Makala

AKILIMALI: Ufugaji wa samaki kwa njia za kisasa

November 28th, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSI

SIKU hizi maendeleo ya kiteknolojia yamewezesha wakulima kuendesha ufugaji wa samaki kwa gharama nafuu bila kuchimba ardhi wala kutumia vyombo vya bei ghali wakati wa kuendesha shughuli yenyewe.

Mbali na kutoa ushauri nasaha kuhusu upatikanaji wa soko la samaki nchini, Chuo Kikuu cha Eldoret ni kielelezo cha taasisi zinazofanya utafiti kuhusu aina mbalimbali ya samaki kwa kuzingatia namna ya kuwatunza.

Mambo ya kimsingi yakiwa ni pamoja na lishe, mazingira bora (ubora wa maji yasiwe ya chumvi nyingi wala madini ya calcium yanayoweza kuleta uchachu) na kuandaa utaratibu wa kudhibiti mkurupuko wa maradhi.

Kwa wakulima wa kiwango kidogo wanaozunguka Uasin Gishu, ufugaji samaki umewapa mtazamo mpya, kinyume na zamani ambapo walitegemea mifugo kama ng’ombe na mbuzi kujikimu katika maisha ya kila siku.

“Malengo makubwa ikiwa ni kufanikisha uzalishaji wa vidagaa vya samaki wengi katika sehemu ndogo, kwa kutumia ubunifu na uangalizi wa makini kwa sababu, upatikanaji wa samaki katika vyanzo asilia vya maji unaendelea kuporomoka,” akasema Lazarus Tarus msimamizi wa mradi huo kutoka Chuo Kikuu Cha Eldoret.

Lazarus anasema mradi huu wa kufuga samaki waliokomaa ulianza mnamo 1991, lakini ule wa samaki wadogo (hatcharies) ulianzishwa yapata miaka minne iliyopita ili kudhibiti soko la samaki kwa wakulima wenye nia ya kujianzishia miradi midogo kama hii.

Kulingana na Lazarus ufugaji wa samaki wadogo una manufaa mengi kuliko wale waliokomaa, kwa sababu nyingi, mojawapo ikiwa ni kuwa vidagaa vya samaki huchukua muda mfupi wa miezi minne hivi kukomaa.

Pili huweza kumpa mkulima hela za haraka ikikadiriwa kidimbwi kimoja kinaweza kuhimili idadi kubwa ya samaki wadogo, katika sehemu ndogo endapo mradi wenyewe utaendeshwa namna inavyostahili.

Lazarus anasema mradi wenyewe umepiga hatua kiasi kwamba wanaendesha ufugaji huu ndani ya kitalu, ili kutoa mazingira ya joto la kadri katika ukuaji wa samaki wadogo wanaoweza kuathirika na maji baridi yanayopatikana kwa wingi katika Bonde la Ufa.

Ingawa ufugaji wa samaki una changamoto zake hasa pale ambapo mzunguko wa maji ya kutoka na kuingia ndani ya vidimbwi umeziba, kwani itafanya maradhi yanayosababishwa na fangasi kusambaa kwa samaki wadogo wasiokuwa na kinga ya kutosha.

Kufikia sasa, Chuo Kikuu cha Eldoret kinamiliki mabwawa yaliyotengenezwa kwa vifaa vya kawaida tu kama vile tandarua zilizozungushiwa mbao za kawaida, zilizolainishwa kwa kupiga msasa wa randa.

Kwa jumla wanamiliki mabwawa 22, ambapo 14 hubeba samaki waliokomaa na mabwawa mengine 8 yaliyosalia hutumika kufuga samaki wadogo, ambao wanaonekana kuteka shughuli nzima kutokana na ufaafu wao katika kilimo biashara na ushindani mkali wa mayai ya samaki sokoni.

“Kila kidimbwi cha samaki wadogo kinaweza kubeba samaki 5000 na kwa jumla vidimbwi vinane vinaweza kubeba samaki 40,000 ambao hawajakomaa bila kuorodhesha wale waliokomaa,”akasema.

Alifichulia Akilimali kuwa soko la samaki linaendelea kupanuka kote nchini kwa sababu ya watu wengi kupendelea kitoweo hiki kisichokuwa na madhara mengi kiafya, kama vile nyama ya ngómbe na mbuzi zinazohusishwa na kisukari na saratani ya damu.

Alieleza kwa wakati mmoja baada ya kuvuna mara moja tu, kwa kipindi cha miezi minne Chuo kinaweza kutengeneza hadi 400,000 kwani samaki mdogo ambaye hajakomaa huuzwa kwa shilingi 10.

Aliongezea kuwa Ili samaki waweze kuchukua muda mfupi kukomaa, wanastahili kulishwa mchanganyiko wa aina mbalimbali ya lishe ambayo ni mchanganyiko wa chakula za kiasili na zile za viwandani.

Lazarus anasema yeye huwalisha samaki waliokomaa mara mbili kwa siku yaani mchana na jioni.

Lakini vifaranga wa samaki hulishwa kila baada ya saa mbili, akiongezea kuwa haifai kuwalisha samaki vidonge vikubwa vikubwa ama chakula chenye vumbi,kwani huenda vikadhuru koromeo zao pamoja na kuleta uzito unaoweza kufanya washindwe kuelea vyema.

Kwa kawaida samaki hawapati athari kubwa ya maradhi ya kuambukizana isipokuwa yale yanayotokana na vimelea vinavyokuwa majini au minyoo,” akaongezea Bw Lazarus.

Atoa ushauri

Lazarus anatoa ushauri kwa wakulima wa samaki kuongeza mabwawa ya kuwafugia samaki wake kila mara idadi yao inapoanza kuongezeka, na kupitisha idadi ya 1,500 katika kila bwawa.

Ishara wanazotoa samaki pale wanapoanza kuugua ni kama vile kushinda katika sehemu moja ya bwawa kwa muda mrefu, na kukosa hamu ya kula chakula wanachorushiwa majini kama punje za unga .

“Ingawa tiba inayojulikana na kuzoeleka sana ni kuwatumbukiza samaki ndani ya bwawa la maji yenye chumvi kisha ukawarudishwa bwawani,”aliongezea.

Hata hivyo anasema ufugaji wa samaki umekuwa na changamoto nyingi hasa ijapo katika sehemu ya kutafuta lishe ambazo mara nyingi huwa ni bei ghali,viwandani na hazipatikani kwa urahisi.

Jambo hili limekuwa likiwafanya wakulima kuwalisha samaki na vyakula visivyokuwa na ubora ambayo hufanya samaki kudumaa na kupoteza thamani.

Wawekezaji katika miradi ya kufuga samaki kote nchini wanaweza kufikia malengo ya kustawisha miradi mikubwa endapo serikali itawekeza katika wizara ya mazingira ili kuhakikisha kuwa maji hayachafuliwi kutokana na shughuli za kibinadamu kama vile ukataji miti ovyoovyo.