Makala

AKILIMALI: Ujuzi wa kutengeneza sabuni wageuka lulu maishani mwake

August 22nd, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

LICHA ya kwamba John Kuria alipata alama 386 katika mtihani wake wa darasa la nane (KCPE) mwaka wa 2007 wenye alama jumla 500 na akaitwa kujiunga na shule ya upili ya Mang’u, hakusonga mbele kielimu.

Kisa na maana? Kupita kwake mtihani huo kuliwatenganisha wazazi wake baada ya babake mzazi kushikilia kuwa hakuwa na pesa za kumlipia karo naye mamake akishikilia kuwa ni ama Kuria alipiwe karo, au talaka itokee katika ndoa hiyo.

“Babangu ambaye alikuwa kibarua tu wa pato la chini alisema kuwa hakuwa na pesa za kunilipia karo, akisema kuwa nilifaa kuachana na masomo ili niwape ndugu zangu wengine watano nafasi ya kupata angalau elimu ya hadi darasa la nane,” anasema Bw Kuria.

Wote kwa pamoja ni watoto sita.

Kwa upande wake, mamake alishikilia kuwa Kuria akiwa mwerevu zaidi alifaa kuwekezewa rasilimali kwa kuwa alionyesha mapema kuwa angeishia kuwa mtu wa maana maishani.

Tofauti hizo za kimtazamo zikaishia babake kung’ang’ania kuwa hakuwa na pesa, naye mamake akishikilia ni ama Kuria asome au talaka itokee.

Talaka ndiyo ilitokea.

Mamake aliingia katika ajira ndani ya shamba moja la kahawa lililo karibu na mji wa Thika akiwa na matumaini makuu kuwa angepata pesa za kumwezesha Kuria kujiunga na elimu ya sekondari.

“Akiwa sasa ndiye tegemeo la kipekee kwa sote sita ndani ya familia yetu, aligundua kuwa malipo aliyokuwa akilipwa yangetosheleza tu mahitaji ya kimsingi na sikuwa na lingine ila tu kujiunga naye katika ajira ya Mzungu ndani ya shamba hilo ili tusaidiane yeye kulea wanawe nami kwa maana ya kusaidia ndugu zangu,” anasema Kuria.

Ndipo ndoto yake ya kuishia kuwa rubani katika siku zake za usoni iliyeyuka kama hewa yabisi.

Mwaka wa 2011, Kuria alitimiza umri wa miaka 18 na ndipo akajisajili katika shule ya uendeshaji magari na ambapo baada ya kuhitimu, aliajiriwa katika kampuni moja ya maziwa mjini Thika.

Mtengenezaji sabuni, John Kuria akiwa katika maabara yake katika Kaunti ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Mwaka wa 2014 akawa amejinunulia pikipiki ambayo aliwekeza katika uchukuzi wa umma almaarufu bodaboda.

Juni 15, 2014, akiwa katika harakati za kusaka wateja wa kupeleka mahali alipwe, akajipa mteja aliyeishia kubadilisha maisha yake kwa kiwango kikuu na ambaye leo hii ndiye injini ya ufanisi wa maisha yake.

“Leo hii kwa mwezi mimi najipa pato la Sh250,000 kama faida. Nina magari yangu mawili. Mimi ni mwajiri kwa watu 10 na ambapo kwa mwezi uo huo mimi huwalipa jumla ya Sh150,000. Nimejinunulia vipande vya ardhi na ploti, nimejenga na nimewaokoa mama yangu pamoja na watoto wake kutoka kwa umaskini,” anasema.

Anaongeza: “Leo hii kuna masuala mawili ambayo siwezi nikasema hunipa majuto: Ukosefu wa elimu na kukosa kuajiriwa.”

Aidha, anasema kuwa kuna tatizo moja la kimaisha ambalo kwake ni geni: umaskini.

Kumbe yule mteja wa kiume ambaye alijitokeza kwa huduma yake ya bodaboda Mjini Thika alikuwa mfanyakazi katika kampuni ya moja maarufu, akiwajibishwa kitengo cha utengenezaji sabuni.

“Niligundua kuwa alikuwa amewekeza ujuzi wake wa ajira ndani ya kampuni hiyo kutengeneza sabuni katika maabara yake ya kibinafsi na tukiwa katika harakati za kuongea kama mteja na mhudumu, akanipa kazi ya kusafirisha sabuni alizokuwa akitengeneza hadi kwa wateja wake mjini Thika,” anasema.

Anasema kuwa alitekeleza wajibu huo kwa uaminifu na kujitolea kiasi kwamba urafiki ulijiri kati yake na mwajiri wake na ambapo baada ya kumhadithia kuhusu maisha yake na jinsi alivyokosa elimu, baraka ya kimaisha ikamtokea.

“Huyo mwanamume aliniambia kuwa angenipa ufunguo wa ufanisi katika maisha yangu. Aliniambia kuwa angenifundisha jinsi ya kutengeneza sabuni. Na akafanya hivyo na amini usiamini, alikuwa akitengeneza sabuni hizo akitumia nyanya na vitunguu kama malighafi,” anasema Bw Kuria.

Kuria alirejea hadi nyumbani kwao katika kijiji cha Kambi kilichoko katika Kaunti ya Murang’a na akaanza kutengeneza sabuni akitumia ujuzi huo aliokuwa amepewa na mwajiri wake.

“Nilianza kwa kununua vitunguu na nyanya, nikalipa nyumba ya kuzindulia biashara yangu na kwa ujumla, mtaji wangu wa kwanza ulikuwa wa Sh1,200,” anasema.

Yeye hutengeneza sabuni za kuogea na pia za kufua nguo, zote zikiwa sabuni za ‘miti’ wala sio za unga au za maji.

Katika kipindi cha wiki moja, alijipa faida ya Sh3,000 kutokana na mauzo ya sabuni vipande 100 na ambapo pikipiki yake ilimfaa sana katika kuafikia wateja.

“Tukiingia mwaka wa 2018, biashara yangu ilikuwa imeshika kasi kiasi kwamba aliyenijua wakati wangu wa shidashida za kimaisha angeshuku kuwa nilikuwa najichapishia pesa bandia nyumbani kwangu. Pesa zilinitembelea kama Baraka ya moja kwa moja kutoka kwa Maulana,” asema.

Bw Kuria anasema kuwa leo hii ako katika harakati za kujiimarisha ili azindue kampuni kubwa ya utengenezaji sabuni na pia taasisi ya kuwapa ujuzi vijana wa kutengeneza sabuni.

“Kwa kila mmoja natoza ada ya Sh3,000 ili kumpa uwezo na ujuzi wa kujitengenezea sabuni. Sina taharuki kuwa nikiwahami wengi na ujuzi huo watashindania soko na mimi. Hapana, sabuni ni bidhaa moja ambayo itabakia kwa soko kwa muda mrefu ujao,” anasema.

Katika harakati hizo, wengi ambao wamefika kwake kuelimishwa kuhusu jinsi ya kutengeneza sabuni hizi huishia hata kusajiliwa naye ili kuafikia mahitaji ya soko.

“Ninaweza kuwa nimepewa zabuni kubwa ya kuuza sabuni na huwa nawapa asilimia kidogo ya soko hilo ili nao wapate yao ili wajipe matunda ya uwezo wao,” anasema.

Lengo lake kuu la maisha ni kujijenga akijenga wengine katika jamii na asaidie wengi kukwepa janga la umaskini uliomfanya akose elimu na karibu umhukumu pamoja na mama na ndugu zao kuwa vibarua maskini katika utumwa wa ajira ndani ya shamba la kahawa.