Makala

AKILIMALI: Sh300,000 kila msimu kutokana na mauzo ya mapapai ya kisasa

October 29th, 2020 2 min read

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

ZAO la mbaazi ndilo hukuzwa na wakulima wengi viungani mwa mji wa Mavindini katika kaunti ya Makueni. Hii ni kwa sababu mmea huu hukomaa kwa haraka katika eneo hili ambalo hushuhudia mvua chache kwa mwaka.

Lakini shamba la Mzee Jonathan Muoki ndilo linaonekana lenye upekee wa aina yake kwani kumepandwa miti mingi ya mapapai. Ni mapapai ya kisasa (Hybrid pawpaw) ambayo ni mafupi ikilinganisha na aina ya zamani na mti mmoja huweza kuza papai 20 kwa msimu mmoja.

Huo sio mradi wake ila ni wa mwanawe wa kiume kwa jina Dennis Nguma mwenye umri wa miaka 27.

Akilimali ilipotembelea shamba hilo la ukubwa wa robo ekari majuzi Nguma ambaye anasomea shahada ya uzamili Kilimo-Uchumi (Agricultural Economics) kijana huyo alisema alianza mradi huo mnamo Januari mwaka huu kabla ya mlipuko wa corona kugunduliwa nchini

“Nilikuwa nimepanda tikitimaji katika shamba hili lakini mapema mwaka huu niliamua kujaribu mapapai ya kisasa baada ya kupata ushauri kutoka kwa rafiki wangu mmoja,” akasema tulipompata akikata matawi yasiyohitajika kwenye miti hiyo.

Nguma amepanda jumla ya miti 120 ya mapapai katika shamba hilo. Hutumia maji kutoka kisima kilichoko karibu kunyunyizia mimea hiyo kwa mifereji ya plastiki ambayo hulowesha maji katika shina la kila mmea.

“Sasa imenipambazukia kuwa kile kilichoanza kama majaribio tu kimegeuka kuwa mradi unaoleta matumaini ya faida kubwa wakati huu ambapo janga la corona limevuruga maisha ya wanafunzi wenzangu baada ya masomo ya ana kwa ana kusitisha,” anasema.

Miaka mitatu iliyopita Nguma alishawishi babake kuchimba kisima pembeni mwa shamba lake, serikali ya kaunti ya Makueni ikilipia sehemu ya gharama ya mradi huo. Ni kutoka kwa kisima hiki ambapo msomi huyu kupiga maji kutumia pampu inayoendeshwa kwa kawi ya jua na kupitisha maji, kwa mifereji ya plastiki, ya kunyunyizia miti ya mipapai.

“Kazi ya kununua na kuunganisha mifereji shambani ilinigharimu Sh10,000,” akasema.

Kwa kutumia pesa zake alizoweka kama akiba, Nguma alinunua mbege aina ya Malkia F1 na kuandaa miche kwenye kitalu. Baada ya miche kuwa tayari aliipanda katika mashimo yenye umbali wa mita mbili kutoka shimo moja hadi nyingine.

Mipapai hunyunyiziwa maji moja kila wiki. Huanza kutoa maua baada ya kufikia urefu wa futi mbili ambayo ni baada ya miezi mitano tangu kupandwa. Mipapai ya kisasa huzaa matunda kwa usawa, kisiasa kwamba ni vigumu kubaini mti wa “kike” au ule wa “kiume”.

Faida nyingine ya aina hii ya mpapai ni kwamba unakomaa haraka kuliko ile ya zamani. Mkulima huanza kuvuna miezi minane au tisa baada ya kupanda miche yake; tofauti na mpapai wa zamani ambao hukumaa baada ya mwaka mmoja, kwa wastani, katika mazingira bora.

“Hybrid pawpaw” huzaa matunda mara tatu kwa mwaka, yakitunzwa vizuri na kunyunyiziwa maji angalau mara moja baada ya kila wiki.

“Kila mpapai unaweza kukuzalia matunda 20 kila msimu wa mavuno. Nakadiria kutia kibindoni karibu Sh300,000 kutoka kwa shamba hili katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Hii ni kwa papai moja huuzwa kwa angalau Sh50, kilingana na ukubwa, katika masomo ya Mavindini, Kathonweni na Wote ambako wateja wanapatikana kwa wingi,” akasema Bw Nguma.

Wadudu ambao wakulima wanafaa kupambana naoi li kupata mavuno bora ni kama vile “mealy bugs” na red spider mites”. Na ugonjwa ambao huathiri mipapai zaidi inajulikana kama “ringspot virus na “Anthracnose” ambayo huathiri matunda yanapoelekea kuwa mbivu.

Wataalamu wanapendekeza kwamba wakulima watumie dawa na mitego maalum (baits) ili kupambana na kudhibiti wadudu hawa waharibifu. Nguma hutumia dawa mbalimbali kupambana na wadudu waharibifu pamoja na magonjwa.

Licha ya kukumbatia kilimo biashara, Nguma anadhamiria kukamilima masomo yake na baada ajisajili kwa shahada ya uzamifu (PHD) katika kozi hiyo hiyo ya Kilimo-Uchumi.