Makala

AKILIMALI: Utaalamu wa kukuza karoti zitakazovutia wengi sokoni

August 8th, 2019 3 min read

Na RICHARD MAOSII

KAROTI ni zao la mbogamboga ambalo aghalabu hupatikana ndani ya mchanga kwenye maeneo yenye miinuko na baridi ya kadri baina ya nyuzijoto 15-21.

Ubora wake unaweza kuchangiwa na upatikanaji wa kiwango sahihi cha madini na unyevu, viungo muhimu ambavyo husaidia kuongeza ladha nzuri na rangi iliyokolea.

Mchanga wa mfinyanzi sio sahihi kukuza karoti kwa sababu huyafanya maji kutuama, kwa upande mwingine ule tifutifu unaopitiza maji kwa urahisi ndio unashauriwa kutumika.

Meneja wa Tumor Hill Farm katika kaunti ya Nyandarua Philip King’ori anasema taasisi yao ilianzisha shamba la kukuza karoti kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya shirika lao.

Aidha waliwekeza katika kilimo cha karoti ili kufanya majaribio ya kitaalam, muradi wawasaidie wakulima wadogo wadogowadogo kutoka Ol-Kalou, Nakuru, Molo na Dundori kujifunza mbinu sahihi za kukuza karoti za kisasa zinazochukua miezi mitatu kukua.

Walilenga kupunguza gharama kubwa ya kununua karoti kutoka kwenye soko la nje ili watumie faida itakayopatikana kufanyia mambo mengine muhimu kama vile kuwekeza kwenye kilimo.

Anaeleza Akilimali kuwa kilo moja ya karoti huwa ni Sh70 msimu ukiwa mzuri lakini wakati mwingine, inaweza kuteremka hadi 50 karoti zikiwa zimejaa sokoni.

Meneja wa kilimo kutoka Tumor Hill Farm, Nyandarua aonyesha baadhi ya mazao ya karoti wakati wa mazungumzo na Akilimali. Picha/ Richard Maosi

Anasema shamba linafaa kutayarishwa mapema kwa kutumia trekta au fahali wanaokokota plau na kulima kina kirefu cha mchanga, wa sentimita 30-45 na kufanya matuta yanayoweza kurahisisha upitaji wa maji na hewa safi.

King’ori anahimiza kuwa mbegu bora zinaweza kubainika kutokana na harufu maalum inayotumika kutathmini ufaafu wake, na endapo mbegu hazitoi harufu yeyote huenda zimepoteza ubora wake.

“Mtawanyiko mzuri wa mbegu unahitajika wakati wa kupanda ili kutoa nafasi ya mbegu kuota kwa wakati unaostahili,” King’ori alisema.

Alieleza kuwa shamba linafaa kuandaliwa vyema kwa kuondoa magugu, ili kuhakikisha kuwa mizizi, maji na hewa safi zinapenya vyema baina ya udongo ili karoti ziwe na afya ya kutosha.

Anasema endapo hili litazingatiwa basi maji hayatatuama, na karoti hazitaoza wala kuchukua muda mrefu kuliko ule uliotarajiwa kukua. Ikumbukwe kuwa mazingira ya kukuza karoti yanahitaji udongo usiokuwa na asidi inayozidi PH4.

Kama mimea mingine inayooteshwa kwa njia ya kawaida, mbegu mojamoja hutiwa katika mashimo na mkulima ajizatiti kufanya matuta, na inashauriwa kuwa mkulima asikuze kwanza miche kisha akahamisha kwa sababu mizizi yake huwa ni dhaifu.

“Katika hatua za mwanzoni mkulima anashauriwa kumwagilia miche maji ili kufanikisha mimea midogo kupata unyevu wa kutosha kabla haijakomaa,” aliongezea.

Alisema mimea inafaa kumwagiliwa maji kila wakati asubuhi na mchana, na kuondoa magugu yanayokuwa baina ya mimea ili karoti zisipate ushindani wa kuwania virutubishi.

King’oria anasema ikumbukwe kuwa majani ya karoti yanafaa kupunguzwa kila wakati, mara ya kwanza ni wakati ambapo huwa zimetimu wiki mbili na idadi ya majani, zinazosalia zinafaa kuwa kidogo na mabaki hayo yanaweza kutumika kama chakula kwa mifugo au kiungo muhimu katika lishe ya binadamu.

Aidha, mkulima atahitajika kutumia chombo safi wakati wa kupunguza majani, ili kupunguza maambukizi ya maradhi kutoka kwa karoti moja hadi nyingine.

Hata hivyo licha ya karoti kufanya vyema katika maeneo ya miinuko kama Nyandarua, King’ori anasema inafaa kulindwa dhidi ya maradhi ya kuambukizana, yanayosababishwa na viini vya bakteria.

Wakati mwingi maradhi yanayoikabili karoti husababishwa na fangasi ambayo inaweza kufanya mimea ishindwe kumea na wakati mwingine kukauka hususan mizizi inapokauka.

“Cha msingi ni mkulima kuhakikisha kuwa anatumia mbegu safi na sahihi ambazo zimeidhinishwa na serikali ili kupunguza hasara wakati wa mavuno,” akasema.

Samadi shambani

Mbolea za asilia kama samadi zinaweza kumwagwa shambani ijapo sio mara kwa mara kwa sababu mbolea nyingi zinaweza kuchoma mimea ya mkulima.

King’ori alieleza kuwa baada ya miezi mitatu, muradi hali ya anga, mbolea na mbinu sahihi ya ukulima, mimea ya mkulima inafaa kuwa tayari kwa ajili ya mauzo.

Zao la karoti hufanya vyema wakati wa mvua nyingi kati ya Aprili na Septemba wakati ambapo mvua ni nyingi na baridi, lakini bei yake hupanda majira ya kiangazi wakati ambapo kupatikana kwa bidhaa hii huwa si rahisi.

King’ori alisema kuwa watu wanashauriwa kula karoti kwa wingi ili kuimarisha kiwango cha macho kuona vizuri hasa wakati wa usiku, aidha anasema juisi ya karoti inaweza kuwa mwafaka zaidi kwa sababu ya ongezeko la virutubishi muhimu vilivyokolea.

Aidha husaidia kufanya seli za binadamu ziendelee kuwa changa ili zisizeeke haraka,na kumfanya mtumiaji abakie kuwa mchanga kwa kuifanya ngozi yake iwe changa na laini.

“Karoti husaidia kupunguza shinikizo la damu mwilini kwa sababu ni chanzo cha madini muhimu kama patassium yanayoweza kusaidia katika ufunguzi wa mirija ya kupitisha damu,” akasema.