Makala

AKILIMALI: Tuktuk zitumiazo biogesi kubadili sura ya uchukuzi

September 12th, 2019 3 min read

Na DENNIS LUBANGA na WANDERI KAMAU

HUENDA mahangaiko ya waendeshaji magari yakafika mwisho baada ya kampuni ya Biogas International Limited kuzindua tuktuk maalum inayotumia biogesi.

Kando na kuwaepushia wahudumu hao gharama kubwa ya mafuta, kampuni hiyo yenye makao yake katika eneo la Karen, jijini Nairobi inalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Kulingana na Meneja wa Mitambo katika kampuni hiyo Bw Josphat Chege, uvumbuzi wao ni wa kipekee, kwani tuktuk hiyo ni tofauti na zingine.

“Uchukuzi ni mojawapo ya matumizi ya biogesi. Muundo wa tuktuk hii ni wa kipekee, kwani ina tenki maalum ambalo huwekwa gesi hiyo ili kuisaidia kuendesha injini yake,” akasema Bw Chege.

Wakati Akilimali ilizuru katika makao ya kampuni hiyo jijini Nairobi, ilibaini kuwa kando na tuktuk hiyo, imeanza mikakati mingine mingi, ambayo lengo lake ni kuwaondolea Wakenya wengi changamoto wanazokumbaba nazo, hasa walio katika maeneo ya mashambani.

Bw Chege alisema kuwa tuktuk hiyo ina uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 80 tenki hilo likiwa limejaa. Chini ya tanki hilo mna betri maalum ambalo huhakikisha haizimi wakati gesi inaisha.

Alieleza kuwa vifaa vyao huwa vinakaguliwa kwa umakinifu ili kudumisha ubora wake.

“Tenki hilo hubeba kati ya lita 10,000 na 20,000 za gesi. Injini yoyote, iwe ya gari ama mtambo wa jenereta inaweza kuendeshwa kwa biogesi kwani mfumo wake wa matumizi ni sawa na wa petroli ama dizeli,” akaeleza.

Tuk tuk hiyo ni sawa kimuundo na gari litumialo gesi aina ya haidrojeni. Gesi hiyo hutumika kwa kuanzisha injini ya gari husika na kuliwezesha kusafiri ilikokusudiwa. Kijumla, matumizi ya gesi hiyo ni sawa na petroli ama dizeli, ila huwa magari hayo hayatoi moshi.

Kulingana wataalamu, kuna magari kadhaa ya muundo huo nchini, lakini utafiti zaidi unaendelea ili kueneza matumizi yake.

“Kwa sasa, inawezekana kutengeneza tuktuk hizi kwa wingi, kwani zina manufaa makubwa, hasa katika uhifadhi wa mazingira na uchafuzi wa hewa. Hata hivyo, changamoto ya pekee tuliyo nayo ni kuwa lazima tuweke biogesi katika matenki, jambo ambalo si rahisi. Ni shughuli ambayo huhitaji vifaa vya kisasa na watu wenye utaalamu mkubwa kuendesha mashine zinazotumika,” akaongeza Bw Chege.

Kampuni hiyo pia imeanza kuzalisha biogesi maalum inayoitwa Flexi Biogas, ambayo hutumika kuendesha tuk tuk hiyo na mashine mbalimbali.

“Huu ni mfumo maalum wa kuzalisha biogesi ambao ni rahisi kuuendesha. Vilevile si ghali hata kidogo,” akasema.

Alieleza kuwa kwa muundo wa tuk tuk hiyo, mtu anaweza kuitumia biogesi hiyo kwa mashine yoyote bila tatizo lolote.

Alisema kuwa uzuri wa biogesi ni kwamba huwa haihitaji kugeuzwa mfumo wake ili kuanza kutumika, kama ihitajikapo kwa petroli ama dizeli.

“Ni kawi ambayo iko tayari kutumika wakati wowote,” akaeleza.

Kulingana na Bi Victoria Ndung’u, ambaye ni meneja katika kampuni ya kuzalisha kawi ya Hivos, kuna haja ya serikali mbalimbali kote duniani kuunga mkono na kufadhili miradi ya kuzalisha biogesi, kutokana na manufaa yake mengi.

“Manufaa ya teknolojia ya biogesi ni uwepo wa kawi safi ya kupikia, kupunguza maradhi yatokanayo na kupumua, kuwawezesha wakulima kutumia mbolea safi kwenye kilimo kati ya mengine,” akasema Bi Ndung’u.

Alisema kuwa Kenya inapaswa kukumbatia miundo kama hiyo ya tuktuk kwani itasaidia sana kwenye harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Ingawa haijaanza kuuzwa, watengenezaji wake wanasema mojawapo ya manufaa yake ni kuwa inaweza kutumia gesi ya kawaida.

Hili linamaanisha kwamba mtu anaweza kwenda katika kituo cha kuuzia gesi na kujaziwa.

“Ingawa muundo wake ni tofauti na wa kipekee ikilinganishwa na tuk tuk zingine, inaweza kutumia gesi ya kawaida ama biogesi aliyojitengenezea mtumiaji,” asema Bw Chege.

Hata hivyo, anaeleza kuwa changamoto tu wanayokumbana nayo ni kuwa lazima mtumiaji awekewe gesi kwa kutumia mitambo maalum ambayo ni wao pekee waliyo nayo.

Mitambo hiyo pia ni ghali, hali inayoifanya kuwa vigumu kwa watu wengi kuimudu.

Ili kusuluhisha hilo, wameanza kuimarisha muundo wa mitungi hiyo, kuhakikisha kuwa atakayeinunua anaweza kujiwekea gesi mwenyewe bila kusumbuka kufika katika makao yao.

“Tuko katika awamu ya majaribio kabla ya kuanza kuziuza tuk tuk hizi kwa Wakenya. Tumeanza hatua za kuimarisha muundo wa mitungi kuwawezesha wanunuzi kujiwekea gesi wakati inapoisha,” akasema.

Watengenezaji wanasema kuwa gharama yake itakuwa juu ikilinganishwa na tuktuk za kawaida kwani imewachukua muda mwingi na teknolojia ya hali ya juu kuitengeneza.

Bei ya kawaida ya tuktuk ni Sh200,000 nchini. Watengenezaji wa tuktuk ya biogesi wanasema kuwa bei yake haitakuwa chini ya Sh300,000 ingawa itategemea tofauti na ubora wake wa kimuundo.