AKILIMALI: Natija itokanayo na kujua mahitaji ya ufugaji mbuzi

AKILIMALI: Natija itokanayo na kujua mahitaji ya ufugaji mbuzi

Na HAWA ALI

MBUZI wa maziwa ni mifugo iliyo bora kwa wafugaji wadogo wadogo, kwa kuwa ni rahisi sana kufuga na kutunza, wanahitaji eneo dogo, ni rahisi kulisha na kumpatia mfugaji maziwa mengi kuliko ng’ombe wanaohitaji mfugaji kuwa na eneo kubwa, chakula kingi na wana gharama kubwa kuwatunza.

Mbuzi wanaofugwa ndani malisho yao makuu ni majani. Aina nyingine za majani zinatumika wakati ambao yanapatikana tu. Ingawa chakula kinapatikana cha kutosha, na kupatiwa kiwango kidogo cha chakula cha ziada chenye virutubisho kama vile pumba aina ya diary meal, kuna upungufu mkubwa wa majani ya msimu.

Kwa hivyo mbuzi wanalishwa zaidi kama sungura. Hili linaweza kuepukwa tu endapo mbuzi wataachiwa huru au kulishwa kwa kutumia majani ya msimu.

Watu wengi huchukulia, ni lazima kumfunga mbuzi kwa kamba. Hili kamwe lisifanyike kwa kumfunga mbuzi kamba mguuni. Si tu kuwa huu ni ukatili, lakini pia inaweza kusababisha mbuzi kujeruhiwa vibaya. Mbuzi afungwe shingoni kwa kamba wakati wote. Ni lazima kuhakikisha kuwa vyovyote utakavyomfunga mbuzi kamba shingoni, imwachie huru mbuzi kuzunguka zizini, vinginevyo kamba fupi inaweza kumkaba mbuzi na kumhatarisha.

Mazoezi na kucheza

Mbuzi wadogo wanaonesha uwezo wa kucheza na kurukaruka katika kipindi cha siku mbili toka kuzaliwa. Wanaonyesha utofauti wa maeneo ya kuchezea kwa kuruka vitu vili vyopo juu ya ardhi. Hii ni hatua muhimu sana katika ukuaji wao

Ni vizuri mbuzi wakaachiwa kuruka ruka huku na kule na kucheza kuimarisha afya. Endapo wataachiwa huru ni wazi kuwa wanakuwa na furaha na ni wazi watakuwa vizuri. Mazoezi yatafanya mifupa na misuli kukomaa vizuri. Inawezekana pia hata kwa mbuzi wanaofugwa ndani kuwekewa vitu watakavyokuwa wanaruka juu yake, mfano unaweza kuwawekea mawe, matairi, au hata gari bovu ili wapande na kushuka.

Uangalizi wa wanachokula

Kama unaweza kuwaachia mbuzi wa maziwa uhuru, utagundua kuwa ni wepesi sana kutambua wanachokula. Kwa lugha nyingine hawaharibu mazingira kwa kula kila kitu kama ilivyo kwa mbuzi wanaofugwa ndani. Wote utawaona wakila aina moja ya chakula na baadaye kuhamia katika aina nyingine. Kwa njia hii inakuwa ni rahisi kwao kupata vitamini, madini na virutubisho vingine kutokana na aina ya mimea inayowazunguka kwa wakati huo na baadaye kubadili chakula, hata kama ni majani tu. Hata hivyo watahitaji chakula cha ziada chenye virutubisho kama vile diary meal na molasesi, endapo wanatarajiwa kutoa kiwango kizuri cha maziwa. Mbuzi wanaokamuliwa wakilishwa vizuri, wanaweza kutoa lita 3-7 za maziwa kwa siku.

Chanjo

Ni furaha ya mfugaji kuona mbuzi wakipata chanjo kwa usahihi. Chanjo dhidi ya ugonjwa wa miguu na mdomo ni lazima, hasa katika eneo ambalo kuna mifugo mingi iliyowekwa katika eneo moja. Ni lazima wachanjwe kila mwaka dhidi ya virusi vya nemonia ya mbuzi. Hii ni aina ya bacteria hatari sana wanaokaa kwenye udongo. Inapotokea pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mifugo aliyeko katika eneo lako.

Dawa ya Minyoo

Ni muhimu kuwapa mbuzi dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu au minne. Tofautisha tiba ya aina nyingine na ya minyoo ili kuepuka madhara yanayoweza kutokana na aina moja wapo ya dawa. Ni vizuri mbuzi wakapatiwa dawa ya minyoo walau mara moja kwa mwaka inayotibu homa ya mbuzi na kukosa hamu ya kula, na angalau mara moja kwa mwaka dawa inayotibu minyoo ya mapafu. Mara chache mfugaji hukosea kwa kuona kamasi kwa mbuzi ni kwa sababu ya baridi kumbe husababishwa na nzi ambao hutaga mayai yake kwenye pua za mbuzi na kusababisha homa.

Maziwa ya mbuzi kwa afya

Ni wazi kuwa wafugaji zaidi na zaidi kila uchwao wanatafuta mbuzi wa maziwa, kama ambavyo wamekuwa wanyama wanaopendelewa zaidi kwa uzalishaji wa maziwa. Maziwa ya mbuzi ni rahisi kumeng’enywa tumboni na yanaweza kustahimiliwa na watu ambao wasingeweza kustahimili maziwa ya aina nyingine. Hayana mafuta mengi na yanafaa zaidi kwa watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa pumu pamoja na matatizo ya ngozi.

Mbuzi wanahitaji malazi mazuri na nafasi ya kutosha

Ni muhimu kutowalaza mbuzi wako sakafuni. Sakafu ya banda lako ni muhimu ikawa imenyanyuka juu na iwe na nafasi ya kuruhusu kinyesi cha mbuzi kudondoka chini. Nafasi hizo ni lazima ziwe ndogo sana ili kuepuka miguu ya mbuzi kutumbukia. Hii ni muhimu kwa kuwa miguu ya mbuzi ni rahisi kukwama na inaweza kusababisha mbuzi kuumia vibaya. Sababu ya kuweka sakafu ya banda la mbuzi kuwa juu ni ili kuzuia mbuzi asilale mahali palipolowana, hii inaepusha mbuzi kukohoa na kutia maziwa doa.

Mbuzi hawapendi mvua

Banda la mbuzi ni lazima liwe na hewa ya kutosha, lakini liwe limefunikwa vizuri ili kuzuia upepo kwa kuwa mbuzi wanaweza kupata kikohozi ama ubaridi kama hawatawekwa kwenye banda lisilofaa. Muhimu zaidi, mbuzi wa maziwa hatakiwi kuachwa apate unyevu, au kulowana (hii ina maana kuwa wasiachwe kwenye mvua). Unaweza kuona kuwa mara tu mvua inapoanza kunyesha, wote wanajaribu kukimbilia kwenye zizi. Ni muhimu sakafu ya banda kutandikwa nyasi kavu. Mbuzi watakula karibu nyasi zote wakati wa usiku, lakini ni muhimu kwao.

You can share this post!

AKILIMALI: Kijana hodari wa uchoraji aliyejigundua kwenye...

AKILIMALI: Kilimo kidijitali ndio suluhu ya uhaba wa...