Makala

AKILIMALI: Subira yake katika ukuzaji nyasi hatimaye yamtuza

October 11th, 2018 3 min read

NA FAUSTINE NGILA

NI JUMAMOSI ya jua kali na Akilimali imezuru Kaunti ya Laikipia. Tuko katika barabara ya kutoka mjini Nanyuki kuelekea maeneo ya Hifadhi ya Ol Pejeta.

Imetubidi kuiacha barabara ya lami na sasa tumefuata kibarabara kilichojaa vumbi. Kushoto na kulia kuna mashamba mapana ya nyasi katika eneo hili lisilo na watu wengi.

Tunasafiri kilomita kama tatu hivi kisha tunaegesha gari letu kando ya shamba moja ambalo limejaa shughuli nyingi za mavuno.

Trakta linaonekana likikata nyasi huku limefuatwa na vumbi usimwone dereva. Katika pembe moja ya shamba hili la ekari nne, kumeegeshwa trakta lingine lililounganishwa na mashine ya kufunga nyasi.

Tunakutana na Bi Jane Mwangi ambaye ndiye mmiliki wa uwekezaji huu. Licha ya kuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili, mama huyu hajafumbia macho kipato kutokana na ukuzaji wa nyasi ya ng’ombe licha kununua shamba katika eneo kame.

Anatuelezea kuwa ingawa shamba hilo alilinunua mnamo mwaka wa 2010, illikuwa 2016 ambapo aliamua kuanza kulitumia kuvuna hela ila kwa changamoto nyingi.

Yeye ni mkazi wa mjini Karatina lakini amewekeza kwa shamba lililoko Laikipia, na ndio maana mwanzoni hakuelewa vizuri hali ya hewa na tabianchi ya eneo hilo.

“Eneo hili ni kame na wakulima hutegemea msimu wa mvua kukuza mimea. Mimi mwanzoni nilianza kwa kupanda viazi na maharagwe lakini nilijuta sana maanake nilivuna hewa licha ya mimea kuonekana ikinawiri. Mvua ilipotoweka, mimea yote ilikauka,” anasimua mwalimu huyu aliyefundisha kwa miaka 25.

Alipoona majirani wakivuna vizuri kutokana na ukuzaji wa nyasi ya ng’ombe, alijitosa mara moja kwa uwekezaji huo lakini bado akagonga mwamba.

“Nilipanda nyasi aina ya African Oat lakini bado sikufanikiwa kupata mavuno niliyotarajia,” anasema mama huyu wa watoto wanne.

Baada ya kuchoka kutumia mbinu zake mwenyewe kuendesha kilimo kwa shamba lake, aliamua kuomba ushauri wa wakazi ambao ni majirani wake.

Bi Jane Mwangi ashika kifushi cha nyasi aina ya Rhodes katika shamba lake la nyasi eneo la Ol Pejeta, Kaunti ya Laikipia mnamo Oktoba 6, 2018. Picha/ Faustine Ngila

Alinunua mbegu za nyasi aina ya Rhodes kutoka kwa Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB) na kujiandaa kwa msimu wa mvua.

Msimu huu amevuna maborota (nyasi iliyofungwa kwa kilo 15) 413 ya nyasi na anatarajia kuiuza kwa kati ya Sh120 na Sh160 huku akifafanua kuwa bei hiyo hupanda hadi Sh300 wakati nyasi ni nadra.

Ingawa kuna tatizo la soko, Bi Mwangi anakiri kuwa mtazamo wa baadhi ya wawekezaji kuwa maeneo kame hayawezi kumfaa mkulima unapotosha, kwani bei ya ardhi iko chini na nyasi hunawiri sana, hasa Kaunti ya Laikipia.

Gharama za kilimo huingia wakati wa mavuno, ambapo mkulima huhitajika kukodisha au kuwalipa wamiliki wa trekta za kukata nyasi na mashine za kufunga nyasi kwa maborota.

Shughuli nzima ya kufunga borota moja itamgharimu mkulima Sh80, lakini akiliuza kwa Sh300 atapata faida ya Sh220 kwa kila borota.

Mkulima mwingine aliyejitambulisha kama Maina alisema kuwa biashara ya nyasi ina faida zaidi iwapo mkulima atapanua kilimo chake na kupanda nyasi kwa ekari nyingi zaidi.

 

Ufadhili

Wamiliki wa trekta katika eneo hili wanakiri kuwa biashara ya kuvuna na kufungia wakulima nyasi imewafaidi, hasa ikizingatiwa trekta hizo wamezikodi kutoka kwa kampuni ya Quip Bank inayoendesha mradi wa Tinga.

“Sisi hukodisha trekta na mashine za kufunga nyasi kutoka kwa kampuni ya Quip Bank ambayo pia hutoa ufadhili na mafunzo ya kuendesha trakta,” akasema Peter Kariuki ambaye pia ni mkulima.

Meneja wa mradi wa Tinga katika Kaunti ya Laikipia Bw Daniel Koome anasema kuwa bei ya kukodisha mashine za kilimo ni nafuu na husaidia wakulima kupunguza gharama za ukuzaji.

“Tumeunda vikundi 20 vya wakulima, kila kikundi kikiwa na wakulima 45-60 na tunawasaidia kukabiliana na changamoto za kilimo hasa utayarishaji wa mashamba, upanzi na shughuli za mavuno,” anasema.

Anaelezea kuwa kaulimbiu ya kampuni hiyo ni kuhakikisha imesaidia taifa hili kuafikia mojawapo ya Ajenda Nne Kuu ya kumaliza uhaba wa chakula nchini kwa kutumia mashine zinazopunguza gharama ya uzalishaji wa chakula, kuongeza ubora wa chakula na hivyo kushusha bei ya chakula.

Hata hivyo, wakulima katika eneo hili wanaitaka serikali iwaepushie mzigo wa kukosa maarifa kuhusu jinsi ya kukuza aina mbalimbali ya mimea na gharama za baada ya mavuno.

“Tutafurahia iwapo tutapewa mbegu za aina za kisasa za lishe ya ng’ombe ili tuweze kufaidika. Tukijua jinsi ya kupanua kilimo na kupanda kwa mashamba mapna, bila shaka tutakuwa tumepata suluhu ya kupunguza gharama ya uzalishaji,” akasema Bw Kariuki ambaye ni baba wa watoto sita.