AKILIMALI: Ufugaji nyuki washika kasi biashara ya asali ikinoga

AKILIMALI: Ufugaji nyuki washika kasi biashara ya asali ikinoga

Na SAMMY WAWERU

BLOSSOMS & Beehives ni duka la asali katika Soko la Wakulima na Wafugaji la Nairobi Farmers Market lililoko katikati mwa jiji la Nairobi.

Akilimali inaelezwa kuwa mwasisi wa duka hilo alianza kwa kuuzia marafiki asali.

Kulingana na Dorah James ambaye ni mhudumu hapo dukani, mmiliki anayemtambua kama Millie, alianza kama jaribio.

Ni jaribio ambalo limeashiria mwanga wa ufanisi katika kukata kiu ya watumizi wa asali jijini Nairobi na viunga vyake.

“Alikuwa akiuzia marafiki, ambao baada ya kuona manufaa ya asali yenyewe na ubora wake, walirejea na wateja wengine,” Dorah asema.

Aidha, kilele chake kimekuwa kufungua duka katika soko lililoko katika mazingira ya hadhi.

Hata ingawa Dorah hana takwimu za kiwango cha mtaji ambacho Millie alitumia kufungua duka hilo la usambazaji asali jijini, kazi hiyo inaendelea kunoga.

Matumizi ya soko la Nairobi Farmers Market yalianza Desemba 2020, na kuzinduliwa rasmi mapema mwaka huu 2021.

“Maeneo ya mijini, wakazi wanageukia matumizi ya asali kwenye vinywaji badala ya sukari,” Dorah aelezea.

Kulingana naye, ongezeko hilo linaendelea kushuhudiwa hasa kipindi hiki taifa na ulimwengu unahangaishwa na Homa ya Corona.

“Wateja wetu, wengi wanasema wanachanganya asali na vinywaji vya mimea asilia kama vile ndimu, tangawizi na vitunguu saumu ili kupiga jeki kinga na kuongeza virutubisho mwilini,” Dorah akasema wakati wa mahojiano akiwa dukani.

Blossoms & Beehives ina mradi wa ufugaji nyuki Kaunti ya Baringo na Pokot Magharibi ili kuzalisha asali.

Dorah James akiwa dukani. Picha/ Sammy Waweru

Huongeza thamani kwa kusindika na mimea asilia inayotibu magonjwa mbalimbali, kama vile Lavender, Hibiscus, Acacia, Ginger, na pia kwa kutumia matunda ja Blueberries na mapera, kati ya mimea na matunda mengineyo.

Ufugaji wa nyuki hauna gharama ya juu. Unachohitaji ni kuwa na mizinga na kuwa katika mazingira yenye mimea au miti inayochana maua.

“Kwa mfano, wakulima wa maembe wana fursa ya kufuga nyuki na kujipa pato la ziada kupitia uuzaji wa asali,” John Ndung’u mkulima wa maembe Murang’a asema.

Mzee Ndung’u ana mizinga kadha katika shamba lake lililoko eneo la Kambiti.

Mizinga ya nyuki katika shamba la Mzee John Ndung’u eneo la Kambiti, Murang’a. Anafuga nyuki katika shamba la maembe. Picha/ Sammy Waweru

“Kando na mapato ya maembe, hurina asali ambayo ina donge nono,” anasema mkulima huyo anayekuza maembe katika shamba lenye ukubwa wa ekari mbili.

Kilo moja ya asali haipungui Sh600, na Ndung’u anasema kiwango anachozalisha hakikidhi idadi ya juu ya wateja anaopata.

Asali inasifiwa kutokana na sukari yake hai na vilevile kushehini madini na virutubisho ambavyo ni muhimu kwenye mwili.

Licha ya bidhaa hiyo kuwa yenye tija chungu nzima, mizinga inapaswa kuwa katika mazingira salama kwa sababu nyuki ni hatari kwa binadamu na wanyama.

You can share this post!

Nimerejea Manchester United izaliwe upya – Ronaldo

Nice waadhibiwa vikali baada ya mashabiki kuzua vurugu...