Makala

AKILIMALI: Mtaalamu wa kilimo na balozi wa siha njema

June 27th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

CHAKULA kinachoenziwa na kuliwa kwa wingi ni kilichosindikwa.

Baadhi ya vyakula vya kusindikiwa, aghalabu hutiwa kemikali ili kuvihifadhi kwa muda mrefu.

Wataalamu wa masuala ya afya huonya dhidi ya kuvila sana kwa sababu ya athari zinazoibuka siku za usoni, uuguaji wa magonjwa kama Jongo, Kisukari, Shinikizo la damu na Saratani yakiwa miongoni mwazo.

Aidha, wataalamu wa afya wanahoji yanaweza yakadhibitiwa kwa kiwango kikubwa iwapo kila mmoja atazingatia lishe kamilifu. Isemwavyo; kinga ni bora kuliko tiba, ulaji wa matunda ainati, uzingatiaji wa chakula asilia na kile hai, ni baadhi tu ya unachohimizwa kutilia maanani mara kwa mara.

Mbali na kuwa mtaalamu wa kilimo, James Macharia ni balozi wa siha bora kupitia jitihada zake za zaraa ya kipekee.

Malalamishi ya kila wakati watu kuugua ndwele zinazowahangaisha kupata matibabu kama vile Saratani, zilishinikiza mdau huyu kutafuta njia mbadala kuyaangazia.

Ukizuru kiunga chake cha Green Oasis Plants Centre kilichoko Kabati, kaunti ya Murang’a, pembezoni mwa lango utakaribishwa na mimea mbalimbali ya kusawazisha hewa chumbani almaarufu Indoor Air Cleaners, yenye maumbo sawa na maua.

Spider plant, Areca Palm, Peace plant, Mothers-in-law palm, Boston Fern na Rubber plant, ni baadhi tu ya mimea hii anayokuza Bw Macharia.

Mazingira ya makazi tunayoishi, aghalabu kiambaza hupakwa rangi zilizochanganywa na bidhaa za petroli, jokofu, vifaa vya plastiki vya kulia na kunywa, chupa za vinywaji, na mazulia, vyote kwa jumla vikiundwa kwa malighafi yasiyokosa kemikali.

“Nyingi ya bidhaa hizo inapozidiwa na kiwango cha joto huachilia gesi ya Carbon, Benzene na Formaldehyde. Kemikali hizo husababisha magonjwa kama ya Kansa, na mimea ya Indoor Air Cleaners imeumbwa na uwezo wa kuzivuta, na kuachilia hewa safi ya oksijeni,” afafanua mtaalamu huyu.

Shirika la usafiri wa Anga ya Juu Amerika (NASA)mwaka wa 1989 lilifanya jaribio la mimea 50 katika safari yake kwa Sayari mbalimbali, na kugundua inaweza kutumika kuzalisha oksijeni badala ya ile ya kujiundia.

Utafiti wake pia uliashiria kwamba mimea hiyo ni bora katika kusawazisha hewa ya nyumba.

Kiunga cha Bw Macharia na chenye ukubwa wa ekari moja na nusu kimesheheni miche ya matunda aina mbalimbali na miti. Ukila tunda kwa siku husemekana “humuweka daktari mbali nawe”, amekipamba kwa matufaha, mapapai, mapera, tree tomato (ya kuongeza damu mwilini), zabibu, Brazilian cherry, bukini, maembe, ndizi, macadamia, hayo yakiwa machache tu kuyaorodhesha.

Isitoshe, amepanda mimea asilia inayokabiliana na matatizo ya tumbo, kudhibiti usambaaji wa Saratani, ugonjwa wa shinikizo la damu na Kisukari, nayo ni; Lemon grass, Herbal Hibiscuss, Mulberry na Herbal Rosemary.

“Nina mashine maalumu ya kuisaga inapokomaa, unga wake hutengeneza sharubati kwa kuuchanganya na maji moto na asali,” aelezea.

Wataalamu wa afya hupendekeza viungo asilia vya mapishi vitumike, na mkulima huyu wa aina yake huvikuza na kuvizalisha. Wakati wa mahojiano alifichua aina saba ya mimea anayolima, na kuunda bidhaa za aina mbalimbali akiitambua kama ‘mints’.

“Kuna mints aina saba kila moja na matumizi yake. Tropical ni ya kuunda peremende, chokoleti (kando na kuunda chokoleti yenyewe, ni ya kutengeneza dawa za kupiga meno mswaki), pepper (mapishi), spear (kubadilisha rangi ya chakula) na corsican (minukato). Apple na orange, pia zinatengeneza dawa za kupiga meno mswaki,” alifafanua.

Kilimo chake kimeegemea mimea yenye ukwasi wa madini ya Calcium, Potassium, Vitamins na Magnesium. Macharia ambaye ni mzaliwa wa Nyeri, anasema mapenzi yake kwa kilimo ameyapalilia tangu akiwa mchanga. Akivuta mawazo yake nyuma, akiwa katika shule ya msingi alikuwa na kiunga kidogo alichopanda matunda na miti.

Wavyele wake walifurahishwa na juhudi zake na hata kumpiga jeki.

Alikuwa na bahati kama mtende kwani shule ya upili aliyojiunga nayo ilitilia maanani masomo ya zaraa, ambapo alishiriki miradi kadhaa ya kilimo.

La kutia moyo, baada ya kuhitimu kidato cha nne, ombi lake kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton, Nakuru liliitikiwa na akasomea Stashahada ya Kilimo-mseto, masuala ya mimea.

Elimu bora ya kilimo

Egerton ni miongoni mwa vyuo vikuu tajika nchini katika utoaji wa mafunzo bora ya kilimo, na kusomea humo kulimnoa na kumuimarisha katika ari yake.

Safari ya mbali huanza kwa hatua moja, mtaalamu huyu aling’oa nanga mwaka wa 2008 kwa kiunga kilichomgharimu mtaji wa Sh23,000 mtaani Kahawa Sukari, kaunti ya Nairobi. Aidha, kilikuwa pembezoni mwa Thika Super Highway, na mradi wa ujenzi wa barabara hii ulipoanza alilazimika kuondoka akahamia Ruiru, Kiambu mwaka wa 2009.

Changamoto kuu eneo hilo ilikuwa ukosefu wa maji, ikizingatiwa kuwa ufanisi katika kilimo unategemea kiungo hiki muhimu.

Mwaka wa 2010 alipata kiunga Murang’a, alichoko kwa sasa. Hata ingawa hakufichua mapato yake wakati wa mahojiano, alisema bei ya bidhaa zake ni kati ya Sh50-500. Ameajiri wafanyakazi sita, na mitandao ya kijamii kama vile; Facebook, Whats App, OLX na Instagram imemsaidia pakubwa kupata soko la mazao yake.

Ili kufanikisha kilimo cha aina hii, anasema mkulima chipukizi sharti awe na chanzo cha maji ya kutosha na ambayo ni safi.

“Ni muhimu kujua kiwango cha asidi (pH) cha udongo, unaopania kufanya kilimo. Wakulima wanapaswa kutibu udongo kwa kutumia lime, haswa kwa kuzingatia maelekezo ya mtaalamu. Wajaribu kadri wawezavyo kupunguza matumizi ya fataliaza ya kisasa, ili uhifadhi virutubisho,” ashauri mdau huyu, akihimiza haja ya kutumia mbolea hai.