AKILIMALI: Mfumo wa Hydroponic na mbinu asilia kukabili magonjwa na wadudu

AKILIMALI: Mfumo wa Hydroponic na mbinu asilia kukabili magonjwa na wadudu

Na SAMMY WAWERU

UGONJWA wa Fusarium wilt ni kati ya changamoto zilizohangaisha wakulima Harun Njoroge na Miriam Karuitha katika safari yao kuimarisha shughuli za kilimo.

Ni ugonjwa wa kuvu ambao ukiingia shambani huacha mkulima akikadiria hasara bin hasara.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya kilimo, Fusarium wilt ni ugonjwa wa udongo – yaani unaosalia udongoni baada ya kuathiri mimea, jambo ambalo huufanya kuwa vigumu kuukabili.

“Huathiri viazi, nyanya, biringanya, pilipili mboga, pilipili hoho, mboga na mimea mingine inayoorodheshwa katika familia moja na mboga,” anasema Meshack Wachira, mtaalamu kutoka Novixa International, shirika linalotengeneza na kuuza dawa za magonjwa na wadudu.

Meshack anasema Fusarium wilt huingia kwenye mimea kupitia mizizi na kuathiri njia au mishipa ya kusafirisha maji.

“Kilele huwa matawi na majani kunyauka na kukauka,” mdau huyo anasema, akieleza kwamba dalili ya ugonjwa huo ni mimea kubadili rangi na kuwa manjano.

Hatua za dharura zisipochukuliwa, mtaalamu Wachira anaonya kuwa ugonjwa wa Fusarium wilt unaweza kusalia udongoni kwa muda mrefu, miaka, na husambaa kupitia maji, wadudu na vifaa vya shambani vilivyotagusana na udongo ulioathirika.

Harun Noroge na Miriam Karuitha walipoingilia kilimo 2018 walihangaishwa na ugonjwa huo, kiasi cha kukosa kupata mazao ya kuridhisha ya mboga walizokuza na pia nyanya.

Miriam Karuitha na mume wake wamekumbatia mfumo wa teknolojia ya kisasa, Hydroponic kukabili magonjwa na wadudu. Picha/ Sammy Waweru

Huku matumizi ya dawa kukabili magonjwa na wadudu yakitajwa kuchangia kwa kiasi kikuu maradhi haratari kama vile Saratani, wanandoa hao walitafiti mbinu za kuangazia changamoto zilizowazingira.

Jawabu walilopata, ni kukumbatia mfumo wa teknolojia ya kisasa kuimarisha shughuli za kilimo, maarufu kama Hydroponic System.

Ni mfumo usiotumia udongo kupanda mimea, na badala yake kutumia malighafi asili kama vile; Pumice (unga wa volkeno) na maganda ya mpunga (rice husks- shells).

Miche huikuza kwa kutumia coco peat (maganda ya nje na nyuzi za nazi, yaliyosagwa) na peat moss (mmea asilia wenye kiwango cha juu cha tindikali).

“Kwa kukumbatia mfumo wa hydroponic gharama kukabili magonjwa na wadudu tumeipunguza kwa kiasi kikubwa. Hupulizia dawa haja inapoibuka,” Harun anaelezea.

Wanandoa hao wenye maono makubwa katika kilimo, hukuza pilipili za rangi tofauti kwenye mahema, eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu.

Wana vivungulio viwili vilivyopambwa kwa pilipili mboga nyekundu na manjano, ambapo hudhibiti wanaoingia ili kutosambaza magonjwa.

“Magonjwa ya mimea pia husambazwa kwa njia ya makanyagio na mavazi, na ndio maana huwa haturuhusu watu kuingia kwenye mahema bila idhini na maelekezo,” Miriam anafafanua.

Kwenye lango la kila kivungulio, wakulima hao wameweka maji yaliyotibiwa ambapo anayeingia sharti makanyagio yake yaloweshwe dawa.

Wakulima hao pia hutumia mkojo wa sungura, pilipili kali zilizopondwapondwa, sabuni majimaji, majani ya mmea asilia wa akapulko kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa ibuka.

Isitoshe, pia hutumia mitego maalum ya wadudu katika mdahalo mzima kuafikia kigezo cha kilimohai.

Wanasema tangu wakumbatie mfumo wa Hydroponic na mbinu asilia kukabili magonjwa na wadudu, wameweza kukwepa athari za Fusarium wilt na magonjwa mengine.

Athari za ugonjwa huo pia zinawiana na za Bacterial wilt, David Karira ambaye ni mkulima wa pilipili mboga akiambia ‘Taifa Leo’ kuwa baada ya mavuno hutandaza na kufunika udongo kwa kutumia karatasi kubwa jeusi, muda wa miezi sita mfululizo.

“Huhakikisha udongo hauingizi hewa wala maji. Baada ya kipindi hicho cha muda, magonjwa na wadudu waliomo huangamia,” Karira anaelezea, akikiri Fusarium na Bacterial wilt ni magonjwa hatari.

You can share this post!

Shujaa na Lionesses kuelekea Uhispania usiku wa kuamkia...

Xhaka amjeruhi Lacazette wakiwa mazoezini kambini mwa...