Makala

AKILIMALI: Teknolojia mpya ya kukuza viazi inavyowapunguzia wakulima gharama

December 27th, 2018 3 min read

NA FAUSTINE NGILA

HALI ya anga ni shwari katika maeneo ya Timau, Kaunti ya Meru wakati Akilimali inazuru mashamba mapana ya ngano, canola na viazi kung’amua teknolojia zinazotumika kufanikisha kilimo kwenye maelfu ya maekari.

Tunafuata barabara ya kutoka Laikipia kuelekea Meru, na tunapokaribia kituo cha utafiti wa mbegu za viazi cha Kisima, tunaingia upande wa kulia na kupata wakulima wakijiandaa kupanda viazi kwa mashine. Wanatwarifu eneo hili linaitwa Wamugi.

Tunampata Bw Martin Dyer juu ya tingatinga akipakia mbegu za viazi kutoka kwa magunia yaliyopangwa kwa lori ndogo. Huku amevalia kaptula na viatu dhabiti vya shambani, anatukaribisha kwa shamba lake kwa lugha mufti ya Kiswahili.

Anatueleza kuwa kwa miongo mitatu amekuwa akifanya kilimo chake kwa mbinu za kawaida bila kutumia mashine, hasa akitegemea vibarua wakati wa kupanda, kupalilia na kuvuna viazi.

“Nilianza kilimo mwaka 1980 wakati ningali kijana na nimepanda mimea mingi tangu wakati huo lakini ni msimu uliopita ambapo nilianza kukuza viazi,” anasema mkulima huyu mwenye asili ya Uingereza.

Anasema kuwa pia ana shamba lingine la ekari 30 ambapo amepanda viazi kwa kunyunyizia maji, lakini kwa mbinu tofauti ya umiliki wa ardhi.

“Mimi hukodisha mashamba haya kutoka kwa wenyeji hapa kisha tunagawana katikati mapato kutokana na mauzo. Gharama zote za shambani ni zangu lakini sote tunafaidi,” anasema.

Yeye hununua mbegu za viazi katika kituo kilicho karibu cha Kisima, kisha kukodisha trakta ya kipekee inayotumia teknolojia ya kisasa kufanya shughuli tano za shambani kwa mpigo.

“Kwa kuwa shamba hili ni pana mno, nimekodi huduma za trakta la kisasa kutoka kampuni ya vifaa vya shambani ya Tinga, ambalo baada ya kulima shamba, linakata mitaro ya kupanda, linatia kiwango kinachofaa cha fatalaiza, linapanda viazi na kisha kufunika mchanga,” anaeleza mkulima huyu mwenye miaka 56.

Trakta lapanda viazi katika shamba la Bw Martin Dyer, Kaunti ya Meru huku wakazi wakiduwazwa na uwezo wake wa vipimo sahihi. Picha/ Faustine Ngila

Kinachoduwaza wakulima wa eneo hili ni kuwa trakta hilo lina mashine inayoweka vipimo sahihi vya upana wa upanzi wa viazi kwenye laini na katikati ya laini.

Anachotakiwa kufanya mkulima ni kutia fatalaiza ya kilo 200 kwanza kwenye sehemu ya nyuma ya trakta kisha kutia mbegu. Linahitaji vibarua wawili pekee pale nyuma wa kupakia mbegu za viazi.

Bw Dyer anasema kuwa kwa siku moja, yeye hupanda magunia kumi ya mbegu za viazi, kazi ambayo itawachukua vibarua zaidi ya 200 siku tatu kuimaliza.

“Wakati ninatumia vibarua, inanigharimu zaidi na kazi yao si nzuri vile. Wao husahau vipimo vya upanzi, kiwango cha fatalaiza na wanapovuna, wao hudunga na kukata viazi.”

Kulingana na utafiti, utumizi wa mashine humpunguzia mkulima gharama kwa hadi asilimia 50 pamoja na kuhakikisha kiwango cha asidi mchangani kimedhibitiwa na kuulainisha mchanga kuwezesha mizizi ya mimea na maji kupenyeza.

