Makala

AKILIMALI: Ubunifu wa vyandarua vyeupe unavyoimarisha kilimo maeno kame

December 24th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Kutunza mimea kunategemea uwepo na upatikanaji wa maji ya kutosha hasa, unapovalia njuga ustawishaji wa mboga za majani, nyanya, karoti, mahindi na viazi .

Ingawa ukame ni changamoto inayowakumba wakulima wengi mashinani, sasa uvumbuzi unaonyesha binadamu anaweza kukuza mimea kupitia kiwango kidogo cha maji au umande unaopatikana katika udongo, majira ya asubuhi.

Aidha mbinu mpya za ukulima zinaonyesha kuwa mkulima anaweza kupigana na wadudu hatari kama vile sisimizi au jeshi la viwavi, wanaoweza kuvamia mimea, ingali shambani kabla ya kukomaa.

Mathew Kipsang Mutahi mwanafunzi wa zaraa kutoka kwenye taasisi ya Rift Valley Technical Training Institute (RVIST), akizungumza na Akilimali alituonyesha muundo mpya wa chandarua cheupe, kilichobuniwa na wanafunzi kwa ushirikiano na taasisi hiyo, zinazotumika kufunika mimea inayoendelea kua.

Vyandarua hivi ni rangi nyeupe kwa nje na rangi nyeusi kwa ndani ,ili kusawazisha miale ya jua inayofikia mimea .

Mutahi anasema utafiti wenyewe ambao sasa umepata mashiko ulilenga kuzuia mmomonyoko wa udongo, na kukuza mimea ya mboga za majani katika maeneo kame yanayohitaji kiwango kikubwa cha maji.

Katika kipande cha ardhi cha nusu ekari taasisi inakuza nyanya,kabeji na spinach ambacho hutumika kulisha shule na kuuza kwa soko la nje wakati wanafunzi wapo likizoni.

“Ingawa mradi wenyewe ni ghali kuanzisha, faida zake ni nyingi kwa sababu mkulima atajipunguzia gharama ya kununua maji wakati wa kiangazi kunyunyiziz mimea maji,”akasema.

Hii ni kwa sababu tandarua hizi maalum hutoa mazingira mazuri ya mimea kukua kwa kupunguza miale ya jua inayofikia mimea.

Mutahi alisema rangi nyeupe husaidia mimea kustahimili joto jingi wakati wa kiangazi,huku rangi nyeusi ikisaidia kukabiliana na baridi kali msimu wa masika.

Kabla ya kufukia mbegu ardhini mkulima anafaa kuchanganya mbegu zake na samadi, akisema kuwa hii ndio njia mwafaka ya kutekeleza kilimo kwa wakulima wazoefu wanaofahamu kutekeleza kilimo chenye tija.

Tukilinganisha na utumiaji wa kitalu mradi huu wa tandarua nyeupe ni nafuu , kwani itamgharimu mkulima takriban 300,000 kutengeneza kitalu cha kawaida.Ambapo tandarua katika shamba la nusu ekari sio Zaidi ya 50,000.

“Aidha mfumo wenyewe utahakikisha kuwa udongo unasalia kuwa safi na laini, kwa sababu mkulima hana wakati wa kutumia kemikali nyingi wakati wa kuangamiza vidudu kama ilivyo desturi,”akasema.

Mutahi anaona kuwa huu ni mfumo unaoenda kutatua matatizo ya wakulima wasiokuwa na njia mbadala ya kuzuia mmomonyoko wa udongo ikiaminika kua mifuko yenyewe hutengeneza matuta ya mchanga yanayoziba maji kusomba udongo.

Kwa upande mwingine tandarua hazitoi nafasi ya magugu kukua, hivyo basi humpunguzia mkulima gharama anayoweza kutumia kuajiri vibarua wakati wa kupalilia shamba lake.

Mutahi anasema serikali za kaunti kwa ushirikiano na wizara ya kitaifa ya kilimo iwawezeshe wakulima kukumbatia mradi kama huu ili kupunguza gharama ya kuzalisha mimea shambani.Pia anashauri wapatiwe elimu ya kutosha namna ya kufanikisha mradi kama huu ambao hauhitaji utumiaji wa kemikali nyingi zinazoweza kuchangia uharibifu wa mazingira.

“Kutumia kemikali nyingi kupita kiasi ndio chanzo cha kupoteza thamani ya mchanga wa asilia,”alieleza Bwana Mutahi.

Msimu uliopita shule ilipata mavuno ya kutosha na kama inavyoonekana wanaelekea kupendelea mifuko ya tandarua nyeupe kuliko utumiaji wa green house.

Aidha baina ya matuta kuna mkondo wa maji ambayo hayawezi kutangamana na mimea kwa njia yeyote ile labda wakati ambao tandarua hizi huwa zimetengeneza nyufa za kuingiza maji.

Lakini ili kuhakikisha kuwa mzunguko wa maji ni wakati wote,kuna mapipa ya lita 200 hivi yanayotumika kuvuna maji msimu wa mvua kwa ajili ya unyunyizaji.

Mutahi anasema hali imerahisishwa kwani mimea inaweza kupata maji kupitia drip irrigation, jambo linalohakikisha maji yanatumika kwa asilimia mia moja.

Mimea yote hatimaye inaweza kutumia maji kikamilifu ,kama tulivyoshuhudia nyanya na kabichi zilizowanda na kusheheni rangi ya kijani kibichi.

Mutahi aliongezea kuwa ifikapo msimu wa kuvuna mkulima anaweza kuondoa tandarua ili kurahisisha kazi ya kuvuna. Anasema kuwa ni mradi utakaowafanya vijana wengi hasa wanaokaa mijini kupenda kilimo kwani ni mfumo uliozingatia kilimo kidijitali.

Ambapo wengi wao hubakia kuwa safi na nadhifu hata baada ya kazi kwani hawawezi kupata kero kutokana na uchafu.

Taasisi ya Rift Valley Technical Training Insitute imekuwa ikitumia mradi wenyewe kufanyia utafiti na kituo cha kufanyia mafunzo kwa wakulima wenye azma ya kujikita katika ustawishaji wa mboga na nyanya.