Makala

AKILIMALI: Soko laendelea kukua la mboga zisizokuzwa kwa kutumia kemikali

May 23rd, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

KAUNTI ya Nyandarua hususan eneo la Nyahururu, huwa na mchanga wenye rotuba ya kutosha kwa wakulima wanaokuza mahindi, viazi, karoti, dania na mboga.

Miaka ya hivi karibuni kumeibuka suala la umuhimu wa ulaji mboga za majani, kutokana na wasiwasi wa kulinda afya zetu au harakati za kuwalinda wanyama.

Kufuatia ulaji wa mboga za majani, mtu huwa hakosi kupata vitamin D, ambacho ni kitu muhimu kwa afya ya mifupa.

Akilimali ilifanikiwa kuzuru baadhi ya mashamba, eneo la Nyahururu kupambanua ukuzaji wa mboga kwa kutumia mbolea za asilia, ambapo tulivutiwa na jinsi ukulima mashinani umepiga hatua kubwa.

Hata hivyo, sikufahamu inapopatikana Tumor Hill, hadi nilipochukua nusu saa hivi kufika shambani humo na kutangamana na Bi Jane Muthoni, wakati akitoka shambani kuchuna mboga.

Akiwa mfanyakazi wa Tumor Hill, taasisi ya kisasa inayotumia mbinu za kisasa kuzalisha vyakula vya aina tofauti mboga zikiwa ni miongoni mwa vyakula hivyo katika juhudi za kujitosheleza, kimahitaji.

Aidha anasema mbali na kuwa mfanyakazi amejipatia ujuzi mkubwa katika sekta ya kilimo cha mboga na angependa kuwaelimisha wakulima wengine.

Tumor Hill ni makao ya kufanyia warsha kwa wageni na watalii, washikadau waliona haja ya kukuza mboga zao wenyewe ili kupunguza gharama ya kutegemea soko za nje.

Muthoni anasema hatua yenyewe imewatengenezea jina ndani na nje ya kaunti ya Nyandarua mbali na kutumika kama kituo cha kufanyia utafiti kwa wakulima chipukizi, wanaomiminika hapa kila siku za wiki.

Kusema kweli ukulima ni uti wa mgongo katika taifa hili, ingawa vijana wengi nchini bado hawajapata msukumo wa kujiingiza kikamilifu.

“Kuna njia mbalimbali za kukuza mboga bila kutegemea kemikali za kisasa ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu,” akasema.

Anasema mkulima anaweza kukuza mboga katika bustani ndogo, kando ya nyumba au ndani ya magunia kama hatua ya mwanzo kabla ya kujiingiza rasmi ndani ya kilimo cha mboga ya michicha ama sukumawiki.

Mbegu za aina mbalimbali zinaweza kukusanywa na kupandwa kama miche kabla ya kuhamishwa ndani ya shamba, pindi zinapokomaa.

Kwa sababu eneo la Tumor Hill ni maarufu kwa ufugaji wa mbuzi na ng’ombe mbolea inayotumika shambani ni ile ya asilia.

Ishara tosha kutokana na mboga zilizoshamiri afya, matawi mapana yaliyokolea rangi ya kijani kibichi.

Anawahimiza wakulima kukumbatia mbinu za kisasa, na wakati mwingine zile za asili ili kuhakikisha ukulima unaenda na Karne ya 21.

Mboga kama sukumawiki zinaweza kuchumwa mara kwa mara, hivyo basi kile kinachohitajika ni mkulima kuziangalia na kuzikagua kwa ukaribu kwa kuzimwagilia maji kila wakati.

Matawi ya mboga yanaposhambuliwa na wadudu, maradhi yanaweza kuzuiliwa pale mkulima anapotumia makapi ya pilipili kukabili wadudu.

Wakati mwingine jivu, lakini hali ikiwa mbaya dawa za kupulizia zinaweza kutumika ijapo sio kwa wingi.

Ukulima wa kukuza mboga unategemea uwezo wa mkulima kutibu udongo na kurekebisha pH, kwa kukuza spishi zinazostahili kimaeneo.

Aina tofauti ya mboga hufanya vyema kulingana na nyanda, zipo mboga zinazokua vizuri kwenye nyanja za juu na zile zinazofanya vizuri katika tambarare.

Bi Jane Muthoni,mfanyikazi katika shamba la Tumor Hill eneo la Nyahururu, Kaunti ya Nyandarua, akitoka shambani kuchuna mboga. Picha/ Richard Maosi

Aidha katika eneo la Tumor Hill anasema wanakuza mboga aina ya Bitter herbs, ambazo haziwezi kushambuliwa na wadudu wa aina yoyote kwa sababu ya ladha na harufu kali inayowatorosha.

Anasema hii ni mbinu moja ambayo wakulima wengi hawajui inaweza kuwasaidia kukabiliana na mkurupuko wa maradhi ya mara kwa mara.

Mbolea za asili kama vile samadi na mbolea ya kijani (green manure) husaidia mimea kuwa na uhifadhi mzuri wa maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Pia husaidia kuleta mshikamano mzuri wa udongo na kupunguza hali ya mpasuko katika udongo.

Anaongezea kuwa mbolea za asilia husaidia kuleta mpangilio mzuri wa udongo na kusaidia hewa kupenya vyema baina ya mchanga.

Hii ni kinyume na mbolea za kemikali ambazo ni adui wa wadudu muhimu kwa mimea na mchanga.
Peter Kangara, mtaalamu wa kupulizia mimea dawa, anasema wadudu hatari wanaokula majani ya mboga wanaweza kujificha chini ya matawi ya mboga.

“Ukiona mistari mieupe ama baadhi ya mashina kuoza au kugeuka rangi basi fahamu mboga wameshambuliwa na wadudu ambao ni hatari,” akasema.