Baadhi ya mbegu za viazi zilizoidhinishwa na serikali katika kituo cha Kisima, Kaunti ya Meru zikiwa kwa trakta tayari kwa upanzi. Picha/ Faustine Ngila

Mhandisi Titus Musyoka aliye pia meneja wa kampuni ya Tinga anasema kuwa ekari moja linahitaji vibarua 30 kwa upanzi na watachukua saa nane huku wakilipwa Sh400 kila mmoja.

“Ukitumia trakta lenye teknolojia hii, ekari moja litahitahi dereva na watu wawili na itawachukua saa tano. Gharama zote ni Sh5,000 ukilinganisha na Sh12,000 kwa vibarua,” anasema.

Anaeleza kuwa wakati wa kuvuna, utumizi wa mashine hiyo humpunguzia mkulima hasara kwa zaidi ya asilimia 30. Vibarua hutumia majembe kuvuna viazi na hujipata wamekata na kuharibu viazi vingi ambavyo vingeuzwa sokoni.

Ni mashine ambayo inaweza kutumiwa kupanda mimea ya aina nyingi, kinachohitajika tu ni vipimo vya upana wa mimea kuwekwa mwanzo kabla ya kuanza kupanda.

Msimu huu Bw Dyer anatarajia kuvuna magunia 200 kwa kila ekari, na kuuza kwa kati ya Sh2,500 na Sh5,000 kulingana na uhaba wa viazi sokoni.

Kupitia ushirikiano na Bayer East Africa, Siraji Sacco, Yara, Sereni Fries na Muungano wa Kitaifa wa Wakulima, kampuni ya Tinga imekuwa ikiwapunguzia wakulima gharama za uwekezaji.

Yara hutoa huduma za kupima kiwango cha asidi kwa bei nafuu, Bayer East Africa inawapa dawa za kuua wadudu na kuzuia magonjwa, Siraji Sacco inatoa ufadhili wa kifedha huku nayo Sereni Fries ikiwa mteja mkuu wa viazi nayo Tinga inawakodisha trakta na mashine.

Mkulima wa eneo la Timau, Meru, Bi Fridah Wachira aonyesha mimea yake ya viazi. Alitumia mashine za kisasa kutayarisha shamba lake. Picha/ Faustine Ngila

“Ushirikiano huu umetufaa sisi wakulima kwa kuwa sasa sihitaji kununua trakta la thamani ya mamilioni. Nahitaji tu hela kidogo za kukodisha mashine hizi,” anasema Fridah Wachira, ambaye ni mkulima wa viazi kilomita kumi kutoka hapa.

“Mashine za kuchimba za Tinga zimenifaa sana kuchimba ardhi ngumu iliyokuwa inazuia mizizi ya viazi kupenyeza mchangani. Kwa wakati mmoja nililazimika kusitisha kilimo change kwa kuwa gharama ilikuwa juu na mvuno yalikuwa duni kutokana na kutumia fahali kupalilia,” akasimulia.

Alisema kuwa awali ekari moja lilikuwa linampa magunia 30 pekee ya viazi lakini baada ya kuanza kutumia teknolojia hiyo, sasa amekuwa akivuna magunia 130 kwenye shamba lake la ekari moja.

Tatizo la wakulima wengi ni kutumia viazi walivyovuna kama mbegu, lakini kupitia mafunzo ya ushirikiano huo, sasa wameelewa kuwa mbegu zilizotibiwa dhidi ya magonjwa na wadudu zinawaletea mavuno ya kufana.

“Wengi hakuwa wanajua kuwa kimo cha mbegu za viazi kinafaa kuwa kati ya sentimita 2 na 3, walikuwa wanapanda viazi vikubwa kama vya sokoni,” anasema Bw Musyoka.

Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri ya Maendeleo katika Eno la Ziwa Victoria Dkt Evans Atera anasema kuwa wakulima wengi huogopa teknolojia wakidai ni ghali bila kuzingatia kuwa wanaweza kukodi huduma hizo badala ya kununua trakta za mamilioni ya pesa.

Ili kufaidi kutokana na teknolojia hii, kampuni ya Tinga imekuwa ikiwarai wakulima kujiunga kwa vikundi ili kupunguza gharama kwa kutumia mashine kwa maekari ya ardhi.