Makala

AKILIMALI: Ufugaji wa batamzinga, kanga na batabukini wampa kipato

March 14th, 2019 3 min read

NA PETER CHANGTOEK

KATIKA shamba la ekari mbili na nusu, katika eneo la Nanyuki, kaunti ya Laikipia, mabatamzinga, mabatabukini, kanga, pamoja na nyuni wengine wanatembeatembea wakijitafutia lishe.

Hili ni shamba linalomilikiwa na akina Onesmus Kibe, 26.

Mkulima huyo alijitosa katika ufugaji wa ndege hao takribani miaka miwili iliyopita, pasi na kujua kuwa ungempa faida.

Baba yake alikuwa amewanunua mabatamzinga wawili; mmoja wa kike na mmoja wa kiume kwa madhumuni ya kurembesha nyumbani kwake, lakini walipoongezeka, Kibe akawa na uchu na ari ya kuugeuza ufugaji huo kuwa biashara.

Batamzinga huyo wa kike alipoyaangua mayai, vifaranga kumi na watano wakapatikana. Baada ya kuwauza kumi kati yao, walipotimia umri wa miezi miwili kwa Sh2,000 kila mmoja, wakasalia na watano.

“Hapo ndipo tulipogundua kwamba ni biashara yenye faida. Nikawanunua wengine sita kutoka kwa wakulima tofauti tofauti,” asema Kibe, akiongeza kuwa kutoka wakati huo, amekuwa akiwauza mabatamzinga, akiwabakiza baadhi yao na kuwanunua wengine kutoka kwa wakulima wengine, ili kuepuka uzalishanaji miongoni mwa ndege wa uzao mmoja.

Mabatamzinga wawili walionunuliwa na babaye waliwagharimu Sh8,000; wa kiume Sh4,500 na wa kike Sh3,500.

Awali, alipokuwa limbukeni katika shughuli hiyo ya ufugaji, alikuwa akivitumia vifaa kama vile sahani ambazo hazikuwa na thamani na vifaa vingine vinginevyo vya plastiki kuwalisha ndege wake, ili kupunguza gharama ya uzalishaji.

Ndege wake wamejengewa vibanda kwa kutumia nyaya maalumu pamoja na mbao ili kuruhusu hewa safi na mwangaza kupenya ndani. Vibanda hivyo vimeinuliwa futi mbili juu kutoka ardhini.

Kibe anasema kuwa yeye huwalisha vifaranga wa mabatamzinga kuanzia wakati wanapototolewa hadi muda wa miezi mitatu uishe, kisha anawaachilia watembee kujitafutia lishe.

Hata hivyo, wanapokuwa wakubwa hulishwa mara moja kwa siku, kisha wao wenyewe hutembeatembea shambani ili kujitafutia lishe.

Mkulima huyo huwalisha ndege wake akizitumia lishe zinazonunuliwa madukani pamoja na samaki aina ya dagaa (omena).

“Mimi huongeza dagaa kwa lishe hizo ili kuiongezea protini. Pia, mimi huwachukulia mabaki ya chakula kutoka kwa hoteli kadhaa zilizoko katika eneo hili,” afichua Kibe.

Mkulima huyo anaongeza: “Mie huwalisha mara moja asubuhi wale wanaotembea kujitafutia lishe na huwalisha mara mbili vifaranga wanaosalia katika vibanda.”

Kwa wakati huu, mkulima huyo ana mabatamzinga 32 waliokomaa na vifaranga 53, mabatabukini 28, kanga 27 waliokomaa. Isitoshe, ana ndege wengine wa aina tofauti.

Kibe anasema batamzinga huyataga mayai kumi hadi kumi na mawili anapoanza, lakini anapokomaa, huyataga mayai takribani kumi na matano.

Anaongeza kwamba yai la batamzinga huuzwa kwa bei ya Sh150. Hata hivyo, wao hawayauzi mayai ya ndege hao.

Hakuna jambo lisilokuwa na changamoto. Kuna baadhi ya matatizo ambayo mkulima huyo anasema amewahi kupitia. Hana soko la kutegemea la mabatamzinga, mathalani kwa hoteli. Kwa hivyo, yeye huwategemea wanunuzi wa kawaida.

Aidha, kuna magonjwa kadha wa kadha, ambayo anasema huwaathiri ndege wake na hivyo kuathiri uzalishaji.

Mbali na hayo, anaongeza kusema kwamba bei ya lishe iko juu mno na gharama ya kuwapa chanjo ndege hao pia iko juu. Hali kadhalika, ni changamoto kwake kuwauzia wateja walioko katika maeneo ya mbali kama vile Kisumu, licha ya kupata oda kutoka maeneo hayo.

“Mimi hutumia matatu zinazohudumu kutoka hapa Nanyuki, kwa hivyo ni vigumu kuwasafirisha kwa miji ya mbali kama vile Kisumu, japo nina wateja wanaotaka kuuziwa kule,” aongeza.

Kibe humuuza batamzinga mwenye umri wa miezi miwili kwa bei ya Sh1,800.

Yule mwenye umri wa miezi mitatu hadi minne huuzwa kwa bei ya Sh3,500 hadi Sh6,000.

Pia, yeye humuuza batabukini mwenye umri wa miezi miwili kwa bei ya Sh2,500, ilhali yule aliyekomaa humuuza kwa bei ya Sh3,500.

“Mimi humuuza kanga mwenye umri wa miezi mitatu kwa bei ya Sh2,500 ilhali yule ambaye amekomaa humuuza kwa Sh3,500,” aongeza.

Mkulima huyo anafichua kuwa yeye huwauza ndege wake wengi kupitia kwa mitandao ya kijamii na huwauzia wateja kutoka miji tofauti tofauti mathalani Isiolo, Nakuru na Nairobi.

“Pia, nina wateja hapa. Wateja wangu wengi huwanunua ili kurembesha nyumbani kwao. Hata hivyo, mimi huwapata wateja wanaowanunua kwa ajili ya nyama, nyakati za likizo,” Kibe adokeza.

Mkulima huyo anaongeza kuwa huuza nyama ya mabatamzinga kwa bei ya Sh900 kwa kilo moja.

Anawashauri waja wasiogope kujitosa katika ufugaji wa mabatamzinga “kwa kuwa biashara hiyo ina faida na ni rahisi kuwatunza ikilinganishwa na ndege wengine”.

Hata hivyo, anawasihi wafanye utafiti kwanza kabla hawajajitosa katika shughuli hiyo, ili wapate ujuzi wasije wakaingia kwenye hasara kwa kukosa habari muhimu.