Makala

AKILIMALI: Mtangazaji maarufu aliye na ari ya kustawisha ukuzaji mboga za kiasili

March 14th, 2019 2 min read

Na PETER CHANGTOEK

SYOKIMAU ni eneo lililo kavu mno na jua kali katika sehemu hiyo hulifanya eneo lenyewe kuwa na joto jingi.

Ni muhali mno kuzisikia sauti za nyuni wakiimba.

Yamkini kwa sababu ya ukosefu wa mvua katika eneo hilo.

Ni nadra sana kupatikana kwa shughuli za zaraa katika sehemu hiyo, ila ujenzi wa nyumba za maskani unaendelea kwa kuwa watu wengi wamezinunua ploti ambazo wananuia kuyajenga maskani.

Licha ya jua kali na joto jingi lililopo katika eneo hilo, mtangazaji mmoja maarufu hushughulika na ukuzaji wa mboga asilia.

Bw Jacob Mogoa, mtangazaji katika kituo cha redio cha China Radio International (CRI), amekuwa akishughulikia uzalishaji wa mboga za kienyeji tangu ahamie eneo hilo, lililoko kilomita chache, upande wa kushoto kutoka kwa barabara kuu ya Nairobi-Mombasa, ukielekea Mlolongo.

Hapo awali, alikuwa akiyatumia mashamba ya kukodi ili kukiendeleza kilimo cha ukuzaji wa mboga asilia katika maeneo kama vile Rongai, Kiserian na Kitengela.

Hata hivyo, baada ya kulinunua shamba na kuijenga nyumba yake binafsi katika eneo la Katani, Syokimau, aliamua kuguria eneo hilo na kuanza kukiendeleza kilimo chicho hicho.

Je, ni lipi lililomsukuma kujitosa katika ukuzaji wa mboga za kienyeji?

Ari ya kuyazalisha mazao bora yasiyokuwa na madhara wala athari mbaya kwa binadamu ndiyo iliyomshurutisha kujitosa katika kilimo hicho.

“Ukiangalia vyakula tunavyonunua kutoka kwa supamaketi wametia dawa sana na vyakula vyetu havikubaliki Uropa kwa sababu wamepiga marufuku matumizi ya viuadudu (pesticides) na viuagugu (herbicides),” asema Mogoa.

Anasema njia aula zaidi ya kuepuka maradhi kadha wa kadha, ni kujikuzia mboga zake za asili, ambazo zitamfanya awe salama.

“Nilikuwa nikikuza na nikichuma, nilikuwa nikiwapa marafiki na kuwauzia, lakini ilifika wakati ambapo nilisema hakuna haja niwauzie, nikaanza kuwapa tu,” aongeza Mogoa ambaye amewahi kuhudumu katika mashirika mbalimbali, mathalani KBC, miongoni mwa mashirika mengine, kabla hajajiunga na CRI.

Ploti yake ni futi 100 kwa 100, na ametumia nusu ya ploti hiyo kuwa bustani anayoitumia kuikuza mimea mbalimbali, mathalani mnavu, mchicha, minyanya, pamoja na mboga nyingine nyinginezo za kienyeji.

Aidha, ana mimea michache ya matunda kama vile mikarakara, miparachichi, migomba, miembe, miongoni mwa mimea mingineyo.

Uvimbe

Jambo jingine ambalo lilimsukuma kujitosa katika shughuli ya ukuzaji wa mboga za asili ni wakati ambapo alikuwa mgonjwa kutokana na uvimbe uliokuwapo kichwani na akashauriwa kuzila mboga za kienyeji.

“Niliwahi kuwa na uvimbe kichwani, nilikuwa nimekuja likizoni hapa Kenya, baada ya kukaa Beijing kwa muda wa miaka minne… Nikawa ninaangukaanguka… Nikaenda Beijing na nikatolewa uvimbe huo kwa kutumia teknolojia ya kisasa… Uzuri uvimbe huo haikuwa kansa. Nilizungumza na madaktari wengi wakaniambia niwe nikila chakula kinachotoa sumu mwilini ili kusaidia kuepuka matatizo kama hayo,” asema Mogoa ambaye ni baba wa watoto wawili.

Hapo ndipo alipoamua kuanzisha shughuli ya kuikuza mimea ya mboga asilia.

“Kilimo hiki hakihitaji mtaji mkubwa,” asema mkulima huyo, akiongeza kwamba aliutumia mtaji wa takribani Sh15,000 kuliandaa shamba, kuzinunua mbegu pamoja na kuzitekeleza shughuli nyingine muhimu shambani.

Isitoshe, mkulima huyo anadokeza kwamba kuna wakati ambapo mkewe alikuwa na vidonda vya tumboni, na alipoanza kuzila mboga hizo za kienyeji, akapona kabisa.