Makala

AKILIMALI: Ufugaji wa kuku faida tele Krismasi

December 24th, 2019 3 min read

Na PETER CHANGTOEK

ALILELEWA katika familia inayojishughulisha kwa kilimo cha ufugaji wa kuku pamoja na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ukuzaji wa mimea kama vile mihindi, minanasi, michai, migomba pamoja na mboga na matunda.

Na baada ya kujifunza kutoka kwa wazazi wake kuhusu jinsi ya kuwafuga kuku, mbali na kusoma makala mbalimbali kuwahusu wakulima waliofanikiwa kwa kilimo hicho, Emanuel Kiprono aliamua kujitosa katika zaraa hiyo ya ufugaji wa kuku pamoja na ndege wengine mnamo mwaka 2014, akishirikiana na dada yake Edna Mibei, kwa kuutumia mtaji wa Sh5,000, pesa taslimu ambazo anasema walizitumia kuwanunua kuku 20.

Hata hivyo, anasema kuwa fedha hizo hazikujumuisha zile za kuvijenga vibanda vya kuwafugia ndege hao, maadamu vilikuwapo vibanda ambavyo vilikuwa vimejengwa tayari, vilivyokuwa vikitumiwa awali kwa shughuli kama hiyo.

Kiprono, ambaye anakiendeleza kilimo hicho katika kitongoji cha Kiptobon, umbali wa takribani kilomita moja na nusu kutoka kituo cha biashara cha Roret, katika Kaunti ya Kericho, anasema kwamba kwa sasa, ana jumla ya kuku 150. Hata hivyo, anafichua kuwa idadi ya juu zaidi ya kuku ambao amewahi kuwa nao ni kuku 650.

Hali kadhalika, anasema kwamba idadi ya juu zaidi ya kuku ambao amewahi kuwauza kwa mkupuo mmoja ni kuku 150, anaosema kuwa aliwauza kwa hoteli moja kule Kisii, mnamo kwa bei ya Sh500 kila mmoja, ambapo alitia kibindoni Sh75,000. Msimu wa Krismasi, yeye hutia mfukoni maelfu.

Licha ya hayo, anasema kwamba alishurutika kuipunguza idadi ya kuku aina ya ‘kuroiler’ kwa sababu ya ukosefu wa soko na kuwauza wengine waliosalia kwa bei ya Sh400 kila mmoja.

“Kuku hao (kuroiler) walikuwa wengi ikilinganishwa na idadi ya ‘broilers’ ambao huhitajika sana kwa hoteli nyingi,’’ asema mkulima huyo, ambaye ni hadimu katika sekta ya kilimo, kwa kampuni moja ya mbegu iliyoko mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Anadokeza kwamba alijitosa katika shughuli ya ufugaji wa kuku kwa sababu kadha wa kadha. Mojawapo ya sababu hizo, ni kuwa ufugaji wa kuku hauhitaji nafasi au shamba kubwa linalofaa kutumiwa kwa shughuli iyo hiyo. Pia, anaongeza kuwa ufugaji wa kuku hauhitaji mtaji mwingi wa kuuanzisha.

Mkulima huyo, mwenye umri wa miaka 33, anaongeza kuwa kuku wanaweza kumpa mfugaji faida ya haraka. Isitoshe, anasema kuwa ni rahisi kuwatunza ndege hao.

Kwa mujibu wa Kiprono, ni kuwa, wao hukusanya mayai kati ya 20 na 30 kwa siku moja, japo azma yake ni kuyatotoa mayai hayo ili kuwapata vifaranga wa kuuza.

“Hatuna nia ya kuyauza mayai kwa wakati huu, mtazamo wetu ni kuyatotoa na kuwauza vifaranga kwa Sh100 hadi Sh150. Lakini, likiuzwa, yai moja laweza kuuzwa kwa bei inayofika Sh20,’’ afichua mkulima huyo, ambaye ana shahada katika masuala ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Shamba ambalo mkulima huyo analitumia kuiendeleza shughuli hiyo ni 0.2 ekari, ambapo ndege hao huruhusiwa kurandaranda kusudi kupata lishe za ziada. Hata hivyo, anasema kuwa kuku hao hulishwa pia kwa lishe zinazouzwa, ambazo huchanganywa na lishe za kienyeji.

Aidha, mkulima yuyo huyo anaongeza kuwa kuku hao hulishwa kwa mahindi yaliyopondwapondwa, masalio ya dagaa, mchele kutoka kwa viwanda vya Ahero, miongoni mwa lishe nyinginezo.

Anasisitiza kwamba huwaruhusu ndege hao kutembeatembea shambani kujitafutia lishe kwa ajili ya kuboresha mayai na nyama kutoka kwao.

Mbali na kuwafuga kuku, yeye pia huwafuga ndege wengine wengineo, kama vile mabatabukini, mabatamzinga, pamoja na kanga. Anasema kuwa kwa wakati huu, ana ndege aina ya kanga watano (5) waliokomaa, mabatabukini saba (7), mabatamzinga kumi na sita (16) waliokomaa, pamoja na tisa (9) ambao hawajakomaa.

Yeye humwuza kuku mmoja wa kienyeji kwa bei ya Sh800, batamzinga aliyekomaa kwa bei ya Sh3,500, na kanga kwa Sh3,000.

Anadokeza kwamba bei ya ndege hao ni bora kuliko ile ya kuku. Fauka ya hayo, anasema kuwa mabatamzinga hukua na kukomaa upesi mno. Mkulima huyo, pia, anasema kuwa gharama ya ufugaji wa ndege hao si ya juu.

Hata hivyo, kuna baadhi ya changamoto, ambazo anasema amewahi kuzipitia. Miongoni mwa ndaro hizo ni pamoja na wadudu na magonjwa, ambayo huwakabili kuku. Pia, anasema kuna changamoto ya kuyatotoa mayai ya mabatabukini. “Pia, mie ni limbukeni kwa uzalishaji wa kanga,’’ adokeza.

Kwa wale wanaotaka kujitosa katika shughuli za zaraa, mkulima huyo anawasihi kutathmini uwapo wa soko kwanza. “Uwapo wa soko ni jambo ambalo ni muhimu sana kabla ya kujihusisha kwa shughuli zozote za kilimo,’’ asema.

Anaazimia kuongeza idadi ya mabatamzinga kuwa zaidi ya mia moja. Pia, anapania kuongeza idadi ya mabatabukini pamoja na kanga kwa kuwa bei za kuuzwa kwao ziko juu kuliko kuku.

Isitoshe, ananuia kujihusisha kwa ufugaji wa kuku wa kienyeji wanaoruhusiwa kutembeatembea, kwa kuwa wao huhitajika mno masokoni.