Makala

AKILIMALI: Siri ya kufanikisha kilimo cha michungwa ya kupandikiza

April 18th, 2019 4 min read

Na GRACE KARANJA

TANGU vuta nikuvute kuhusu bei ya chini ya mauzo ya kahawa na majani chai ishike kasi katika Kaunti ya Murang’a, wakulima sasa wanaonekana kuchukua mkondo mpya na kuachana na kilimo hicho kilichokuwa kimepata umaarufu mkubwa miongoni mwa wakazi katika miaka ya hapo awali.

Wakulima wameamua kutovunjwa moyo tena madali wanaendelea kujifaidi. Hata hivyo, wakulima sasa wamejihusisha na kilimo cha mazao kama vile mboga na matunda kama vile parachichi, machungwa; huku walio na vyanzo vya maji wakionekana kukuza viazi vikuu kwa wingi pamoja na ndizi.

Hata hivyo, takriban nusu ya Kaunti ya Murang’a hasa maeneo ya Gatanga ya chini, ni kame huku visima vya maji na mito ikiendelea kukauka.

Wakulima kutoka maeneo haya wanaendelea kushauriwa kupanda mimea ambayo inaweza kustahimili hali ya hewa iliyoko kama vile mtama, mbaazi, mihogo na maharagwe. Vilevile, kuna miti ya matunda ambayo pia inaweza kukuzwa katita sehemu ambazo hazipokei mvua nyingi .

Leo, jarida la ‘Akilimali’ linamwangazia Bw Peter Manyeki ambaye kwa miaka mingi amekuwa akitegemea kilimo cha machungwa.

Alipohamia maeneo haya ya Rubiru takriban miaka 30 iliyopita kutoka alikoishi maeneo ya Maragwa, anasema kwamba alipata wenyeji wa hapa wakiwa na uzoefu wa kupanda tu mahindi peke yake na baadhi maharagwe na waliopanda miti ya matunda walionekana kukuza mipapai tu.

Anasema kwamba alinunua miche kadhaa ya michungwa na kupanda ambapo haikukauka kama wengi walivyohadithia. Wengi walianza kumuuliza siri ambapo alisema aligundua kuwa kuotesha kabla ya mvua ya msimu kunyesha na kufuatiliza unyunyiziaji maji kwa muda wa misimu sita ya eneo hilo ambayo ni miaka mitatu.

“Majirani wangu hawakuamini kwamba mtu anaweza kupanda michungwa na iweze kukua. Walijua tu kukuza mindimu na mipapai. Wengi walikuja kwangu kuniuliza siri nami sikusita kuwapa ushauri. Ili mti ushike chini na usikauke tena kwa muda wa miaka mitatu, unafaa kunyunyiziwa maji angalau mara tatu kwa juma. Wengi hawakufahamu kwamba miti aina yeyote ya matunda inastahili kuoteshwa mwezi mmoja au miwili kabla ya mvua kunyesha na si mvua unapoanza kunyesha kama wengi walivyofanya,” anaeleza Bw Manyeki kutoka eneo la Rubiru, Kaunti ya Murang’a.

Hata hivyo, anaonya wakulima dhidi ya kupanda miti ya matunda wakati wa msimu wa mvua kubwa (mwezi wa tatu/nne) kwa sababu punde tu inapowacha kunyesha, hufuatiwa na kipindi kirefu cha jua cha miezi sita au zaidi kabla ya mvua ya msimu wa Oktoba na Novemba kuanza.

Anasema kuotesha mwezi wa tisa na kusubiri mvua ya mwezi wa Oktoba kuja hufaidi miti ya matunda sana kwa kuwa baadaye kipindi cha jua ambacho hufuata ni cha miezi miwili na nusu peke yake, na hapa mkulima anaweza kunyunyizia maji miti yake kwa muda mfupi kabla ya kuanza kwa mvua.

Jinsi ya kupanda

Kama anavyoeleza Bw Manyeki, mtu yeyote anayeazimia kupanda michungwa anaweza kwa sababu haihitaji kazi nyingi na iliyoko haichoshi.

Anasema wengi huhofia bei za kununua miche iliyo tayari na kusahau kuna njia nyingine rahisi ya kupata miche kama vile kutoa mbegu kwa ndimu zilizoiva na kukomaa vizuri na uziweke kwenye maji kisha uchague zinazozama kwani zinazoelea juu ya maji hazioti, uzianike zikauke kabisa.

Mbegu hizo zioshwe kwa maji safi ili kutoa utelezi ambao unaweza kufanya mbegu hizo kuchukua muda mrefu kuota au kutoota kabisa.

