Makala

AKILIMALI: Ukale una thamani

November 6th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

TAIFA Leo Dijitali ilipomtembelea Mzee wa Mtaa, Bw Hussein Abubakar, 74, ambaye ni mfanyabiashara wa kazi za sanaa za kale, alikuwa anaendelea kupanga vitu hivyo katika meza yake iliyo karibu na ngome ya Fort Jesus, katika Kaunti ya Mombasa.

Kwa miaka minane sasa, mzee huyu wa mtaa Old Town amekuwa akiuza kazi hizo za sanaa kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali nchini, na hata kutoka mataifa mengine.

Bidhaa zake zimetengenezwa kwa vyuma vya shaba nyekundu na shaba nyeupe na bei ni kati ya Sh300 hadi Sh7,000.

“Bidhaa nyingi hapa zinatoka ng’ambo, haswa nchi za bara Asia,” akasema Abubakar.

Katika meza yake, baadhi ya vitu vilivyopangwa kwa njia ya kuwavutia wageni ni sahani, bakuli kubwa, karai za kukarangia vyakula mbalimbali, birika za kahawa, buli ya chai, kikaango, vikombe vidogo vya kahawa na mvinyo, sufuria na vikombe vya maji.

Pia, kuna kengele zilizotumika ndani ya meli, visu, vijiko, vidude vya kuzima na kushikilia mishumaa na majagi.

“Wateja wangu wengi hununua bidhaa hizi kurembesha nyumba zao. Wengi huvichukua wakavipaka rangi upya ili kuving’arisha tena,” akasema Bw Abubakar huku akiongeza kuwa wateja wake wengi walikuwa wazungu miaka ya nyuma lakini sasa, watalii wa humu nchini ndio wanampa riziki.

“Kila siku huwa nakuja kazini, kisa mazaoea, kwani najua Mungu Ndiye Anatoa riziki,” akasema huku akilalamikia hali mbaya ya biashara ambayo imesababishwa na janga la corona.

Hata hivyo, anasema kuwa ana matumaini makubwa serikali ya Kaunti ya Mombasa itawapa msaada wa kifedha ili waweze kuinua biashara zao ambazo ziliathirika pakubwa na kuwepo kwa virusi vya corona nchini, na zaidi marufuku ya kuingia na kutoka katika eneo la Old Town baada ya idadi ya watu walioambukizwa maradhi ya Covid-19 kuongezeka.

Baadhi ya sanaa za kitambo ambazo Bw Hussein Abubakar anaziuza karibu na ngome ya Fort Jesus, Mombasa. Picha/ Diana Mutheu

“Corona imelemaza uchumi wetu, lakini bado tuna matumaini kuwa tutapata wageni baada ya hoteli na hata makavazi ya Fort Jesus kufunguliwa,” akasema.

Alisema kuwa kazi hiyo imemwezesha kukimu mahitaji ya familia yake, huku akiwapa vijana mawaidha kuwa wasitegemee kazi za ofisi kila wakati, bali wawe wavumbuzi wa kuanzisha biashara zao wenyewe.

“Vijana wa sasa, sio wengi wapendao kazi za biashara, bali wanataka kazi za kutumwa. Hakuna kazi nzuri kama ile ya kujituma. Biashara zote zimebarikiwa na Mungu, kilichobaki ni mtu kufanya bidii tu,” akasema.