Makala

AKILIMALI: Teknolojia ya kuongeza bidhaa thamani yawaajiri vijana 150

December 24th, 2020 2 min read

Na RICHARD MAOSI

Kulingana na Profesa Erastus Kang’ethe ambaye ni mhadhiri mstaafu kutoka Chuo Kikuu Cha Nairobi, vijana wanaweza kujiajiri katika sekta mbalimbali endapo watafanyia kazi ujuzi wanaopata kutoka taasisi za kiufundi.

Anasema inafaa wajitume na kuwa wenye subira kwa kuwekeza katika kilimobiashara, mijini au mashambani ili waje kuwa watu wa kujitegemea siku za baadaye badala ya kusubiri kazi za kuajiriwa.’

Licha ya watu wengi mashambani kutegemea kilimo cha mahindi, nyanya na ndizi, bado kuna nafasi nyingi za ajira ndani ya value chain, ambazo bado hazijavumbuliwa,’ akasema.

Uongezaji bidhaa thamani (Value chain) ni kuanzia pale mkulima anapopanda mazao yake shambani, kupalilia, kuvuna na hatimaye kusafirisha mazao viwandani kila hatua ikiajiri vibarua.

Akilimali ilipata fursa ya kutembelea taasisi ya Kenya Industrial Research and Development Institute (KIRDI) katika barabara ya Kisii-Keroka, viungani mwa mji wa Kisii ambayo hutoa mafunzo kwa vijana, na kuzingatia mifumo ya teknolojia.

Aghalabu huwa ikilenga kuwasaidia vijana wajianzishie miradi midogo kama vile kutengeneza lishe ya mifugo.Aghalabu mbali na kutengeneza aina mbalimbali ya lishe kutokana na matunda na mboga.

Kirdi inasambaza bidhaa hizi kwa maduka ya kijumla na shule.Tulikutana na Dennis Onyinkwa ambaye amefaidi na teknolojia ya kuzidisha thamani (value addition).

Anaweza kutengeneza sharubati, mikate, vibanzi na chakula cha watoto kutokana na ndizi aina ya carvedish.Isitoshe Dennis amepata ujuzi wa kutengeneza aina ya siagi ambayo imetengenezwa kutokana na zao la beetroot na hutumika kupaka katika mkate.

Anasema kuwa aina hii ya siagi ni bora kwa afya ikizingatiwa kuwa imetokana na hali halisi ya zao la beetroot bila kuongezewa kemikali za aina yoyote.Dennis alieleza kuwa awali alikuwa na wazo la kujifunza namna ya kuongezea bidhaa thamani ndiposa akatembelea taasisi ya Kalro (Kenya Agricultural and Livestock Research institute) kukutana na wataalamu

Alipata maelezo kuhusu aina mbalimbali za teknolojia za kilimobiashara, ndiposa akaamua kuzamia ile ya kutengeneza bidhaa kutokana na mazao ya ndizi, beetroot na maziwa.

Hapa ndipo alianza kuungana na vijana wengine, huku akiwahimiza wajaribu kupanda mazao ya beetroot na ndizi wengi wao wakiwa ni wale wanaotokea katika familia za wakulima mashinani.

Akiwa miongoni mwa vijana wengi wanaofaidi na mradi huu ambao umewaleta pamoja vijana zaidi ya 150, anasema serikali kuu iwekeze zaidi katika nguvu kazi ya vijana.

Kulingana na Dennis vibanzi vinavyoundwa kutokana na ndizi vinaweza kutengeneza Sh2200, badala ya Sh700. Hivyo basi mkulima anaweza kutengeneza faida ya Sh1500 kwa siku.Isitoshe Dennis amejifundisha teknolojia ya kukanda mikate kutokana na unga wa ndizi , na hatimaye kupakia katika mifuko maalum kabla ya kusafirishwa katika maeneo mbalimbali.

Anasema kuwa mboga na matunda huchukua sehemu muhimu sana kwa yeyote ambaye anajifundisha teknolojia ya kuongezea mazao yake thamani.

Pili aliongezea kuwa mazao ambayo yameongezewa thamani huchukua muda kabla ya kuharibika kwa sababu mara nyingi huwa yamekaushwa.hivyo basi yanaweza kudumu.

Kulingana na mwalimu wake Bi Aska Nyakwara walianzisha mradi huu wa kufundisha vijana mnamo 2008, ikizingatiwa kuwa kaunti ya Kisii ina mazao mengi ya shambani ambayo hayana soko.