Makala

AKILIMALI: Tabitha na mumewe wachangamkia kilimo cha ngano

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA eneo la Karuga, Nyahururu, Kaunti ya Laikipia, tunakutana na mkulima Tabitha Wanjiku ambaye huwa anashirikiana na mumewe katika kilimo cha ngano.

Ngano hukuzwa kwa wingi katika eneo la Laikipia lakini kulingana na Wanjiku, wao wamefa ikiwa kulima mmea huu katika sehemu ya ekari mbili ya shamba lao.

Bi Wanjiku mwenye umri wa miaka 32 anasema kuwa walianza kilimo hiki mnamo 2015 na kwa sasa, huu ni msimu wao wa tano wa kupanda ngano na wana kila sababu ya kutabasamu.

Kulingana naye, ngano huchukua muda wa hadi miezi sita pekee shambani kabla ya kuvunwa. Kwa kawaida, huwa wanaipanda mwezi wa tano kila mwaka na kuvuna baadaye mwezi wa kumi na moja au Disemba. Anaelezea kwamba katika mwezi wa nne, shamba huandaliwa kwa kulimwa ili liwe tayari kwa upanzi mwezi wa tano. Anasema kwamba upanzi wa ngano huwa unafanyika kwa kutumia mashine maalumu ambayo hukokotwa kwa tinga-tinga au trekta.

Mbegu za ngano wanazopanda huwa zinachanganywa na mbolea pamoja na kupandwa kwa mashine hii. Mbolea ya kiasili pia hutumika katika kilimo hiki. Bi Wanjiku anaelezea ya kwamba mbegu hizi huwa wanazinunua katika shirika la wakulima la Kenya tawi la Nyahururu.

Katika kila ekari moja ya shamba mbegu zinazohitajika ni kiasi cha gunia la kilo hamsini na kwa kuwa wao wana shamba la ekari mbili huwa wanahitaji mbegu kiasi cha kilo mia moja.

Upanzi unapofanyika kwa mashine huwa inawachukua muda wa saa moja pekee kupanda ekari mbili. Baada ya wiki moja hivi mmea huchipuka kutoka mchangani. Kwa muda wa miezi mitatu mmea huu huhitaji kupigwa dawa ya kuzuia wadudu hatari, ugonjwa wa kutu pamoja na dawa ya kukausha majani yanayokua shambani bila ya kuhitajika.

Ugonjwa hatari wa kutu huwa unatokea wakati kuna upungufu wa mvua ama wakati mvua ni nyingi kupita kiasi. Bi Wanjiku anaendelea kusema ya

kwamba katika muda huu pia mbolea huongezwa ili kuendelea kuupa mmea huu madini muhimu ili kuboresha afya ya ngano.

Kwa kawaida ekari mbili za shamba la ngano huhitaji kilo mia moja za mbolea. La mno ni kuwa katika mwezi wa Agosti mmea huu huanza kutoa mazao ya ngano na baadaye mwezi wa kumi ngano hii huanza kukauka, na kwa mwezi mmoja tu huwa iko tayari kwa mavuno. Wakati wa kuvuna sawia na kupanda huwa inachukua muda mfupi wa saa moja.

Kila ekari moja kulingana na Bi Wanjiku ina uwezo wa kuvunwa magunia ishirini na mawili na kwa hivyo katika shamba lao kila mwaka huwa wanavuna magunia arobaini na manne. Anasema ya kwamba baada ya kuvuna huwa wanauza ngano hii kwa wafanyabiashara wa kati ambao huwa wanainunua kwa wingi.

Kwa miaka michache iliyopita wamekuwa wakiuza gunia moja kati ya Sh2,600 na Sh3,000. Hata hivyo, anasema kwamba baada ya mavuno, huwa anapanda viazi katika eneo hilo hilo kuanzia mwezi wa disemba hadi machi. Baadhi ya changamoto ambazo Bi. Wanjiku anaelezea ambazo wakulima wa ngano hukumbana nazo ni pamoja na kunyesha kwa mvua wa kati wa mavuno.

“Mvua inaponyesha mwezi wa kumi na moja wakulima kwa mara nyingi huenda hasara kubwa kwani ngano iliyokauka ingali kwa mmea huwa inaanza kukua upya,” anatoa maelezo.

Ngano inapokua pia huandamwa na baadhi ya magonjwa ambayo yasipotibiwa kwa wakati huwa yanaathiri mavuna pakubwa. Zaidi ni kuwa pembejeo zinazohitajika tangu upanzi kufanyika ni za bei ya juu mno kuanzia na mbegu, mbolea na dawa za kupigana na maradhi.

Mwito wake na haswa wa wakulima wengi ni kwamba serikali iweke mikakati thabiti ya kuhakikisha wanapata masoko ya nje ili kuhakikisha wanapata mauzo bora za kwa mazao yao.