AKILIMALI: Mhandisi aliyestaafu jeshini sasa ni mfugaji hodari wa mbuzi wa maziwa

AKILIMALI: Mhandisi aliyestaafu jeshini sasa ni mfugaji hodari wa mbuzi wa maziwa

Na PETER CHANGTOEK

KILOMITA chache kutoka jijini Nairobi, katika eneo la Ruai, ndiko anakoishi James Nyaga, 64, mhandisi aliyestaafu kutoka katika jeshi miaka kadhaa iliyopita.

Baada ya kustaafu kutoka katika kitengo hicho, Nyaga, aliamua kufanya shughuli ya ufugaji wa mbuzi wa maziwa, shughuli ambayo anaionea fahari mno.

Mfugaji huyo anasema suala la ukosefu wa shamba kubwa la kuuendesha ufugaji halifai kuwa kizingiti kwa yeyote mwenye nia.

Ploti yake ni kipimo cha robo ekari, na katika sehemu moja ya ploti hiyo, amevijenga vibanda ambavyo huvitumia kuwafuga mbuzi zaidi ya hamsini (50).

Vibanda hivyo vimejengwa kwa mbao na vimeinuliwa kwa urefu wa futi moja na nusu.

Usafi hudumishwa katika vibanda hivyo, na haupo uvundo ambao mara nyingi hupatikana katika mahali panapofugwa mbuzi.

Kwa mujibu wa Nyaga, yeye hupata maziwa lita 2-4 kutoka kwa mbuzi mmoja kila siku.

Hata hivyo, si mbuzi wote ndio hukamwa, kwa kuwa baadhi yao hawajafikia umri wa kuzaa na kukamwa.

Mfugaji huyo anadokeza kuwa yeye hupata jumla ya lita 20-25 kwa siku kutoka kwa wale ambao hukamwa.

Endapo atayauza maziwa yote ayapatayo kila siku, ni dhahiri shahiri kuwa atazipokea pesa nyingi kwa siku, maadamu lita moja ya maziwa hayo huuzwa kwa kati ya Sh150-200.

Hili linabainisha bayana kwamba ana uwezo wa kuzitia mfukoni zaidi ya Sh3,000 kila siku.

Hata hivyo, anadokeza kwamba huyazalisha maziwa kiasi fulani kwa kusudi la kutumiwa nyumbani kwake.

Hapo awali alianza kufanya shughuli ya ufugaji wa mbuzi kwa kusukumwa na uraibu tu aliokuwa nao. Hata hivyo, uraibu huo huo ukakita mizizi na akaanza kuongeza idadi ya mifugo hiyo.

“Nilimnunua mbuzi wa kwanza kwa Sh15,000 kutoka kwa jirani yangu aliyekuwa akizihitaji pesa kwa dharura kule mashambani. Kwa wakati huo mbuzi huyo alikuwa akitoa maziwa nusu kikombe,’’ anafichua Nyaga ambaye hutoka Kaunti ya Embu.

Baadaye, akawanunua wengine kutoka maeneo ya Muranga, Meru, Thika na Embu. Nyaga, ambaye ni baba wa wana watatu, anadokeza kwamba anakadiria mtaji alioutumia kukiasisi kilimo hicho kuwa takriban Sh100,000 pesa taslimu.

James Nyaga akiyauza maziwa ya mbuzi katika duka lao lililoko mjini Ruai. Picha/ Peter Changtoek

Linaloshangaza mno kutoka kwa mfugaji huyo ni kuwa, kinyume cha matarajio ya wengi ambao hudhani nyasi ndizo zitumiwazo tu kuwalisha mbuzi, yeye hatumii nyasi, na hakuna chochote cha rangi ya kijani kibichi katika vibanda wanakolishiwa mifugo hiyo!

“Siku hizi kuna uhaba wa mashamba ya kupanda nyasi na mimea ya kuwalisha mbuzi,’’ anasema, huku akiongeza kuwa mabadiliko ya hali ya anga pia, yamechangia kuadimika kwa nyasi.

Awali, alikuwa akiamini kuwa ufugaji wa mbuzi humhitaji mtu kuwa na nyasi tu, lakini kuzipata nyasi zenyewe, hususan katika maeneo ya Nairobi, kukawa kama kuitafuta sindano katika shamba la mpunga! Lisilo budi hutendwa. Hivyo basi, akashurutika kujitengenezea lishe za kuwalisha mbuzi wake.

“Tulichukua muda wa miaka takriban mitatu kabla hatujapata vipimo na mchanganyiko mwafaka wa lishe. Kwa lishe tunazozitengeneza, mimi hutumia kilo moja yazo, ambazo hugharimu Sh50 kwa kila mbuzi aliyekomaa,’’ anasema, akisisitiza kwamba lishe hizo zina madini 18.

Mfugaji huyo ana aina tatu za mbuzi shambani kwake; ‘Saanen’, ‘French Alpine’ na wale anaowaita ‘Kenya Alpine’.

Mbali na kuwa mfugaji hodari, yeye pia ni katibu wa muungano ujulikanao kama ‘Nairobi Dairy Goats Breeders Association’.

Muungano huo una duka katika eneo la Ruai, viungani mwa jiji la Nairobi, ambalo huyanunua maziwa kutoka kwa wanachama kwa Sh150 na kuwauzia wateja kwa Sh200 kwa lita moja.

Anawashauri wale wanaonuia kuanzisha zaraa ya ufugaji wa mbuzi wa maziwa kutolichukulia suala la ukosefu wa shamba kubwa kuwa kizingiti.

Aidha, anafichua kwamba ufugaji wa mbuzi wa maziwa hauna kazi ya sulubu.

You can share this post!

AKILIMALI: Kibao-mbuzi ni aina mpya ya mbuzi ambayo inaweza...

RIZIKI: Alipenda baiskeli utotoni, sasa ni fundi hodari wa...