AKILIMALI: Ni faida kuongeza viungo thamani

AKILIMALI: Ni faida kuongeza viungo thamani

Na PETER CHANGTOEK

ALIKAMILISHA masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta mwaka 2020, ambapo alisomea shahada ya Soshiolojia na Saikolojia.

Hata hivyo, Stephanie Njeri, 24, ameanzisha kampuni ambayo huwasaidia wakulima wanaoikuza mimea ya viungo, kwa kuyanunua mazao yao na kuongeza thamani, kwa kuzitengeneza bidhaa malimbali.

Kampuni yake inajulikana kwa jina Ukoo Farm Products, na huyanunua mazao yaliyozalishwa pasi na kuzitumia kemikali zozote, maathalan; pilipili, tangawizi, iliki, mdalasini, karafuu, n.k, na kuongezea thamani kwa kuyasaga mazao yenyewe, na kupakia kwa sacheti na mikebe na kuwauzia wateja mbalimbali.

“Awali, nilikuwa nikinuia kujihusisha na ukulima, lakini nikabadili mawazo nilipogundua kuwa, kuna mazao ya ziada yanayozalishwa na wakulima, na tatizo haliko kwa uzalishaji, bali lipo kwa miundomsingi, uuzaji na uongezaji wa thamani, kwa kutaja tu machache,” aeleza.

Hivyo basi, akaamua kujitosa katika shughuli ya kuongeza thamani kwa mazao ya viungo, kwa sababu wakulima wadogowadogo huwa hawana ujuzi wa kuongeza thamani kwa viungo hivyo.

Huku akiwa na mtaji wa takribani Sh50,000, na wazo hilo pevu, Njeri akajitosa katika shughuli hiyo jijini Nairobi, mwaka 2020, na biashara yake inaendelea kunawiri.

Alipokuwa akifanya utafiti kuhusu mradi huo, aliwashirikisha wakulima wadogowadogo, hususan wanawake, kutoka katika maeneo ya mashambani.

Kwa wakati huu, yeye hushughulika na usagaji na upakiaji wa mazao ya viungo pekee. Hata hivyo, anafichua kwamba, wana mashine ya kutengeneza mafuta ya nazi, na mwishoni mwa mwezi huu wa Januari, mafuta hayo yatakuwa yakiuzwa masokoni.

Njeri huyanunua mazao hayo kutoka kwa wakulima walioko katika maeneo ya Nakuru, Nyeri, Meru, Mombasa, miongoni mwa maeneo mengineyo. Hata hivyo, hushurutika kuvinunua viungo vinginevyo kwa wauzaji wa jumla, hasa wakati ambapo viungo vyenyewe havipatikani kwa urahisi kwa wakulima.

Anafichua kuwa, ili kuwafaidi wakulima wadogowadogo, huwanunulia mazao yao kwa bei zilizo juu kwa asilimia kumi, ikilinganishwa na bei zilizoko sokoni.

“Sisi hununua tangawizi kilo 50 kwa kati ya Sh6,000 na Sh6,500, ikitegemea misimu. Hununua soya kwa Sh700-Sh900, pilipili manga kwa Sh8,000-Sh8,500, iliki kwa Sh6,700, karafuu kwa Sh6,200, mdalasini kwa Sh5,800 na jira kwa Sh6,400,” afichua.

“Kwa wakati huu, tumepanda mimea ya dania ambayo tutatumia kwa uzalishaji wa poda ya dania. Muda unavyozidi kusonga, tunaweza kushughulika na mazao mengine, lakini kwa sasa, tunashikilia uongezaji wa thamani kwa mazao yanayozalishwa na wakulima wadogowadogo,” asema Njeri.

Kwa wakati huu, yeye hupeleka mazao hayo kusagwa katika kampuni nyingine.

“Hata hivyo, tuna mashine ya kutengeneza mafuta ya nazi, na tutaanza kutengeneza mafuta hayo mwishoni mwa mwezi huu,” aongeza.

Anasema kuwa, mazao wanayoyanunua huzalishwa na wakulima hao pasi na kutumia kemikali. Aidha, anaongeza kuwa wakulima hao hutumia mbolea asilia na viuadudu asilia.

Isitoshe, anadokeza kuwa, usafi hudumishwa na wakulima shambani, na huyanunua mazao yaliyo bora kutoka kwao.

Bei za bidhaa

Njeri huuza soya gramu 80 kwa Sh120, gramu 200 kwa Sh300. Pia, huuza gramu 80 za tangawizi kwa Sh150, na gramu 200 kwa Sh350. Vilevile, wao huuza pilipili manga zilizosagwa gramu 80 kwa Sh180 na gramu 200 kwa Sh400. Aidha, huuza gramu 80 za pilau masala kwa Sh180 na gramu 200 kwa Sh370.

Kwa wakati huu, ana wafanyakazi watatu na hutangaza biashara yake kupitia kwa mitandao ya kijamii k.v. Twitter na Instagram. Aidha, huziuza bidhaa zao kupitia kwa Jiji, Mkulima Young, Pigiame na Jumia.

Kwa sasa, wao huziuza bidhaa zao katika Kaunti ya Nairobi tu, lakini iwapo wateja watamudu gharamu ya kusafirishiwa bidhaa hizo katika maeneo mengine ya nchi, wako tayari kuwauzia.

Kuna changamoto kadha wa kadha ambazo amewahi kuzipitia katika biashara hiyo, kama vile ukosefu wa fedha za kutosha za kuimarisha shughuli hiyo.

Pia, kuna changamoto ya ubaguzi wa umri, ambapo baadhi ya watu humwona akiwa mdogo sana, kiasi cha kutompa muda wa kuzungumzia masuala ya biashara.

Njeri ananwasihi wale ambao wana nia ya kujitosa katika biashara kama hiyo, kuhakikisha kwamba wanatengeneza bidhaa zilizo bora, ili wawe na wateja kwa wingi. Pia, anasema kuwa kuna changamoto, lakini hakuna jambo jema linalopatikana kwa urahisi.

Katika siku za usoni, anapania kuziuza bidhaa zake nje ya nchi.

You can share this post!

AKILIMALI: Mwanachuo anayelipa karo kwa kufinyanga vyungu...

AKILIMALI: Lishe bora ya mifugo msimu wa kiangazi