Makala

AKILIMALI: Uuzaji samaki wawezesha mjane kujijengea ploti

November 26th, 2020 2 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

BIASHARA ya kuuza samaki huonekana kawaida wa watu wengi lakini kwake Bi Consolata Achieng’ ni kazi yenye thamani.

Kwa zaidi ya miaka 15, Bi Achieng’ amekuwa akiuza aina mbalimbali ya samaki, kazi ambayo imemsaidia kuwalea wanawe baada ya kifo cha mumewe mapema 2011.

Kabla ya kuanza biashara yake mwenyewe, alikuwa ameajiriwa na mwanamke mmoja ambaye alimuuzia samaki na kupokea malipo kila siku, kulingana na kazi yake.

“Niliajiriwa kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya kuanza biashara yangu mwenyewe. Wakati huo, nilipata changamoto za mtaji na ikanibidi ninyenyekee huku nikijifunza maswala ya biashara,” akasema Bi Achieng’.

Kabla ya kuhamia Nakuru, Achieng’ aliishi Kisumu na wakati wa kazi hiyo, aliweza kutambua sehemu mbalimbali za kuagiza samaki kwa bei nafuu.

“Licha ya kwamba nilikuwa nimeajiriwa, sikuangalia mshahara tu, ila nilikuwa darasani pia kwani maono yangu ya kumiliki biashara yalisalia akilini mwangu,” akasema Bi Achieng’.

Alipogura kazi hiyo ya kibarua, Bi Achieng’ alisema alianza biashara yake kwa mtaji wa Sh1, 000 pekee, pesa ambazo alichangiwa na marafiki.

Pesa alizolipwa mbeleni likidhi mahitaji madogo ya nyumbani pekee. “Hata ingawa pesa hizo zilikuwa kidogo, wakati huo samaki wa kuagiza walikuwa bei ya chini na ilikuwa rahisi kupata faida. Nilijipa moyo na kukaza kamba,” akasema.

Baada ya mumewe kuaga dunia, Bi Achieng’ alisema hali iligeuka tofauti na maisha yakawa magumu zaidi. Majukumu yote ya nyumbani yalimlimbikizia na akalemewa kusawazisha biashara pamoja na kukimu mahitaji ya nyumbani.

Usaidizi aliopata kutoka kwa mumewe ulikuwa umeisha na ikambidi kujikakamua hata zaidi.

“Mume wangu alipoaga, watoto wetu walikuwa bado wadogo na nikachukua jukumu la kuwasomesha pamoja kukidhi mahitaji mengine kama kuwalisha kupitia biashara hii,” akasema.

Samaki wake, yeye huagiza kutoka maziwa Naivasha na Victoria, katika kaunti ya Kisumu, ambapo husafirishwa kupitia magari ya usafiri wa umma.

Bi Achieng’ huuza samaki kama vile Tilapia, Nile perch (mgogo wazi kwa njia ya mtaani), pamoja na Mad fish.

Samaki hao huletwa wakiwa bado mbichi ambapo huwakausha kwenye jua nyumbani kwake kijijini Asieko, Nakuru Magharibi.

Inapotimu mwendo wa saa kumi jioni, Bi Achieng’ hufika sokoni Soko Mjinga Takriban kilomita tano kutoka nyumbani kwake kwa ajili ya mauzo.

“Nauza samaki wakiwa wamekaangwa kwa mafuta au wakiwa freshi ukilingana na matakwa ya mteja,” akasema.

Samaki wadogo huuzwa kati ya Sh100 na Sh250 na wale wakubwa kati ya Sh300 na Sh450.

Kwa siku moja, Bi Achieng’ huuza kati ya samaki 40 na 50 au 60 wakati biashara ni nzuri.

“Faida yangu huwa tofauti kila siku kwani hutegemea nimeuza samaki wangapi. Huwa ninapata faida ya kati ya Sh5, 000 na Sh6, 000,” akasema.

Alifichua kuwa biashara hiyo imemwezesha kuweka akiba ambayo sasa hivi imejenga nyumba tano za kukodisha katika sehemu ya kando ya nyumba yake.

“Nilipojenga nyumba za kwanza mbili za kukodisha, sikutumia hela zingine ila zile zilizoweka akiba kwa muda. Nilipotaka kuongeza nyumba zaidi ndipo nilichukua mkopo katika benki na ninaendelea kulipa,” akasema.

Hata hivyo, Bi Achieng’ alisema amepitia changamoto nyingi kwenye biashara hiyo ikiwemo kupotea mzigo wa samaki wakati anapoagiza.

Mara si moja, amefika katika stendi ya magari kuchukua mzigo wake na kupata haupo licha kulipia maelfu ya pesa.

Aidha, wakati mwingine biashara huwa mbovu na kumsababishia hasara ya hali ya juu.

“Wakati fulani unapata kuwa wateja ni wachache na samaki ni wengi. Hapo huwa nakadiria hasara kubwa kwa kulazimika kutengeneza samaki hao kuwa kitoweo nyumbani,” akasema.

Changamoto nyingine Bi Achieng’ alisema ni kuchukua ni kuagiza mzigo kabla ya kufanya malipo na kisha mauzo yanakuwa ya kiwango cha chini. Wakati mwingi amelazimika kulipia mizigo kutumia pesa zake mwenyewe haswa kwa wafanyabiashara wa Kisumu ambapo samaki huwa bei ghali.