Makala

AKILIMALI: Mradi wa ufugaji bata bukini ulivyoleta tija kwa wakulima

May 30th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Uwekezaji katika ufugaji wa aina mbalimbali za ndege, ni miongoni mwa desturi kongwe ulimwenguni.

Bata bukini ni mojawapo ya ndege ambao mkulima atamudu kuwalinda japo kwa gharama; wanapatikana kwenye familia moja na bata wa kawaida.

Isipokuwa bata bukini ni wakubwa kwa kimo, rangi yao ni nyeupe au kijivu na wengine wana mabaka meupe na meusi. Aidha wao hushamiri vyema katika maeneo yenye baridi kali hususan nyanda za juu.

Nchini Kenya, bata bukini hufugwa katika mkoa wa Bonde la Ufa na eneo la Kati kwa mfano Kiambu, Nyeri, Murang’a na Meru.

Akilimali ilipata fursa ya kuzuru eneo la Tumor Hill kaunti ya Nyandarua, kutangamana na wakulima wanaojipatia tija kubwa kutokana na mradi huu.

Milima ya kupendeza ilitukaribisha katika eneo la Tumor Hill, kilomita nane hivi kutoka mji wa Nyahururu.

Tumor Hill inaendesha mradi wa ufugaji wa bata bukini na kuku, ili kutosheleza mahitaji ya ndani kwa ndani, wakati huu ambapo gharama ya bidhaa za mifugo ni ghali.

Patroba Maranga ni mmoja wa wakulima. Kwanza anasema siri ya kuwatunza bata bukini ni kuyaelewa ulaji wao, mazingira wanamokulia, mahitaji ya soko na jinsi ya kukabiliana na mkurupuko wa maradhi.

Pili, anawahimiza vijana kujipatia ujuzi wa kufanya ukulima, ili kuyaboresha maisha yao, katika ulimwengu wa sasa ambapo nafasi za ajira ni finyu.

Patroba alitangulia kufafanua kuwa, umuhimu wa kutoa kiwango sahihi cha lishe kwa bata bukini, ndege wa kigeni ambao wamekulia sana bara Asia.

“Wakati mwingi chakula chao kinahitaji kuchanganywa na nafaka zilizosagwa, maji ya kutosha na kuwaweka ndani ya mazingira safi,” Patroba akasema.

Alieleza kuwa wakati wa kuwafuga, mkulima anahitaji kuwawekea bwawa la maji, hususan idadi yao ikiwa kubwa, ili kuwapumbaza dhidi ya kuzurura katika mazingira jirani.

Agizo hili huwaepushia hatari ya kupata maradhi ya kuambukizana, ama hasara ya kupotea wanapokosa mwelekeo wa kurudi nyumbani.

Ndege hawa wenye milio kama firimbi wana rangi ya kuvutia, hupenda kuogelea na mara nyingi hujipanga wawili wawili wakitafuta sehemu ya kutaga mayai.

Kulingana na Patroba, bata bukini wana hekima nyingi hasa ijapo kwenye suala la kukabiliana na adui. Yeyote anapoingilia mazingira yao na kuwachokoza ama kuiba mayai hana budi kukabiliana nao.

“Huweka ulinzi mkali na kuwafurusha wageni wapya wanaozuru makazi yao, na wakati wa kuangua dume ndio huyalinda mayai,” akasema.

Ingawa malezi yao ni kama kuku wa kawaida, mayai huangua baada ya wiki tatu takriban siku 21 tangu wayatamie mayai.

Bata bukini hutaga kati ya mayai 6-8 kutegemea na mazingira wanamokulia na utulivu wa akili wanaopata. Purukushani na kelele kutoka kwenye sauti za magari au viwanda hukata uwezo wao kutaga mayai kwa wingi.

Kulingana na mkulima huyu, bata jike ndiye hutoa matunzo kwa vifaranga anapowazingira wa mabawa yake na kuwapatia joto.

Vifaranga huchukua kati ya miezi 2-3 kukomaa ndipo wakaanza kutembea japo kwa kuyumbayumba, kabla ya kupata nguvu, kwenye miguu wakasimama tisti.

Patroba Maranga akionyesha bata bukini wanaofugwa Tumor Hill, katika eneo la Nyahururu, kaunti ya Nyandarua.
Picha/ Richard Maosi

Alieleza kuwa kinda ambaye hajakomaa huuzwa kwa Sh1,500, naye bata bukini aliyekomaa huuzwa kati ya Sh5,000-6,000.

Japo Tumor Hill haiuzi bata bukini wake sokoni, msimu wa sikukuu za kitaifa ndio wakati mwafaka ambapo wateja wengi humiminika sokoni.

Aidha, wafugaji wa kibinafsi kutoka maeneo jirani ya Molo, Nakuru, Eldoret na Naivasha humiminika Tumor Hill kujipatia elimu ya kutosha kuhusu ufugaji wa ndege hawa wanaohitaji uangalifu wa hali ya juu.

Pia, taasisi za elimu kama vyuo vikuu vimekuwa vikipata fursa nzuri ya kufanya utafiti kwenye mlima wa Tumor Hill, ili kujiongezea maarifa.

“Nyama ya bata bukini ni kubwa ikilinganishwa na ndege wa kawaida, wao wanaweza kufikisha uzani wa kilo 12 ama zaidi,”alisema.

Lakini Patroba anatahadharisha mfugaji asiyaguse mayai ya bata bukini kwa mikono wakati yakiwa hayajaanguliwa.

Anasema hili hufanya mayai yaharibike kabla ya kuanguliwa ama kuangua mapema kabla ya wakati unaokusudiwa kufika.

Patroba asema mfugaji hana budi kabisa kuhakikisha, ndege wake wanapokea chanjo ya mara kwa mara, ikiwezekana mara tatu kwa mwezi au zaidi.

“Bata bukini wanaweza kuambukizwa maradhi ya Newcastle kama inavyotokea miongoni mwa kuku, anachohitajika kufanya mkulima ni kuwapatia chanjo kila baada ya miezi mitatu,”akasema.

Mkurupuko wa maradhi unaweza kupunguza idadi ya bata, endapo mfugaji hatachukua hatua ya haraka kukabiliana na maradhi.

Maradhi haya husambazwa na vimelea vinavyotokana na virusi na dalili zake ni kama vile kutoa kinyesi cheupe, kupumua kwa taabu na kutikisa kichwa.