Makala

AKILIMALI: Mfumo wa teknolojia ya kisasa kunywesha kuku maji na dawa

December 21st, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MOJAWAPO ya mahitaji muhimu katika ufugaji wa kuku na ndege wa umaridadi, ndio nyuni, ni kuwepo kwa maji ya kutosha na yaliyo safi.

Usafi katika vizimba vya kuku, lishe na maji unapaswa kuwa wa hadhi ya juu.

Msambao wa maradhi ya kuku na pia vimelea huchangiwa na mazingira machafu, hivyo basi kuongeza gharama kwa mfugaji kupitia matibabu.

Ili kujaribu kudumisha kiwango cha usafi hususan kwenye maji, baadhi ya wafugaji wa kuku wamekumbatia teknolojia ya kisasa kuwanywesha.

Ni mfumo wa matumizi ya mifereji – paipu na mabomba, inayowekwa kwenye vizimba vya kuku na ndege.

Caroline Murigu, mfugaji wa kuku Kaunti ya Kiambu amekumbatia mfumo wa teknolojia hiyo.

“Mfumo huu unaondoa gharama ya kununua vifaa vya kuwawekea maji. Isitoshe, unasaidia kudumisha usafi wa maji wanayokunywa, kwani matumizi ya vifaa wazi huyachafua na pia kuvichafua jambo ambalo ni hatari kwa afya ya kuku,” Caroline anaelezea.

Kukithiri kwa uchafu katika mazingira ya kuku, ni chocheo la msambao wa magonjwa, hasa yanayosababishwa viini.

Mfumo wa kisasa kunywesha kuku maji na dawa kwa njia ya paipu maalumu zenye mifereji. Picha/ Sammy Waweru

Paipu yenye mabomba, yaani tapu zinazodondoa ama kutoa maji kuku au ndege wanapozidona inasindikwa kwenye ukuta wa kizimba.

Idadi ya tapu inalingana na kiwango cha kuku wa mkulima.

“Urefu kutoka sakafuni unapaswa kuwa kimo ambacho kuku watafikia ili kukata kiu cha maji,” anasema Mtaalamu Mutuku, ambaye pia amekumbatia mfumo huo katika mradi wake wa kuku.

Mtaalamu huyo wa masuala ya ufugaji wa kuku na nyuni anasema mfumo wa teknolojia hiyo pia unatumika kuwapa kuku dawa.

Mifereji imeunganishwa na tangi au chanzo cha maji.

“Yanakowekwa maji ndiko dawa hutiwa, kuku wanainywa kwa hiari,” mdau huyo anasema, akieleza kwamba mfumo huo unaondolea mfugaji kibarua cha kukimbizana na kuku, kuwakamata ili kuwapa dawa.

Cha kutia moyo, kando na kuondoa leba ya kuwapa kuku dawa, gharama ya paipu zinazotumika ni nafuu ikilinganishwa na vifaa wazi (water troughs).

Isitoshe, paipu hizo zinadumu muda mrefu.

“Kimsingi, ni mfumo unaorahisisha shughuli za ufugaji wa kuku na ndege na pia kudumisha kiwango cha usafi,” anasisitiza Mtaalamu Mutuku.

Mkurupuko wa maradhi ya ndege kwa kuku ni suala linalohangaisha wafugaji wengi na kuzima ari yao.

Kiwango cha hali ya juu ya usafi kikidumishwa, matumizi ya mfumo huo yakijumuishwa, magonjwa yatakuwa yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.