“Baada ya hapo, tengeneza kitalu vizuri na umwage mbegu hizo kisha uzifukie kwa udongo kiasi. Mwagilia maji kila siku na baada ya wiki mbili hadi tatu, mbegu hizo zitaanza kuota. Zikifikia Semtimeta 3-5, miche hiyo ihamishiwe kwenye pakiti za plastiki zilizo na udongo pamoja na mbolea ya kutosha na iwekwe kwenye kivuli kiasi, ”anaeleza.

Ansema kwamba miche hii ya mindimu ikifikia Sentimeta 30-40, yeye hutafuta michungwa iliyokomaa na ambayo haina magonjwa kutoka shambani lake na kufanya upandikizi.

Kazi hii inahitaji utaalamu wa hali ya juu na iwapo mkulima hana ujuzi wa kufanya hivyo anaweza kutafuta ushauri kutoka kwa maafisa wa kilimo kutoka eneo husika.

Endelea kumwagilia maji mara kwa mara ili kuhakikisha kuna unyevu kila wakati chini ya miche hiyo.

Hapa, kabla ya miche hiyo kuungana ili kuhamishwa, tayarisha shamba kwa kuchimba mashimo, kuweka mbolea na itakuwa vyema zaidi ikiwa mkulima atafanya hivyo kabla ya mvua kunyesha.

Baada ya kati ya siku 14-21 mmea huu huwa tayari umeungana na mara nyingine matawi kuchipua, sasa unaweza kufungua utepe na kuhamisha huku ukimwagilia maji shimo kabla ya kupanda.

Palilia miche angalau mara 2-4 kwa mwaka. Baada ya miaka mitatu miti itakuwa na ukubwa wa kutosha na hata inauwezo wa kutoa maua.

Miti ipaliliwe tu karibu na mmea huku sehemu nyingine ikifyeka ili kupunguza gharama ya wafanyikazi.
Ushauri kitaalamu.

Bw Gabriel Mwaniki ni afisa wa serikali wa kilimo ambapo yeye hutoa huduma za kilimo kwa wakulima kutoka wadi ya Kakuzi.

Anaeleza kwamba michungwa hufanya vizuri sana katika sehemu iliyo na joto kwa sababu sehemu hizo haziathiriwi na wadudu waharibifu ambao pia husababisha magonjwa kwa miti hii.

“Sehemu zinazofahamika kwa jua kali kama vile Machakos, Makueni sehemu zingine za Murang’a, michungwa hukua vizuri kwa sababu ni nadra sana kuambukizana magonjwa,” anasema.

Anasema kuna aina mbili za michungwa Valencia ambayo haina vikonyo.

Uzao wake ni wa wastani na matunda yake hayaivi kwa haraka hivyo hayaozi upesi. Ingine ni Jaffer ambayo huathirika sana na jua kali ambapo matunda yake huanguka kwa sababu matunda yake hukua na huiva haraka. Miti hii ni mikubwa na inazaa sana.

Anashauri kwamba michungwa ipandwe kwenye mchanga mwekundu kwa sababu hustawisha miti kwa haraka . Anasisitiza kwamba miti ipewe nafasi ya kutosha ili hewa iweze kupenyeza ndani ipasavyo na rahisi.

“Mche upandwe kwenye shimo lenye futi 20. Kutoka mti mmoja hadi mwingine iwe mita sita na pia mstari mmoja hadi mwingine iwe mita 6. Mbolea ambayo inafaa zaidi ni ile iliyooza ya mifugo au majani na kwa kufanya hivyo miti hii ikitunzwa vizuri inaweza kuendelea kumpa matunda mkulima hadi muda wa miaka ishirini,” anasema.

Ugonjwa wa mizizi

Dalili za ugonjwa huu ni kwamba maganda huoza juu ya mizizi au katika mti halisi na matawi yake.

Wakati tu mti unapoambukizwa gundi hutoka sehemu iliyovamiwa.

Matawi hubandilika na kuwa ya majano, kisha hufa ngozi yake na mti mwenyewe hatimaye huangamia na kufa usipotibiwa kwa haraka.

Suluhu lifaalo ni kuyatoa maganda yaliyoathirika au kuyachoma kwa moto. Usipande miti kwenye mchanga mzito au wenye maji mingi.

Ugonjwa wa rangi ya kijani

Ugonjwa huu husababisha matawi kuwa na majano. Matunda huwa madogo yaliyobonyeka. Mti waweza kunawiri bali na msimu.

Ugonjwa huu huambukizwa na mdudu aitwaye pyslid. Zuia mdudu huyo kwa kunyunyizia dawa na miti iliyoambukizwa itunzwe kando na inayokua ili isiambukizane.

Wadudu
Kuna mdudu mweusi wa chungwa na nzi wa machungwa. Wadudu hawa hujitokeza katika makundi upande wa chini wa tawi. Hufunikwa na safu ndogo ya nta nyeusi. Nyunyizia madawa ya kuwaangamiza wadudu.