Makala

AKILIMALI: Ugumu wa kazi EPZ ulimpa wazo la biashara ya vinyago

March 14th, 2019 2 min read

Na CHARLES ONGADI na HASSAN POJJO

AKILI ni nywele na kila mtu ana zake.

Hii ndiyo kauli ya Bi Elizabeth Musyoki ambaye licha ya kutokuwa na ujuzi wa kuchonga vinyago lakini amekuwa akivuna pato kutokana na uuzaji.

Ni katika eneo la Akamba Handcraft eneo la Changamwe, Mombasa ambako tunamkuta Bi Musyoki akiwa katika pilkapilka zake za kusaka mkate wake wa kila siku akiuza vinyago aina mbalimbali.

“Naam, hapa ndipo napatia riziki yangu ya kila siku na wala sijuti kufanya kazi hii inayofanywa sana na akina baba,” asema Bi Musyoki alipotembelewa na Akilimali katika duka lake eneo la Akamba Handcraft.

Bi Musyoki aliamua kuacha kazi katika kampuni ya EPZ na kuamua kujitosa katika biashara ya kununua na kisha kuuza vinyago.

Bi Elizabeth Musyoki akiwa katika duka lake eneo la Akamba Handcraft, Changamwe, Mombasa. Picha/ Hassan Pojjo

Kulingana naye, hakuweza kumudu ugumu wa kazi katika kampuni hiyo ambayo nusura iathiri afya yake.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10, Bi Musyoki ameibuka kuwa muuzaji stadi wa vinyago jimbo la Pwani kutokana na weledi wake wa kuelewa matakwa ya wateja wake.

Anasema kwamba licha ya kutokuwa na ujuzi wa kuchonga sanamu, kajaaliwa na Maulana jinsi ya kuchuma mali kutokana na uuzaji wa vinyago anavyonunua kutoka kwa wachongaji katika karakana ya Akamba Handcraft iliyoko Changamwe.

Mbali na kununua na kuuza vinyago kadhalika Bi Musyoki anaelewa barabara jinsi ya kuremesha vinyago hivyo ili kuvutia zaidi wateja.

“Kwa siku naweza kurembesha vinyago zaidi ya 25 na kuvuna kati ya Sh500 hadi 1,500 mbali na kuuza aina mbali mbali ya vinyago,” afichua.

Anaeleza kwamba mara baada ya kununua vinyago katika karakana kutoka kwa wachongaji, huanza kusaka soko hasa maeneo yanayotembelewa na watalii kutoka ughaibuni ambao hupenda sana bidhaa zake.

Mara nyingi, Bi Musyoki huuza vinyago vyake maeneo ya Malindi, Ukunda, Voi na Narok ambako kwa siku anaweza kuvuna kati ya Sh5,000 hadi 10,000 kulingana na hali ya soko.

Anakiri kwamba ameweza kupiga hatua kubwa tangu ajitose katika biashara hii anayosema imeweza kubadilisha maisha yake maradufu.

“Ni biashara nzuri ambayo naipenda kwa kuwa haina presha, ninaifanya kwa wakati wangu bila kushurutishwa na yeyote kama niliyofanya awali iliyokuwa ngumu kupindukia na yenye mapato duni,” asema Bi Musyoki.

Anasema kwamba siri kuu ya mafanikio yake katika biashara hii inayotawaliwa sana na wanaume ni kujituma kila mara kazini.

Misukosuko ya kisiasa

Hata hivyo, analalamika kwamba biashara yake huathirika nyakati za misukosuko ya kisiasa ya baada ya uchaguzi wakati wateja wake wengi ambao ni watalii wanaozuru nchini hukataa kuzuru nchini.

Ni katika kipindi hicho ndipo hulazimika kuuza vinyago hivyo kwa bei ya kutupa ilmradi ameweka chakula mezani.

Bi Musyoki anawaasa akina mama wenzake kujituma kwa kila wanalofanya hasa katika biashara na bila shaka matokeo mazuri watayaona.

Kama wasemavyo wavyele kwamba mchagua jembe si mkulima, Bi Musyoki anawaasa akina mama wenzake walio mijini kujituma kila wakati kwa kufanya kazi yeyote halali inayoweza kuleta mapato.