Makala

AKILIMALI: Mtama zao la kutegemewa kuliko mahindi eneo lisilopokea mvua ya kutosha

May 16th, 2019 2 min read

Na FRANCIS MUREITHI

KATIKA eneo moja la Kaunti ya Baringo, kilomita chache kutoka mandhari yanayopendeza ya ziwa Baringo, kuna mashamba yanayovutia macho katika eneo la Olkokwe katika kata-ndogo ya Waseges.

Mashamba haya yamepandwa mmea wa mtama unaokua kwa uzuri licha ya eneo hili kutambuliwa kama eneo kavu kutokana na upungufu wa mvua.
Mkulima Joshua Koima, ni mmoja wa wakulima shupavu wa mtama na shamba lake la ekari mbili limekuwa kivutio cha wengi.

“Niliamua kupanda mtama kwa kuwa upanzi wa mahindi katika eneo hili huwa na mazao finyu kwani unahitaji mvua nyingi ilhali mavua inayopitakana hapa ni chache mno kila mwaka,” anasema Bw Koima.

Aidha, Bw Koima ni mmoja wa wakulima wa mtama wanaopanda zao hili kupitia mradi wa Sinendet unaowajumuisha wakulima kutoka maeneo yasiyo kavu sana na yaliyo kavu zaidi (ASAL).

Mradi huu wa Sinendet unawaleta pamoja zaidi ya wakulima 20 wakiwa na lengo la kuimarisha kilimo cha mtama na kujipatia donge nono.

“Kabla ya wataalamu wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Egerton na taasisi ya kimataifa ya utafiti ya maeneo yasiyo kavu (ICRISAT), wakulima wengi hapa walikuwa wanapanda mahindi na mtama ambao mbegu zake hazikuwa zimeidhinishwa na hivyo kuwafanya wapate hasara badala ya faida,’’ anasema Bw Koima.

Hata hivyo hali ya kilimo cha mtama katika eneo hili imebadilika na kuwa kilimo cha faida kwani sasa wakulima wanapanda mbegu mpya ya mtama ijulikanyo kama mtama gredi nambari moja na kujipatia mavuno mengi.

Na ili kuimarisha kilimo hiki cha mtama, wakulima katika eneo hili hali kadhalika huchanganya upanzi wa mtama kwa kupanda sambamba mazao mengine kama vile maharagwe, kunde, njugu karanga na ndengu.

Bw Samson Kaibon, mwenye umri wa miaka 42, ambaye pia ni mkulima wa mtama kutoka kata ndogo ya Olkokwe huvuna magunia 10 ya mtama kutoka shamba lake la ekari moja na kuzoa Sh100,000 baada ya kuyauza sokoni.

“Faida hii ilinishangaza mno hata sikuamini macho yangu kwani hii ni faida ambayo ni mara tatu ya zao la mahindi na tangu nipate faida hiyo kubwa sijawahi legeza kamba na kilimo cha mtama na sibanduki,” anasema Bw Kaibon.

Kwa mujibu wa Bw Kaibon, mbegu mpya ya mtama huchukua takribani miezi mitatu kukomaa ili hali mbegu ambazo hazijaidhinishwa huchukua hadi miezi sita kukoma.

“Kupanda mahindi katika eneo hili ni sawia na kucheza karata lakini tangu nianze kupanda mtama sina la kujutia au kuwaza kutokana na upungufu wa mvua kwani zao la mtama halihitaji mvua nyingi na ndiposa mimi hupendelea kupanda mtama kwani ni na uhakika wa kupata mazao kemkem,” anakiri Bw Kaibon.

Kabla ya kuhamia kilimo cha mtama Bw Kaibon alikuwa anavuna magunia nane za mahindi na baada ya kuyapeleka sokoni na kuuza kwa bei ya Sh2,000 kwa kila gunia la kilo 90 alijipatia faida ya Sh16,000.

Changamoto

Hata hivyo kilimo cha mtama kina changamoto zake si haba ambazo nyakati nyingine huwakanganya wakulima.

Tatizo nyeti hapa ni ndege aina ya mzingi (weaverbird) na kwelea (quelea) ambao hushambulia mmea wa mtama hasa wakati unaanza kukomaa na kufyonza maji na kufanya unyauke.

Na ili kukabiliana na tatizo hili, wakulima hawa wamewaajiri vijana ambao hurauka mapema kuanzia saa kumi na mbili asubuhi na kuwafurusha ndege hawa na kisha kurudi tena mashambani kuanzia saa kumi hadi saa kumi na mbili unusu jioni wakati ndege wanafanya marejeo mashamba.

Eneo hili kwa mujibu wa watalamu wa kilimo nyanjani hupokea mvua ya kati ya milimita 500 hadi milimita 1,000 kila mwaka ambayo inatosha kwa kilimo cha mtama.

Mtama hauathiriki sana kutokana na upungufu wa mvua.