Makala

AKILIMALI: Si mzaha, avokado za Hass 'dhahabu' soko la kimataifa

October 17th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

MKULIMA anapoanzisha mradi wowote ni sharti azingatie mambo yafuatayo: aina ya udongo, tabianchi, upatikanaji wa maji, rutuba miongoni mwa mambo mengineyo.

Hali ni kama hiyo katika mwonekano wa shamba la kukuza parachichi aina ya Hass, ambazo kufikia sasa zimechukua zaidi ya asilimia 80 ya soko la avokado zinazokuzwa humu nchini kwa ajili ya kuuzwa Ulaya.

Kiwango kinachozalishwa humu nchini hakiwezi kutosheleza mahitaji ya soko, kwa sababu ni wakulima wachache tu wanaovumisha upandaji wa avokado za Hass kutoka mashinani, wakisaidiwa na taasisi za utafiti kupata soko la uhakika.

Mmoja wao ni kijana Lamech Kabuti kutoka eneo la Kamunyaka, Kaunti ya Murang’a kilomita mbili hivi kutoka Kenol aliyevalia njuga ukuzaji parachichi kama njia ya kujikimu kimaisha.

Anasema tangu ahitimu kutoka Chuo Kikuu Cha Egerton aliona ni afadhali ajiajiri, baada ya kuzunguka katika ofisi za umma akitafuta nafasi ya kazi.

Kabuti amekodisha shamba ambapo anakuza miche takriban 50,000 ya hass katika kipande cha ardhi mita 8 kwa 24 mraba na zote hutumika katika kilimobiashara.

Kazi yake kuu ikiwa ni kuwasambazia wakulima miche ya Hass kutoka mkoa wa kati, Bonde la Ufa na Pwani huku akiwapatia ujuzi wa bure namna ya kuendesha upanzi huu usiofanywa na wengi.

Pamoja naye amewaajiri vijana watano wanaomsaidia kuangalia mimea, kuanzia hatua ya kupanda hadi wanapovuna, kwa misimu mitatu kila mwaka.

Kulingana na Kabuti anasema kuwa miti ya parachichi inafaa kuwa karibukaribu, ili iweze kupokea miale ya jua kwa pamoja, na wakati mwingi sehemu ya kupanda parachichi iwe safi bila magugu.

Aidha, wakati wa kupanda mkulima ahakikishe shamba lake lina maji ya kutosha, vilevile mkulima akumbuke kupalilia mimea yake angalau mara moja kila wiki ili kuwezesha ukuaji wa kasi.

“Miche ya Hass inahitaji maji mengi kuliko parachichi za kawaida ili kukoleza madini vizuri na kutengeneza mafuta ambayo ni kiungo maalum katika zao la avokado,” alisema.

Kabuti anahimiza wakulima kuwekea avokado mbolea pindi zinapohitimu miezi 6-8, na hili hufanyika kila mara hususan baina ya Februari na April ambapo huwa ni msimu wa kuchipuka.

“Miche inapoanza kutoa maua ni wakati mwafaka wa kuzuia maradhi na viwavi wanaopenda kutafuna matawi ambayo bado ni machanga,” akasema.

Matawi ambayo hayana matumizi yanaweza kukatwa na kuondolewa kwenye mmea, ili kutoa nafasi nzuri kwa parachichi kukomaa haraka.

Parachichi 80

Anasema kuwa kwa kila mti wa parachichi anaweza kuvuna parachichi 80, kutoka kwenye mti mmoja ambapo shamba lake dogo linabeba takriban miti 50.

Kwa msimu mmoja anaweza kupata baina ya parachichi 3500-4000 ambapo bei ya tunda moja sokoni sio chini ya 20, na bei ikiwa nzuri wanunuzi huchukua kwa 50.

Ekari nzima ya shamba inaweza kubeba zaidi ya miti 700 ambapo mkulima akijizatiti, anaweza kujivunia mamilioni kutokana na mradi huu pekee akiondoa hela za matumizi yote.

Kuafikia mahitaji ya soko

Akizungumza na Akilimali mtaalam wa zao la parachichi, kutoka Kakuzi Gathee Kelvin alisema kabla ya kuweka mbolea katika parachichi, ni wazo bora mkulima kufahamu aina ya udongo wake.

Baada ya kupanda miche mkulima ahakikishe anawekea mimea yake rutuba kuanzia sehemu ya mizizi kwenda juu bila kufikia matawi.

Gathee anasema kuwa mpandaji ahakikishe anaweka kiwango sahihi cha dawa ya kupulizia, bila kuzidisha katika baadhi ya sehemu na kupunguza kwingineko.

Aliongezea kuwa madini aina ya Phosphorus ni muhimu katika ukuaji wa mizizi ya parachichi, aidha hupatia mizizi nguvu ya kuchukua maji kutoka mchangani na kuyasafirisha hadi kwenye matawi.

“Mbali na hayo Phosphorus husaidia mimea kupata chembechembe ya virutubishi kama vile chakula na kuipatia nguvu ya kusimama imara isiyumbishwe na upepo,” aliongezea.

Kulingana na Lamech Kabuti, zao la Hass huuzwa kwa wafanyabiashara katikaka soko la Kenol, Kaunti ya Murang’a, ambao hatimaye huchukua jukumu la kutafuta masoko ya mijini mara nyingi wakilenga Nairobi, Mombasa na Meru.

Pia wakulima wadogo kama Lamech wamekuwa wakisambaza parachichi katika viwanda vya kutengeneza juisi ya parachichi, jambo linalofanya bidhaa yenyewe kuwa adimu sokoni.

Aidha makampuni ya kutoa mafunzo kuhusu zao la parachichi nchini mojawapo ikiwa ni Kakuzi yenye tawi kuu mjini Thika, yamekuwa yakiingilia kati na kuwasaidia wakulima kupenya katika soko la kimataifa.

“Ili kuhakikisha kuwa wakulima hawapunjwi na madalali wanaonunua Hass kwa bei nafuu na kuuza kwa bei ghali,” Gathee akasema.

Hili linajiri baada ya Kenya kuingia katika mkataba wa kuuza parachichi katika soko la nje hususan barani Asia ambapo walaji wa zao hili ni wengi.

Wakati wa kuvuna mkulima anaweza kuvalia glavu na aendeshe shughuli yake kwa utaratibu, wakati ambapo hakuna mvua hii ni kwa sababu haya ni matunda ambayo yanaweza kuharibika kwa urahisi.

Kampuni ya Kakuzi yenyewe imekuwa ikiwasaidia wakulima kupenya hadi katika soko la kimataifa kama vile Uchina na Uingereza.

Gathee anaeleza kuwa wakulima kadhaa wanaweza kushikana na kuanzisha mradi kama huu ili kujiongezea kipato hasa faida pale wanaposafirisha bidhaa zao katika soko la nje.

 

[email protected]