Makala

AKILIMALI: Saladi isiyolikuzwa na wengi ingawa ina soko tamu

December 20th, 2018 3 min read

Na GRACE KARANJA

Katika jamii nyingi za humu nchini Kenya akina mama wana ujuzi wa miaka mingi kuhusu aina mbalimbali ya mimea, ambayo inaweza kukuzwa na kuuzwa katika masoko maalum.

Hili linathibitishwa na Bi Carol Wanjiru ambaye amejitosa katika kilimo cha mboga na kuwa kielelezo bora kwa jamii na hususan akina mama kwa jumla, kwamba wanaweza kujitegemea wenyewe hata bila ya kuajiriwa.

Kilimo cha saladi ni mojawapo ya kilimo cha mboga aina ya kabeji ambacho wengi hawakijui na hawakithamini. Kulingana na Bi Wanjiru, Wakenya wengi bado hawana ufahamu kuhusu mboga hii ya saladi ikiwa ni tofauti na mataifa yaliyo endelea, ambayo wao hutumia muda mwingi kufikiri namna ya kutunza afya zao.

“Hapa kwetu tunapenda kula tu mchicha, managu, sukumaki na spinachi tulizozoea bila kusahau kabeji. Wenyeji katika mataifa yaliyoendelea wanatilia maanani sana chakula wanachokila hasa wao hupenda sana mboga na matunda. Saladi haijulikani sana na wenyeji lakini tunauza sana katika hoteli za kifahari,” anasema.

Yeye alisoma na kuhitimu kama afisa wa mauzo katika Chuo Kikuu cha Nazarene na baadaye aliajiriwa na kampuni moja ya kibinafsi mjini Nairobi. ?Ni wakati huo alipoanza kilimo cha mboga hii ya saladi na kugundua kwamba ilimpa kipato cha haraka na kingi kuzidi mshahara wake.

Aliamua kuacha kazi ofisini na kuanza rasmi kilimo cha mboga hii almarufu lettuce. ?”Mimi nilibadilisha mawazo na kuanza kujiajiri mwenyewe ambapo miaka hiyo minne sijajuta,” anasema Caroline kutoka eneo la Olooloitikoshi, Kaunti ya Kajiado.

Anasema kwamba mboga hii ya saladi hufanya vizuri sana hata maeneo ambayo hayapokei mvua kila wakati. Ikiwa mkulima ana maji ya kutosha hakuna sababu ya kutojishughulisha na biashara hii. ?Hata hivyo, anasema kuwa kuna aina tofauti za mmea wa saladi kama vile ile nyekundu, ile ambayo huwa na kichwa sawia na kabeji na pia ile iliyo na kichwa lakini majani yake yameachana akidokeza kwamba zote hukua kulingana na hali ya hewa katika eneo husika.

“Hii iliyo kama kabeji hupendwa sana hapa nchini hasa katika hoteli zinazotopokea watalii hivyo soko letu liko sawa.

Pia katika hoteli za mijini mboga hii huwa ni bora zaidi katika utayarishaji wa saladi ingawaje wenyeji wengi hasa katika mitaa iliyo na wakaazi wengi, na pia mashinani hawajakumbatia matumizi yake,” anaeleza Bi Wanjiru.

Kama anavyoeleza, kilimo cha saladi ni rahisi sana na hakihitaji muda mwingi bora tu mkulima ana maji ya kutosha. Anashauri mkulima kuandaa mbegu kwenye kitalu kabla ya kuotesha shambani. Mimea hii itakuwa tayari baada ya mwezi mmoja akionya wakulima kutozidisha umri wa mimea kwenye kitalu.

Hata hivyo, anasema kuwa mbolea ya mifugo inafaa zaidi kwa mboga hizi ikizingatiwa kuwa zinakomaa kwa muda mfupi. Hata hivyo anaomba wakulima kufuata ushauri wa kutumia madawa ya kemikali ili kuzuia maradhi.

“Ikiwa mkulima atatumia madawa kutoka viwandani afuate maagizo kutoka kwa watalamu wa mimea ili kuepuka magonjwa yanayoweza kutokana na madawa hayo kwa sababu mboga hizi hukomaa kwa muda wa mwezi mmoja,” anaeleza.

Anasisitiza kwamba kupalilia mimea kila mara magugu yanapotokea huzuia mmea maalum kudhoofika hivyo kukua vyema na hatimaye kuboresha soko. ?Anasema kwamba zao hili la saladi huwa tayari baada ya mwezi mmoja kutoka wakati wa kuoteshwa shambani.

“Naupenda sana mmea huu kwa sababu baada ya mwezi mmoja huwa tayari na hili nalifahamu punde tu kichwa chake kinapojaza vizuri katikati tunda lake. Mimi huuza saladi moja kati ya Sh20 hadi Sh30 kwa kila kichwa kulingana na soko,” anasema.

Changamoto za mkulima hazikosekani lakini anasema ukimpa mtaalam nafasi yake katika shamba lako itakuwa rahisi kupambana na magonjwa au wadudu wanaoshambulia mimea.

?Ushauri wa Julius Nduati, mtaalamu wa kilimo cha mimea:

* Jua hali ya udongo wa shamba lako ili kuutibu kama utakuwa na upungufu wa madini au rutuba.

* Njia ya kunyunyizia maji kwa matone ndio mwafaka kabisa. Mbinu zingine zisizo za drips zaweza kuchafua mboga kwa kutupia mmea matope hivyo kuuwekea kikwazo sokoni.

* Ikiwa mkulima amewekeza katika vifaa vya maji atatumia Sh5, 000 za kulipia bili ya stima ya kupiga maji kutoka kwa bomba.

* Mkulima atahitaji mimea 20 hadi 30 elfu katika ekari moja.

* Madawa ya kunyunyizia dhidi ya wadudu na magonjwa yatamgharimu mkulima Sh7, 000 bila kusahau mbolea na upimaji wa mchanga ambazo zitakugharimu Sh10,000.

* Katika ekari moja iliyotunzwa vizuri mimea 20,000 ikiuzwa kwa Sh20 ambayo ni bei ya chini mkulima anaweza kupata Sh400, 000. Anawashauri wakulima kuwa na uzoefu wa kubandilisha mazao ili kuepuka magonjwa.