Makala

AKILIMALI: Ulemavu haujamzuia kubobea katika sekta ya kilimo na ufugaji

December 24th, 2020 2 min read

Na HAWA ALI

Kuna msemo usemao, “shida si kuzaliwa maskini bali kuishi kimaskini”. Msemo huu ni wa maana sana na unabeba ukweli mzito.

Katika kuwadhihirishia wakulima kuhusu hili, Akilimali ilipata fursa ya kumtembelea mmoja wa wasioona Bw Raphael Gitonga anayeishi katika kijiji cha Ma Acre, Kaunti ya Kiambu.

Gitonga anasema kuwa alipata tatizo la kuumwa na macho akiwa darasa la pili na kutibiwa kwa dawa za kienyeji zilizomsababisha mboni ya jicho kuoza na hatimaye kumletea upofu.

Anasema kuwa, kutoona hakumnyimi yeye fursa ya kujishugulisha na kilimo na kupata faida kubwa kuliko hata wasio na tatizo lolote.“Mimi nina tatizo la kutoona, lakini namshukuru Mungu kwani natumia hisia za miguu na mikono katika shughuli zangu zote za kila siku, hasa za kilimo ambayo ni shughuli inayoniingizia kipato kama watu wengine na ninakipenda sana,” alisema Gitonga.

Anaongeza kuwa, akiwa shambani, hutumia miguu sana na mara chache mikono ili kutambua kuwa amelima wapi na wapi bado.

Mkulima huyu asiyeona, anatambua ukubwa wa eneo la shamba lake kwa kutumia miguu kupima, na hata kwenye kupalilia mazao yake anajua kuwa hili ni zao na hili ni gugu na kamwe hafanyi kosa.

Kuhusu alivyojiingiza katika kilimo, Raphael anaeleza kuwa, wazazi wake walimkuza katika misingi ya kutegemea kilimo. Aidha, shule ya msingi aliyosomea (ACK Kaanwa Primary-Meru) walikuwa wakifanya shughuli za kilimo, hivyo kuendelea kumjengea msingi wa kupenda na kuthamini zaidi kilimo.

Alieleza kuwa, hata alipoweza kujiunga na shule ya sekondari ya Njia Boys, Meru ambapo aliishia kidato cha pili kutokana na uchumi wa wazazi kuwa mbaya, bado alijifunza kilimo.Gitonga anafafanua kuwa, mwaka 2001 wazazi wake walimwoza mke ambaye pia alikuwa akipenda kilimo hivyo wakiwa pamoja waliendeleza kilimo cha mahindi, miraa na karanga kwa ajili ya familia.

Hata hivyo, mwaka 2003 mke huyo alimtoroka na kumwacha peke yake hali iliyompelekea kujiunga na kikundi cha muziki mjini Meru alikokuwa mpigaji mzuri wa gitaa.

“Kazi hii ilinipatia kipato kikubwa na baadaye nikaamua kuoa mke mwingine kwa jina Imelda ambaye naishi naye mpaka sasa na tumejaliwa watoto wanne,” alisema.

Gitonga anaeleza kuwa, kazi ya upigaji gitaa ilipungua hivyo maisha nayo yakaanza kuwa magumu. Kwa msaada wa rafiki yake mmoja eneo la Nkubu, alianza tena kulima viazi na ndizi na maisha yake yakawa mazuri kama awali. Alihofia kuwa mke wake angemtoroka kama alivyofanya yule wa awali.

“Baada ya kuanza maisha Nkubu, tuliendeleza shughuli za kilimo ambapo tulianza kulima ndizi, mboga za aina mbalimbali, na kufuga kuku. Tuliweza pia kutotolesha mayai kwa kutumia mashine, lakini tukashindwa kuendeleza ufugaji huu kutokana na mayai mengi kutoanguliwa,” aliongeza.

Gitonga anaeleza kuwa, mradi wa mboga uliweza kuwaingizia kipato, kwani waliweza kuzalisha na kuuza kwa majirani na katika masoko ya Chogoria, Meru na Nkubu. Hapo ndipo alipopata pesa za kununua kipande cha ardhi nusu ekari katika kijiji cha Ma Acre, Kaunti ya Kiambu anakoendeleza kilimo chake hadi leo.

Alinunua ardhi hiyo kwa Sh400,000 mwaka 2010Yeye na mkewe wanaendeleza kilimo na ufugaji huko. Wamejipanga kuotesha mboga nyingi kipindi cha masika ili waweze kuuza kwa wingi kwani kutakuwa na soko kutokana na kugundua kuwa wakati huo watu wengi hawaoteshi mboga.

“Si mboga tu, pia tunalima ndizi, maharagwe na nduma na tuko kwenye maandalizi ya shamba kwa ajili ya upanzi japo tumekodisha ardhi nyinginezo eneo jirani ambapo tunakuza mimea tofauti. Pia, tumeanza kufuga kuku wachache wa nyama kwa ajili ya kuuza na kujiongezea kipato pamoja na kupata mbolea” alisema.