Makala

AKILIMALI: Mwalimu anavyotumia teknolojia kuvuna hela kutokana na kilimo mseto Makueni

November 14th, 2018 2 min read

Na FAITH NYAMAI

AKILIMALI ilipomtembelea Bi Bibian Mutavi kwenye shamba lake katika kijiji cha Mutiswa karibu na soko la Barazani, Kaunti ya Makueni, ilimpata akiwalisha ng’ombe wake huku wafanyakazi wakijiandaa kuwakama.

Shamba lake mwanamke huyu kwa jina “Mukalu Farm” linatumia technolojia ya kisasa hali inayowavuta wakulima kutoka sehemu tofauti za kaunti hiyo kuja kumtembela Bi Mutavi kupata masomo ya kilimo biashara.

Bi Mutavi alianza ufugaji huo mnamo Januari 2015. Kwenye shamba hilo la ukubwa wa ekari 10, Bi Mutavi amewafuga ng’ombe wa maziwa 10 aina ya Friesian. Shambani mwake anakuza nyanya, vitunguu, mihogo, mahindi na pilipili hoho.

“Nilipata hamu ya kujihusisha na kilimobiashara miaka nne iliyopita, kwa hivo wakati mwingi nikiwa siko kazini nautumia kuwatunza ngombe wangu na mimea niliyo nayo kwenye shamba langu,” alisema Bi Mutavi.

Bi Mutavi, ambaye pia ni mwalimu wa shule ya msingi iliyoko kilomita chache kutoka nyumbani mwake alisema kuwa kilimobiashara kimeweza kuongeza mapato yake ya kila mwezi.

Alianzisha ukulima huo baada ya kuwekeza  takribani Sh500,000 kutokana na kazi anayoifanya ya ualimu.

Alianza kwa kununua ng’ombe wawili wa maziwa kwa takriban Sh280,000  na kuwatengenezea zizi la kisasa la kuwafugia. Alizidi kuongeza idadi ya  ng’ombe hao ukulima wake ulipozidi kumletea donge nono.

Kati yao,  anawakama watatu na wawili watakuwa wakizaa kwa muda wa miezi mitatu ijayo.

Ili kuhakikisha kuwa ng’ombe hao wanatoa maziwa mengi na hawapatwi na mangojwa mara kwa mara, Bi Mutavi amewatengenezea vyumba vya kulala, sehemu ya kula na sehemu ya kunywa maji.

“Hii inahakikisha kuwa wanakaa kwenye vyumba ambavyo ni safi na hawapati na magonjwa,” alisema.

Huku akisaidiana na wafanyakazi, yeye huwalisha ng’ombe hao asubuhi na mapema mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, saa sita mchana na saa kumi na mbili jioni.

Bi Bibian Mutavi akiwa na mfanyakazi wake John Musembi shambani katika kijiji cha Mutiswa, Kaunti ya Makueni. Picha/ Faith Nyamai Bw John Musembi, mfanyikazi wa Bi Bibian Mutavi akiwakamua ngombe- Picha Faith Nyama

Bi Mutavi amepanda nyasi ya kutosha ambayo huwahusisha wafanyikazi kutengeneza chakula chenye afya kwa ng’ombe hao.

Pia, nyasi hiyo huchanganywa na sukuma wiki, kabichi na mimea ya mahindi ambayo amepanda kwa wingi kwenye shamba lake.

“Tunawachanganyishia pia chumvi na unga wa samaki ambazo hutumika kuwapa ng’ombe hao afya njema,” alisema.

Amemshirikisha pia daktari wa ng’ombe ambaye huhakikisha kuwa amewapa ng’ombe hao chanjo na dawa mara kwa mara. Daktari huyo pia hufuatilia rekodi ya kuwapa mbegu za kiume na kuzaa.

Ngombe hao, Bi Mutavi alisema kuwa ,amewapa majina ya kike kama njia ya kuwatambua na kujua wakati wa mwisho wa kuwapa mbegu za kiume

“Daktari huakikisha kuwa amewapa chanjo mara kwa mara ili kuwakinga kutokana na magonjwa,” alisema.

Kukamua ngombe hao, anatumia teknolojia ya  mashine wa kukamua maziwa kama njia ya kuimarisha usafi.

Kulingana na Bi Bibiana, Mashine hiyo inazigatia usafi wa hali ya juu, na pia inaraisihisha kazi ya kukamua.

“Kabla ya kukamua ngomb’e hao, tunaakikisha kuwa matiti yake ni safi kwa kuyaosha na maji moto,” alisema.

Bw John Musembi ambaye ndiye huwakama ng’ombe hao, alisema kuwa mashine hiyo ni lazima isafishwe na kuhifadhiwa kwenye  mahali safi.

Ng’ombe hao hutoa maziwa ya kati ya lita 20 na 30 kila siku huku akipata lita 75 kutoka kwa ng’ombe watatu anaowakama kwa sasa.

Kila siku, yeye hupata Sh5,250 baada ya kuuza maziwa na Sh157,500 kila mwezi.

Mtalaamu wa ng’ombe wa maziwa Bw Felix Opinya kutoka Chuo Kikuu cha Egerton alisema ni muhimu sana wakulima kuzigatia usafi.

“Ni lazima mkulima aakikishe kuwa maziwa yake ni safi,” alisema.

Kwenye vyumba kulala ngombe hao, Bw Opinya alisema mkulima ni lazima azingatie usafi wa hali ya juu.

Kando ma kuuza mazima, Bi Mutavi huuza mihogo, sukuma wiki, kabichi, mahindi, vitunguu na nyanya kwenye masoko ya Sultan Hamud, Kathonzweni, Salama, Kasikeu na Emali.

Kwenye mazao aliyopata mwezi uliopita, alipata faida ya Sh100,000 baada ya kuuza mihogo na Sh200,000 baada ya kuuza vitunguu.