Makala

AKILIMALI: Uchongaji vinyago jibu la uhaba wa kazi nchini, Kapesi ni mfano bora

August 15th, 2019 2 min read

Na CHARLES ONGADI

SOKO la New Magongo lililoko mita chache tu kutoka kituo cha polisi cha Changamwe, Mombasa ni maarufu sana kwa kazi ya uchongaji vinyago Pwani.

Hivi majuzi, Akilimali ilishika kiguu na njia hadi soko hili kujionea jinsi wananchi wa matabaka yote wanavyojipatia riziki.

Lakini tofauti na matarajio, hapa mbali na shughuli za uchongaji vinyago pia kuna watengenezaji vyatu vya kiasilia maarufu kama kirikiri ama akala.

Hata hivyo, tulibahatika kukutana na kijana Muthami Kapesi, anayejichumia hela kutokana na kazi ya uchongaji vinyago.

“Ninachonga vinyago kila sampuli hasa kulingana na oda ninayopata kutoka kwa wateja wangu wanaotoka sehemu tofauti nchini,” asema Muthami katika mahojiao hivi majuzi.

Muthami ni fundi wa kuchonga vinyago kila sampuli ikiwemo wanyama kama simba, ngiri, tembo,twiga, ngamia na hata bakuli.

Kulingana na Muthami, kazi hii alifunzwa na rafikiye Kalonzo Kyallo mwaka wa 1996 baada ya kumaliza masomo yake ya darasa la nane katika shule ya msingi ya Mlangeni huko Machakos.

Muthami aeleza kwamba alifahamu fika kwamba wazazi wake wangelimudu kumlipia karo ya kuendeleza masomo yake ya shule ya upili na kuamua kujitosa katika uchongaji vinyago kama kitega uchumi.

Ilimchukua kipindi cha miezi mitatu pekee kujifunza mbinu ya uchongaji vinyago kutokana na ari aliyokuwa nayo kujifunza kazi hiyo.

Hata hivyo, Muthami anafafanua kwamba kazi yake ni kuchonga vinyago kisha kuwaachia wenye kununua kazi ya kufanya marembesho wanayohitaji katika vinyago vyao.

Hununua miti anayotumia kuchonga vinyago vyake kutoka mjini Malindi na wakati mwingine kutoka nchini Tanzania.

“Kuna aina ya miti tunayotumia kuchonga vinyago inayopatikana hasa kutoka Malindi ama nchini Tanzania,” aeleza.

Kwa mfano anachonga kimoja cha twiga saizi ndogo kwa kati ya ksh 50 hadi ksh100 wakati kubwa akichonga kwa kati ya ksh 300 hadi ksh 500.

Kuna pia vinyago vya wanyama kama mbogo, simba, ngiri, na sokwe ambayo bei hulingana na umbo na mara nyingi hutoza kati ya Sh500 hadi Sh1000.

Wakati kazi inapokuwa nzuri, Muthami hupata oda ya kuchonga vinyago hata 100 ama hata 200 tofauti jambo ambalo wakati mwingine kuwaajiri wenzake kumsaidia.

Muthami anasema kwamba mara nyingi wateja wake huwa ni wenye maduka makubwa ya vinyago katikati ya miji ama katika hoteli za kitalii.

Wengi wao huja kutoka nchi jirani ya Tanzania kununua vinyago kwa minajili ya kwenda kuwauzia watalii wanaozuru nchi hiyo.

Aidha, Muthami asema ijapo kazi uchongaji vinyago imeweza kumkwamua kiuchumi lakini pia kuna changamoto anazopitia.

“Kuna wakati kazi huwa ovyo na ninaweza kumaliza hata miezi miwili bila kupata oda ya nguvu,” asema.

Muthami anaeleza kwamba mabroka wamewanyima nafasi ya kufaidi kutokana na ujuzi wao kwa kununua vinyago kutoka kwao kwa bei ya chini kisha kuwauzia watalii kwa bei ghali.

Mikakati

Anaiomba serikali kuingilia kati kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba ni wao ndio wanaowauzia wateja wao moja kwa moja bila kuwahusisha mabroka.

“Kwa mfano katika soko la dunia wanaopelekwa kuuza vinyago kamwe sio wachongaji bali wengi wao ni mabroka wanaojifanya kwamba wao ndio wenyewe na kufaidi kwa jasho si lao,” asema Muthami katika mahojiano.

Anawahimiza vijana kushikana pamoja na kubuni njia za kujipatia riziki badala ya kupoteza muda wakitafuna mogoka na miraa ambayo mwishowe huwashawishi kujitumbukiza katika maovu.