa Sh6, 000.

Hata hivyo, Bw Tanui alisema mbuzi aina ya Alpine huwa na bei ya juu ikizingatia ubora wake. Mbuzi mdogo wa Alpine huuzwa kwa Sh20, 000 na aliyekomaa huuzwa kwa Sh25, 000.

Kwa mwaka mmoja, Bw Tanui alisema biashara ya mbuzi humpa kati yaSh400, 000 na Sh500, 000 ikizingatia msimu na soko.