Makala

AKILIMALI: Utapata faida tele ukijitosa katika kilimo cha uzalishaji machungwa na ndimu kuegemea upandikizaji

December 5th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na CORNELIUS MUTISYA

NI mwendo wa saa mbili asubuhi. Hali ya hewa ni shwari kabisa huku umande ukiendelea kuyeyuka mithili ya barafu msimu wa kiangazi.

Akilimali inafika katika boma la mzee mmoja na kumpata akijiandaa kwenda shambani sawa na wakazi wengine wa kijiji cha Kaliluni, eneobunge la Kathiani, Kaunti ya Machakos.

Bw Sammy Muinde ni mkulima maarufu ambaye hukuza aina mbalimbali ya mimea. Hata hivyo, anavuma mno kutokana na kilimo cha machungwa ya kupandikiza (grafted oranges) na mmea wa ndimu.

Anasema ni fani hii ya kilimo iliyomfanya kujulikana ndani ya nje ya eneo hilo ikizangatiwa kuwa yeye ndiye mtu wa kwanza kuanza kukuza machungwa kupitia njia hii ya kisasa na yenye thamani kubwa.

Lakini mbona mkulima huyu akaamua kupanda machungwa ya kupandikiza?

Mzee Muinde, 65, anafanya uamuzi huo kutokana na sababu kwamba aina hiyo ya machungwa hukomaa kwa haraka tofauti na machungwa ya kawaida.

Kwa wastani machangwa ya kupandikiza huwa tayari kuvunwa baada ya miaka miwili au miaka mitatu. Hii ni tofauti na yale ya kawaida ambayo hukomaa baada ya miaka mitano, anasema.

Isitoshe, machungwa ya kupandikizwa hupendwa sana na wateja ikilinganishwa na yale ya kawaida kwa sababu huwa matamu mno, anaongeza mkulima huyu.

Katika shamba lake la ukubwa wa ekari moja Bw Muinde ana miti 400 ya aina mbili ya machungwa. Sehemu moja ya shamba (ukubwa wa robo ekari) amepanda machungwa ya Valencia ambayo hufanya vizuri katika hali ya anga yenye joto na kiwango fulani cha ukavu.

Na katika sehemu iliyosalia Bw Muinde amepanda machungwa aina ya Washington Navel ambayo huwa hayana mbegu, yana maji mengi na ni matamu zaidi.

Kila mti wa mmea wa machungwa huzalisha kati ya matunda 120 na 150 katika msimu mmoja ambao ni kati ya mwezi Aprili hadi mwezi Novemba kila mwaka, anasema.

Kulingana na wataalamu wa kilimo cha matunda (horticulture) machungwa ambayo yamepandwa kwa njia ya kawaida huzalisha kati ya matunda 60 na 70 kila mwaka. Yanazalisha matunda yenye mbegu nyingi na hayana utamu yakilinganishwa na machungwa ambayo yamependikizwa na mdimu.

Bw Muinde, anasema kuwa katika msimu mmoja anaweza kuvuna tani 4.5 ya machungwa kutoka shambani.

“Kwa wastani, mimi huuza kilo moja ya machungwa kwa Sh50 kwa wale ambao wanunua kwa bei ya jumla na Sh70 kwa wateja wanaonunua kwa bei ya rejareja, anasema.

Elimu ya sekondari

Mzee Muinde anasema alianza kilimo baada ya kukamilisha masomo katika kiwango cha shule ya upili zama hizo.

Baadaye alijiunga na taasisi moja ya kilimo eneo la Eldama Ravine na akafanya kazi katika mashamba makubwa maeneo mengi nchini kama meneja wa kilimo.

Mnamo 1998, alihamia kwa masomo zaidi na huko ndiko alijifunza utalaamu wa kilimo cha kupandikiza.

“Niliporejea nchini niliamua kutumia tajriba na haiba yangu katika fani ya kilimo ili kuwafaa watu wa eneo ninakotoka na pia ili kuitunza familia yangu baada ya kuafikiana na mke wangu” asema mzee huyu mcheshi.

Siku hizo mzee huyu mchapa kazi amekuwa akitembelewa na wakulima wa kila tabaka ili awafunze mbinu faafu za kuboresha na kuimarisha kilimo chao, na hasa kilimo cha matunda ya kupandikiza.

“Nimekuwa nikipokea wageni wengi kila siku ili niwafunze machache ninayoyafahamu kuhusiana na kilimo cha zao la matunda ya kupandikiza ambalo ni adimu mno maeneo haya,” asema Bw Muinde.