AKILIMALI: Ni mashine ya kisasa ya kuchuma chai, lakini kuna hofu ‘itameza ajira’

AKILIMALI: Ni mashine ya kisasa ya kuchuma chai, lakini kuna hofu ‘itameza ajira’

Na WANDERI KAMAU

KWA muda mrefu, uchumaji wa majanichai nchini umekuwa ukiendeshwa kwa njia ya mikono, hasa miongoni mwa wakulima wadogo wadogo.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, wamiliki wa mashamba makubwa ya zao hilo wameanza kukumbatia matumizi ya mashine za kisasa ili kuboresha na kuharakisha uchumaji wake.

Hayo yamefikiwa kufuatia uvumbuzi wa mashine ya kisasa iitwayo ‘Mchai’, ambayo imeleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya majanichai nchini.

Kwa mujibu wa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mchai Kenya, Mhandisi Ben Lan, mashine hiyo imeanza kuboresha uchumaji majanichai, licha ya kuwa katika hatua za mwanzo kwenye matumizi yake nchini.

Mashine hiyo ina uzani wa kilo 1.7

“Huu ni muundo mpya. Tuliitengeneza kwa muundo huo kwa sababu tulibaini wakulima walikuwa wakitumia fedha nyingi sana kununulia pembejeo za kilimo na kuwalipa wafanyakazi wanaowachumia majanichai yao. Kwa mfano, wakulima katika eneo la Kati huwalipa wafanyakazi Sh13 kiwastani wa kila kilo moja ya majanchai wanayowachumia. Wafanyakazi katika maeneo mengine nchini huwatoza wakulima Sh8 kwa kila kilo moja wanayowachumia. Kwa kuwa tayari kuna mashine kubwa kama hii, tuliona ikiwa heri kutengeneza nyingine ndogo itakayowasaidia kupunguza gharama wanazotumia kuwalipa vibarua kuwachumia zao hilo,” akasema kwenye mahojiano na Akilimali.

Kwenye shughuli ya kuwaonyesha wakulima matumizi ya mashine hiyo katika mashamba kadhaa ya majanichai katika Kaunti ya Nandi, Lan alisema wakulima wengi wanamiliki mashamba madogo, hivyo ni vigumu kwao kumudu kununua mashine kubwa.

“Ni mashine yenye uzani wa kilo 1.7 na inayotumia betri. Huwa inabebwa kwa mgongo. Betri yake inaweza kuweka moto kwa kati ya saa sita hadi saa nane, ijapokuwa muda huo hulingana na aina ya kazi anayofanya anayeitumia,” akaongeza.

Alisema kuwa mashine haiwezi kuingiza maji, ni rahisi kubebwa na anayechuma majanichai na ina nafasi kubwa ya kukusanyia majanichai yanayochumwa.

“Ni muhimu kubaini kwamba mashine hii huwa haina kelele wakati inapotumiwa. Betri yake huwa inawekwa moto kwa stima inapoisha,” akasema.

Alieleza ubora wa majanichai inayochuma huwa sawa na yale yanayochumwa kwa njia ya mikono.

Mashine sio ghali

Kulingana naye, mashine hiyo si ghali kama ambavyo wakulima wengi wamekuwa wakihofia.

Mashine hiyo, ambayo matumizi yake tayari yameidhinishwa na Halmashauri ya Kusimamia Majanichai Kenya (KTDA) huwa inauzwa kwa Sh28,000.

Hata hivyo, bei hiyo imekuwa ikiongezeka na kufikia Sh32,000 kutokana na gharama za kodi.

Alisema walifikia bei hiyo baada ya kubuni makubaliano na halmashauri.

Alisema inawasaidia sana wanaoitumia kuongeza kiwango cha majanichai wanachochuma kwa muda mfupi sana, ikilinganishwa na matumizi ya mikono.

“Kwa mfano, ikiwa wafanyakazi wako hukusaidia kuchuma kilo 1,000 kwa mwezi, mkulima anaweza kuokoa hadi Sh8,000. Vile vile, anaweza kujipatia mapato kwa kuikodisha kwa wakulima wenzake,” akaeleza.

Bw Paul arap Karan, ambaye amekuwa akikuza majanichai kwa zaidi ya miaka 30, alisema kuna uwezekano mashine hiyo itakumbwa na upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya wakulima lakini watakumbatia matumizi yake.

Naye Bw David Serem, ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kimam, Kaunti ya Nandi, alisema mashine hiyo inaweza kutumika kwa siku kumi mfululizo bila kupata matatizo yoyote.

Kufikia sasa, zaidi ya wakulima 1,200 wameanza kuitumia kote nchini. Bw Lan alisema wanaweka mikakati kuwafikia wakulima wengi zaidi katika sehemu tofauti nchini.

You can share this post!

Shirika lataka IEBC izuiwe kukagua saini

BIASHARA MASHINANI: Lishe mbovu nusura ifagie sungura wake;...