AKILIMALI: Mlinzi anayevuna pato kwa kukuza sukumawiki za kudumu kipindi kirefu

AKILIMALI: Mlinzi anayevuna pato kwa kukuza sukumawiki za kudumu kipindi kirefu

Na PATRICK KILAVUKA

JOSEPHAT Baraza Okech amestawisha kilimo cha mboga aina ya sukumawiki ambayo inadumu muda mrefu wa miaka kadhaa.

Shughuli hii yeye hufanyia katika boma la mwajiri wake kwani yeye pia ni bawabu.

Mkulima huyu anasema mja anafaa kutumia akili na fursa ile aliyonayo kufanya kitu cha kumsaidia na jamii pana.

Mapenzi yake makubwa katika ukulima yamemchochea tajiri wake kumpa sehemu pembezoni mwa boma kuimarisha nyenzo za kilimo cha mboga hiyo ambayo inamsaidia kutia hela mfukoni.

Alianza ukuzaji bila mtaji. Kwa kutumia tu fursa aliyopewa na tajiri pamoja na bidii na ari, sasa analisha jamii pana na kuuzia hata mahoteli. Kando na kupanda mboga za kiasilia, hupandamiche ya matunda.

Kwa miaka mitatu sasa, anasema kilimo chake kimenawiri na anatiwa moyo zaidi wakati wateja wanajitokeza kumnunulia kazi ya mikono yake kwa moyo mkunjufu huku wanausifu ukulima ambao umefaulu japo sehemu ni ndogo.

Alianzaje? Baraza bila kuficha anafichua kwamba, ukuzaji wake wa sukuma ulianza bila hata senti kwani mbegu ya sukuma alipewa na mama mmoja ambaye alikuwa ameipanda kwake.

Mkulima Josephat Baraza Okech akivuna sukumawiki pembezoni mwa boma la tajiri wake liliko mkabala wa barabara ya Muguga Green, Westlands. Picha/ Patrick Kilavuka

“Nililetwa mbegu kumi za sukumawiki na mama huyo aliyefurahishwa na jinsi nilivyokuwa nikifanya ukulima wa kunde na dania mwanzoni na akanishi kuzipanda,” afichua Okech na kuongezea kwamba, siku iliyofuata alimletea na akapanda pasi na kujua kwamba huo ndio mwanzo wa kukitisha mizizi katika ukulima huo.

Muda si muda, sukumawiki ilinawiri sana na hata akapanua sehemu ya upanzi na wateja waliofika hapo kununua wakawa wanavutiwa na mboga hiyo ambayo sasa inakidhi hitaji la mboga kwa wingi.

Kwa siku, Baraza amekuwa akitia kibindoni Sh300-500 kupitia kuuza kwa wateja wake na mahoteli yaliyo Westlands anakofanyia ukulima wake kwenye mkabala wa barabara ya Muguga Green, Westlands.

Yeye huuza kila kifungu Sh 50 wakati anapovuna.

Hutunzaje aina hii ya mboga? Baraza anasema sukuma wiki ni mboga rahisi sana kukuza ukiwa na ari ya ukulima.

Yeye huipanda na mbolea ya kiasilia kutoka kwa mifugo hususa mbuzi.

“Hutumia mbolea ya mbuzi au ile imetengenezwa kutokana na takaka ninayoizoa. Huichanganya vyema na mchanga na sukuma inashamiri sana jinsi inavyoonekana,” anasema Baraza ambaye hulima mashimo na kisha kuweka mbolea asilia halafu hupanda mbegu aliyotoa kwa sukuma ya kitambo (suckers) na kuipanda moja kwa moja kwenye mashimo.

Hatimaye, huifunika robo tatu ili kuacha sehemu ambayo itahifadhi maji ya mvua au ya kunyunyizia kwa matumizi ya mbegu hiyo kujiotesha na kukua kwani, huhitaji maji mengi ndiposa isinyauke.

Anadokeza sukuma hii hukua kwa haraka sana inapopata matunzo ya kufaa na baada ya kujikitisha, yaweza kuchukua muda mfupi kuanza kuvunwa.

Ili, uliendelea kuvuna mboga hii kwa wingi, anasema baada ya kuvuna, ya kupasa kuiachilia kwa wiki mbili hivi kuzalisha maradufu huku ukiipalilia na kuipa maji kwa wingi kama kuna kiangazi kudumisha mazao yake.

Ameepukana kabisa na matumizi ya dawa za kunyunyuzia kuangamiza wadudu waharibifu na ukungu kwenye sukuma ila, hunyunyuzia maji mara kwa mara hali ambayo inawatokomeza wadudu hao. Aidha, kukinyesha wanaangamizwa na sukuma hupata fursa ya kukua katika mazingira salama na kutoa mazao kwa wingi.

Kuhakikisha kuna ongezeko la mazao na sukuma inazidi kukua juu zaidi, anasema hutoa mbegu zinazochipukia (suckers) na kuipanda tena au kuwauzia wale ambao wanakuja kuinunua kwa minajili ya kupanda.

“Ukiacha mbegu ambazo zinazochipukia kukua kwenye sukuma, itasababisha sukuma kutopata uwezo wa kukua vyema ikienda juu kwa sababu mbegu hizo (suckers) husababisha mngangano wa chakula na kuifyonza hali ambayo inaikosesha kuwa na uwezo wa kujihimili na kuendelea kukua zaidi. Hivyo basi, hutakiwa kuondolewa au kupandwa kama mbegu tena.

Isitoshe, usipomwagilia maji, vijidudu huharibu mtawa ya sukuma kwa kusababisha ukungu unaoiharibu.

Mbali na tajiri wake kumhimiza na kumtia motisha kuendeleza kilimo cha mboga hii, amekuwa mteja wa kwanza hali ambayo imejenga imani yake kwani, licha ya kuwa mlinzi, amempa fursa ya kufanya ukulima siku tatu kwa juma hali ambayo imeinua kilimo hicho.

Mbali na sukuma, amepanda pia miche ya miparachichi, miembe na matunda mengineo ambayo anapanda baada ya kupata mbegu zake kutoka kwa matunda ambayo yananunuliwa na tajiri. Pia, hupenda kupanda maboga ya kiasilia japo shamba limeadimika.

Mboga ya sukuma imekuwa ya faida kwake kwa muda amehusika na upanzi na imemsaidia kujikimu na kusomesha.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa kijiji cha Kihunguro wahangaika baada ya makazi...

Ana matumaini tele kushiriki katika raga ya hadhi akifuata...