Makala

AKILIMALI: Namna miradi ya kitamaduni huandaa vigoli kuwa wanawake wa kuheshimika

November 21st, 2019 2 min read

Na LUDOVICK MBOGHOLI

WANAWAKE Warabai wamebuni miradi kadha ya kitamaduni wakilenga kuzima ndoto za wasichana wanaovunja ungo dhidi ya kuingilia ‘anasa’ zinazoweza kuwatenga katika jamii na kuwakosesha wachumba.

Makundi ya miradi ya kina mama yaliyoshiriki majuzi makala ya nane ya sherehe za Rabai Grand Cultural Festival, yalibainisha mbinu zinazotumiwa kukinga wasichana hao dhidi ya ukosefu wa heshima kwa waume wao katika siku zijazo.

“Tumeanzisha miradi ya kuwafunza namna ya kuishi katika ndoa na kuimarisha uaminifu kwa waume zao” akasema Bi Luvuno Joha wa kundi la Amani Chela katika mahojiano na Akilimali.

“Miradi tunayowafunza wasichana hawa ni ya upishi wa kitamaduni, jinsi ya kuwapikia waume viazi vitamu vya kienyeji, kuwaandalia mihogo ya kuchemsha, mikate ya ndizi (au mabumunda) na mihogo ya nazi” Luvuno adokezea Akilimali.

Aidha aliambia Akilimali kuhusu mafunzo ya uandalizi wa kunde za nazi, mabenda ya kuchemsha, mchicha (Kirabai ‘Kisonya’), mchunga na sima au ugali (almaarufu Wari) ni lazima wasichana hao wayaelewe vyema.

“Ni lazima waelimishwe kwa uwazi namna ya kuandaa vyakula hivyo. Kabla binti hajaolewa au kwenda kwa mume, ni lazima tumfunze mapishi haya ili asiende kumpa mumewe matatizo na kutuletea aibu kwenye boma” asema Bi Luvuno.

Kupitia kwa Luvuno Joha, Akilimali imebaini kina mama hao pia huwashauri mabinti wanaotarajiwa kuolewa.

“Tuna majukumu muhimu mno katika jamii zetu za Warabai. Tuna wakusanya mabinti na kuwafundisha namna ya kuimarisha miradi ya upishi” anaelezea Bi Luvuno huku akishikilia kuwa kila mama anachukua mabinti wawili au watatu kwa lengo la kuwafunza upishi na jinsi ya kukaa na kuishi na mume.

“Hata kulima, tunawafundisha maana wengi wao wamezoea mambo ya Kizungu,” Luvuno aarifu zaidi Akilimali kwenye mahojiano.

Kulingana naye, mabinti hao pia hufunzwa jinsi ya kucheza ngoma za kitamaduni na namna ya kuvalia mavazi ya kitamaduni kama hatua ya kulinda na kudumisha mila na desturi za Warabai.

Naye Bi Asha Juma anadai kuwa wasichana wanaoshindwa kuzingatia miradi ya utamaduni wa Kirabai, wakibahatika kupata waume wa kuwaoa, watashindwa kuimarisha ndoa zao.

“Kama binti anashindwa au hataki kuzingatia ushauri tunaompa, basi hana bahati ya kuishi vyema na mume. Akiolewa, anaweza kumaliza mwaka au miaka miwili tu na arejeshwe kwao,” anasema Bi Asha Juma.

“Kwa mfano, mbali na mafundisho ya upishi tunayompatia msichana, pia tunamfundisha ajue zaidi jinsi ya kujikimu kimaisha akiwa hana mchumba” Bi Asha anafafanua.

“Ni lazima binti ajue upishi na mambo mengine muhimu ya unyumba. Kwa mfano, anapaswa pia kufahamu jinsi ya kutengeneza vifaa vya matumizi nyumbani” asema Bi Asha huku akitolea Akilimali mfano.

“Vifaa ambavyo binti anapaswa kufahamu kutengeneza ni kama hivi unavyoona hapa, kuna kaha za kunywea maji, pawa za kukorogea mboga chunguni au sufuriani, vikapu na vikahana” Bi Asha Juma aambia Akilimali huku akionyesha baadhi ya vifaa hivyo.

“Kama alivyotangulia kusema mwenzangu, hatukubali wasichana wetu hapa Rabai waende kwa waume wakiwa hawafahamu lolote. Hii ndiyo sababu wazee walishauriana wakaamua kina mama tuwe mstari wa mbele kuhakikisha wanapata mafunzo ya kitamaduni kabla ya kuolewa” akariri Bi Asha.

“Mbali na yote haya, msichana wa Kirabai pia anahitajika kufahamu na kuzingatia yote anayoambiwa na mumewe. Waume wetu ni wahifadhi wa miti inayokua katika misitu yetu, hivyo wanawake ni lazima wafahamu miti muhimu na isiyo muhimu” anaelezea.

“Kuna miti muhimu ya kuenziwa na kutunzwa kama Minyenze, mibamba kofi (ya mbao) na mizaphe ambayo wanawake wanakatazwa kuikata na kuitumia kwa makaa au kuni” aarifu zaidi Asha Juma.

Inadaiwa dhamira ya wanawake kuwafunza wasichana kuitambua miti hiyo ni kutaka kuwaepusha kuikata ovyo na kuitumia kama kuni au kuichoma kwa ajili ya kutaka kupata mkaa.

“Kutunza mazingira ni miongoni mwa miradi yetu kwa mabinti wanaoelekea kubalehe, lazima waelewe kutunza miti na kuhifadhi mazingira ya misitu” Bi Asha Juma apasha Akilimali kwenye mahojiano.